Amana za wateja benki ya DCB zaongezeka kwa asilimia 97.3

May 7, 2019 2:21 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Benki ya DCB yaendelea kupata mafanikio makubwa. Picha|Mtandao.


  • Tangu benki hiyo ianzishwe imefanikiwa kukuza amana za wateja kutoka Sh2 bilioni mwaka 2002 hadi Sh75 bilioni Desemba mwaka jana.
  • Pia mikopo imeongezeka kutoka Sh1 bilioni mwaka 2002 na kufikia Sh90 bilioni Desemba mwaka jana.
  • Yapewa changamoto ya kusogeza huduma kwa wananchi.

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya benki zikishindwa kujiendesha kwa kukosa mtaji, Benki ya Biashara ya Dar es Salaam (DCB) imeendelea kujipatia mafanikio katika ukuzaji wa amana za wateja, mikopo na faida inayopatikana baada ya kodi. 

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya DCB, Godfrey Ndalahwa amesema tangu benki hiyo ianzishwe imefanikiwa kukuza amana za wateja kutoka Sh2 bilioni mwaka 2002 hadi Sh75 bilioni Desemba mwaka jana.

Hiyo ina maana kuwa ndani ya miaka 16 tangu kuanzishwa kwake amana ya wateja imeongezeka kwa asilimia 97.3, jambo lililosaidia kuongezeka kwa kiwango cha mikopo inayotolewa na benki hiyo yenye makao yake jijini Dar es Salaam

“Pia mikopo imeongezeka kutoka Sh1 bilioni mwaka 2002 na kufikia Sh90 bilioni Desemba 2018, faida ikiwa ni Sh17.7 bilioni 17.7 baada ya kodi,” amesema Ndalahwa alipokutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jijini Dodoma jana.

Ndalahwa amesema pia katika kipindi cha miaka 16 ya utendaji wake, benki hiyo imeshatoa gawio la zaidi ya sh11 bilioni  kwa wanachama wake.

Hata hivyo, DCB bado ina kibarua kigumu cha kujiimarisha zaidi katika kipindi hichi ambacho watu wengi wanazigeukia huduma za kifedha kwa njia ya simu. 

Naye Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameupongeza uongozi benki ya DCB kwa kufanikiwa kubadili muundo kutoka benki ya jamii na kuwa benki ya biashara.

“Benki nyingi za jamii zimekufa baada ya kushidwa kujiendesha lakini ninyi DCB mmeweza kumudu kujiendesha hadi kufikia kuwa benki ya biashara,” amesema Majaliwa.


Zinazohusiana: 


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ameutaka uongozi wa benki hiyo umetakiwa kuimarisha kitengo cha elimu kwa umma ili jamii ifahamu huduma wanazozitoa ikiwemo kutoa elimu juu ya umuhimu wa kufungua akaunti na kurahisisha mazingira ya kutolea huduma kwa wateja.

Waziri Mkuu ameitaka benki hiyo isogeze huduma kwa wananchi hususan maeneo ya pembezoni ambayo bado hayajafikiwa na benki nyingi ili wahakikishiwe usalama pamoja na fedha zao.

Januari 2018, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilifuta leseni za benki tano na kuziweka chini ya mrasimu kwa sababu ya kukumbwa na matatizo ya kifedha.

Benki hizo ni Covenant Bank for Women, Efatha Bank Limited, Njombe Community Bank Limited, Meru Community Bank Limited, na Kagera Farmers’ Cooperative Bank Limited.

Mei 17, 2018, benki za Twiga Bancorp (Twiga Bancorp Limited) na benki ya Posta Tanzania (TPB) ziliunganishwa na kuwa benki moja kutokana na Twiga Bancorp kuwa na upungufu mkubwa wa mtaji.

Enable Notifications OK No thanks