Polisi yamkamata aliyetangaza TikTok  kumuuza mtoto Sh1.6 milioni

January 7, 2025 1:12 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Mtuhumiwa adai alifanya hivyo kujipatia umaarufu mtandaoni 
  • Huenda akalipa faini isiyopungua Sh 5 milioni au kifungo kisichopungua miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limemkamata John Isaya (21) dereva wa bajaji na Mkazi wa Mtaa wa Bukala wilayani Sengerema kwa tuhuma za kutengeneza na kusambaza picha mjongeo kwenye mitandao ya kijamii (Tiktok) akitangaza kumuuza mtoto wake kwa Sh1.6 milioni kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza Wilbroad Mutafungwa aliyekuwa akizungumza na wanahabari  jana Januari 6, 2025 amesema ukamataji wa mtuhumiwa huyo umetokana na taarifa iliyotolewa na msemaji wa Jeshi la Polisi David Misiime aliyetaka mtu huyo kutafutwa ili awajibishwe kwa mujibu wa sheria,

“Mtuhumiwa alikamatwa Januari 4, 2025 katika wilaya  ya Sengerema na baada ya kufanya mahojiano alidai tukio hilo ni kutafuta umaarufu kupitia mitandao ya kijamiii,” amesema Mutafungwa.

Aidha, mtuhumiwa amekamatwa ikiwa zimepita siku mbili tangu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Wenye Mahitaji Maamlum  Doroth Gwajima, kulitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha mtu huyo anatafutwa na  kuchukuliwa hatua za kisheria.

Sheria ya Makosa ya Mtandao inapiga marufuku kupakia maudhui yenye  matusi ya kibaguzi au unyanyasaji kupitia mtandao ambapo adhabu yake yaweza kuwa faini isiyopungua Sh5 milioni au kifungo kisichopungua miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, linamshikilia Dotto Sita (32) ambaye ni fundi ujenzi mkazi wa mtaa wa Kishiri Jijini Mwanza kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti mtoto wa mwaka mmoja na miezi kumi.

Kwa mujibu wa Mutafungwa mtuhumiwa huyo kwa nyakati tofauti amekuwa akimfanyia ukatili mtoto huyo jambo lilolosababisha hali ya afya ya mtoto  kuwa dhaifu ambapo raia wema walitoa taarifa kwenye dawati la jinsia na watoto ili kufuatilia.

“Kutokana na taarifa hizo, Jeshi la Polisi lilifika eneo la tukio na kumkuta mtuhumiwa akishirikiana na mke wake anaitwa Aneth Mhano(23) wakiwa na jitihada za kumpeleka mtoto huyo hospitali kwa ajili ya kupata matibabu ambapo walifika katika kituo cha afya cha Usumau kilichopo eneo la Kishiri lakini walielekezwa kumpeleka mtoto huyo kwenye zahanati ya Serikali ya Igoma na katika harakati za matibabu mtoto huyo alifariki dunia,” amesema Mutafungwa

Kamanda Mutafungwa amesema mbali na kumkamata mtuhumiwa huyo pia wanamshikilia mama mzazi wa mtoto huyo Aneth Mhano kwa kushindwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi au kwa jirani zake juu ya ukatili aliokuwa akifanyiwa mtoto ili hatua ziweze kuchukuliwa na kuokoa maisha ya mtoto.

Mwili wa mtoto huyo umefanyiwa uchunguzi na umekabidhiwa kwa  baba yake mzazi Emmanuel Daud (28) na ndugu wengine kwa ajili ya mazishi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks