Ahueni: Urahisi upimaji Uviko-19 waimarisha biashara mpaka wa Tanzania, Kenya

November 2, 2021 8:35 am · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni katika mpaka wa Horohoro mkoani Tanga.
  • Madereva watumia siku moja kupima na kupata majibu.
  • Shughuli za biashara, usafirishaji zarejea na kuimarika.

Tanga. Ni saa mbili kamili asubuhi, anatarajia kuanza safari ya kupeleka mzigo wa mahindi upande wa Kenya kama hesabu zake za siku.

Ni miongoni mwa madereva wanaoshuhudia kuimarika kwa shughuli za usafirishaji na upimaji wa virusi vya Uviko-19 katika mpaka wa Horohoro tofauti na ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita.

“Sasa hivi mambo yako freshi, siyo kama zamani. Tunavuka bila tatizo lolote,” anasema Mathias Kilau, dereva anayesafirisha mahindi kutoka mkoani Rukwa kwenda Kenya kupitia mpaka huo uliopo Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga. 

Mpaka huo unaotenganisha Tanzania na Kenya ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika na janga la Corona (Uviko-19) hasa katika sekta ya usafirishaji na biashara. 

Eneo hilo la Horohoro huwakutanisha watu mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wadogo, madereva, wasafirishaji na watu wanaoishi hapo kwa shughuli mbalimbali za kibiashara.

Mei mwaka 2020 mpaka huo ulifungwa  ikiwa ni hatua ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Uviko-19 baina ya nchi hizo, jambo liloathiri shughuli za biashara.

Watu walipoteza ajira, bidhaa ziliharibika huku malori yakisitisha shughuli zake kusubiri hali ya Uviko-19 iimarike.

Itifaki ya Umoja wa forodha wa Afrika Mashariki ya mwaka 2004 ibara ya 22 kipengele (c) inaeleza kuwa vizuizi vya mpakani baina ya nchi vinaweza kuwekwa kwa mambo yanayoathiri maisha ya binadamu, mazingira na maliasili, usalama wa umma, afya ya umma au maadili ya umma.

Msongamano wa malori umepungua katika mpaka wa Horohoro unaotenganisha Tanzania na Kenya baada ya kurahisishwa kwa upimaji wa Uviko-19. Picha| Gift Mijoe.

Baadhi ya madereva wa malori wameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kwa sasa wanapita bila usumbufu mpakani hapo kwa sababu vikwazo vya usafiri vimelegezwa na nchi zote mbili zimeweka utaratibu mzuri wa kupima Uviko-19.

“Hii ni tripu yangu ya tano ndani ya wiki hii. Kipindi cha mgogoro hata tulikuwa tunawaza tunafanya nini maana kwa wiki unaweza kushangaa ukibahatika sana una tripu moja, kwa hiyo kwa kweli tunakwenda sawa sasa,” anasema Paul Charles mfanyabiashara anaesafirisha mahindi kutoka mkoani Mbeya kwenda Mombasa.

Charles anasema wakati Uviko-19 umechachamaa mwaka jana, alikuwa anatumia siku tatu kuvuka mpaka huo kuelekea Kenya, jambo lililosababisha kupunguza kasi ya ufanyaji biashara na mapato yake.

Mbali na changamoto ya kiuchumi pia muda wa kukaa mpakani uliongeza gharama za kujikimu kwa madereva hali iliyosababisha vipato vyao kuyumba.

“Tulikua tumepanga kukaa siku moja mpaka mbili, ilivyokua inatokea tunakaa mpaka siku nne ilikua hatari maana pesa tuliyotegemea kuhudumia familia unakuta inatumika kujikimu,” anasema Mwarami Yahya dereva  wa roli mpakani hapo. 


Mambo yarahisishwa

Hata hivyo, baada ya tahadhari dhidi ya ugonjwa huo kuimarishwa ikiwemo utoaji chanjo na vipimo vya mpakani, shughuli za kibiashara zimeanza kuimarika kwa pande zote mbili. 

Kwa sasa, madereva na wasafirishaji wa pande zote mbili wamerahisishiwa mchakato wa upimaji wa Uviko-19 baada ya uanzishwaji wa kituo cha pamoja cha mpakani (One Stop Border Post (OSBP)) ambacho kinaruhusu madereva kuingia na kutoka baada ya kupata kipimo katika nchi yoyote kati ya Tanzania na Kenya.

Utaratibu huo pia umetatua changamoto ya madereva kukaa mpakani kwa zaidi ya siku tatu wakisubiri majibu badala yake inachukua siku moja kufanya vipimo na kupata majibu.

“Kiukweli hali siyo ile ya zamani. Sasa hivi kwanza tunapata majibu kwa wakati, lakini una uwezo wa kutoka na kuingia mpaka siku 14 zipite. Hii imekua afadhali sana kwetu sisi,” anasema Hassan Hood, dereva anayesafirisha mahindi kutoka Rukwa kwenda Kenya. 

Mwongozo wa Serikali kwa wasafiri namba 8 ulioanza kutumika Septemba 19, 2021, umerahisisha kazi ya kupima Uviko-19 mpakani ambapo hakuna gharama zozote za kupata kipimo cha haraka (C19RAT) kwa madereva wanaopita katika mipaka ya Tanzania.

Wakala wa kuidhinisha mizigo (Clearing and forwarding agent) mpakani hapo, Stanley Magoda ameiambia www.nukta.co.tz kuwa kutokana na takwimu alizonazo,  akilinganisha kipindi kilichopita na sasa, utaratibu wa uvukaji umerahisishwa na hali ya biashara inaonekana kutengamaa.

“Sasa hivi walau tunaona biashara inasonga, tulikaa muda mrefu hapa hatuoni pesa,” anasema Stanley akionekana mwenye matumaini makubwa kuhusu kesho yake.

Malori yakisubiri kukaguliwa katika mpaka wa Tanzania na Kenya wa Horohoro mkoani Tanga. Picha| Gift Mijoe.

Anasema Kundi kubwa lililoathirika kabla ya hali kutengamaa, ni wafanyabiashara wadogo wadogo waliokuwa wakitegemea kusafirisha mizigo kwa wakati kabla haijaharibika.

“Sasa hivi naona kidogo kuna uafadhali japo siyo sana ila mwanga upo,” anasema Magoda.

Kenya inashika nafasi ya tano kwa uwekezaji nchini Tanzania ikitanguliwa na mataifa mengine kutoka nje lakini ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki Kenya ni ya kwanza. 

Kenya imewekeza miradi 513 yenye thamani ya Dola za Marekani 1.7 bilioni (Sh3.9 trilioni) ambayo imetoa ajira zipatazo 51,000 za Watanzania. 

Aidha, zipo kampuni 30 za Tanzania ambazo zimewekeza mtaji ndani ya Kenya wenye thamani ya Ksh19.33 bilioni (Sh410.8 bilioni) na kutoa ajira kwa watu 2,640.

Ushirikiano wa nchi hizo mbili katika shughuli za kibiashara una umuhimu mkubwa kwa na vikwazo vyovyote vile vinaweza kupunguza kasi ya wanawanchi kujiletea maendeleo.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof Michael Ndanshau anasema Uviko-19 umechangia kuleta migongano ya kidiplomasia katika nchi mbalimbali hivyo mazungumzo na busara ndiyo suluhu ya kutatua changamoto kama hizo hasa zinazohusu biashara ya mipakani.

“Njia ya msingi kuzingatia kuondoa migogoro baina ya nchi ni kwa kuingia makubaliano rasmi kwa njia ya mikataba inayoweza kuzuia kutofautiana mara kwa mara,” anasema Prof Ndanshau.

Kwa sasa, Serikali za Tanzania na Kenya zinaendelea na kampeni ya kuchanja chanjo ya Uviko-19 kwa raia wake ili kuwakinga na maradhi hayo huku elimu ya kuchukua tahadhari ya kunawa mikono, kuvaa barakoa nayo ikipewa kipaumbele.

Hatua hiyo inasaidia kupunguza maambukizi kwenye jamii huku shughuli za kibiashara na usafirishaji zikiimarika. 

Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW