IMF kuipatia Tanzania Sh1.3 trilioni kupambana na Corona

September 8, 2021 11:24 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Fedha hizo zitatumika kukabiliana na athari za ugonjwa huo.
  • Zitasaidia kuinua uchumi na kuimarisha shughuli za maendeleo. 

Dar es Salaam. Shirika la Fedha Duniani (IMF) limeidhinisha kuipatia Tanzania mkopo wa dharura wa Dola za Marekani milioni 567.25 (Sh1.3 trilioni) kwa ajili ya kukabiliana na athari za ugonjwa wa Corona (Uviko-19).

Taarifa ya IMF iliyotolewa Septemba 7 mwaka huu imesema bodi ya shirika hilo imeidhinisha kutolewa kwa kiasi hicho cha fedha ambapo kitaisaidia Tanzania katika kuhimili mahitaji yatokanayo na janga la Uviko-19.

IMF imeeleza kuwa uchumi wa Tanzania ulitikisika  kutokana na athari za Uviko-19, hivyo msaada wa kifedha ni muhimu kuurejesha katika hali ya kawaida.

“Uchumi umeripotiwa kukua kwa asilimia 4.8 mwaka 2020 na ukuaji huo unaweza kubaki katika kiwango hicho mwaka 2021,” imeeleza IMF katika taarifa hiyo. 

Shirika hilo limeeleza kuwa Tanzania inatahitaji usawa wa malipo wa asilimia 1.5 ya pato lake la ndani (GDP) wakati mamlaka zikitekeleza mipango ya kujikwamua katika athari za janga hilo na kuhakikisha uchumi unaimarika wakati huu wa wimbi la tatu Uviko-19.

“Janga la Uviko-19 limeathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa Tanzania na afya na ustawi wa watu wake….ongezeko la umaskini na kuathirika kwa sekta ya ajira,” amesema Kaimu Mtendaji Mkuu na Mwenyekiti wa Bodi ya IMF, Bo Li.

Amesema hali hiyo inaiweka nchi katika hatari kwa sababu deni la ndani na nje linaongezeka kutokana na athari za Uviko-19 hasa baada ya kupungua kwa shughuli za utalii.

Fedha hizo zilizotolewa na IMF zitatumia kuimarisha sekta ya afya kwa kuongeza kasi ya utoaji chanjo ya Uviko-19,  uboreshaji wa sera za fedha ili kuendana na hali ya wakati huu na kuinua sekta isiyo rasmi ambayo imeajiri Watanzania wengi.

Hata hivyo, shirika hilo limesema lingependa kuona fedha hizo zinatumiwa vizuri kwa kuzingatiwa uwajibikaji na uwazi ili zilete matokeo yaliyokusudiwa ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania. 

Tanzania imepata mkopo huo baada ya kukamilisha mambo muhimu ikiwemo utoaji wa takwimu kuhusu maambukizi ya virusi vya Corona ambapo tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani Machi mwaka huu Tanzania ilianza kutoa tena takwimu hizo hadharani.

Hadi kufikia leo Septemba 8, Tanzania imerekodi visa vya Uviko-19 1,367 kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Machi 2020 Tanznaia iliiomba IMF mkopo huo wa dharura kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo bila mafanikio lakini mwaka mmoja baadaye Tanzania ilihuisha tena ombi hilo.

Mwakilishi mkazi wa IMF nchini Tanzania, Jens Reinke mwezi Juni mwaka huu aliviambia vyombo vya habari vya kimataifa kuwa moja ya vigezo vya utoaji wa mkopo wa aina hiyo ni pamoja na takwimu muhimu kuhusu Covid 19 ili kujua hali halisi ya maambukizi ya ugonjwa huo ikoje nchini.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW