Madereva wa malori walalamika kukwama mpakani Kenya

May 14, 2022 6:08 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wasema wanatumia siku 14 hadi 21 kuingia Kenya kupitia mpaka wa Horohoro.
  • Sababu kuu ni Kenya kutoanza kutumia kutumia mfumo wa pamoja wa huduma ya forodha.
  • Serikali yaahidi kumaliza changamoto hiyo kwa mazungumzo.

Dar es Salaam. Baadhi ya madereva wa malori wa Tanzania wanaosafirisha mizigo kwenda Kenya wamelalamikia kutumia muda mrefu kupata vibali vya kuvuka mpaka wa Horohoro, jambo linaloathiri ufanisi wa biashara wa nchi hizo mbili.

Mpaka wa Horohoro uliopo mkoani Tanga ni kiungo muhimu cha usafirishaji bidhaa na watu kati ya nchi hizo mbili za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Baadhi ya madereva wanaotumia mpaka huo kuingia Kenya wamesema  wanapata usumbufu mkubwa kwa sababu wanatumia muda mrefu unaokadiriwa kufikia siku 14 hadi 21 kuvuka mpaka wa Horohoro kwenda nchini Kenya.

Kuchelewa kuvuka mpaka kunawaletea matatizo ikiwemo kutumia gharama kubwa zisizolingana na posho za safari wanazopewa na waajiri wao, lakini pia baadhi ya bidhaa zinaharibika kabla ya kuvuka mpaka.

Madereva hao waliokuwa wakitoa madai yao kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba jana Mei 13, 2022 wamesema wenzao kutoka Kenya wanaoingia Tanzania wanatumia siku zisizozidi 3 kuvuka mpaka huo.

Wamedai utofauti huo wa muda wa kuvuka mpaka unawapunguzia ushindani wa kibiashara. 

Itifaki ya Umoja wa forodha wa Afrika Mashariki ya mwaka 2004 inazitaka nchi wanachama wa EAC kuondoa vikwazo vya kibiashara ikiwemo kuwa na kituo cha pamoja cha mpakani (One Stop Border Post (OSBP)) ili kurahisisha shughuli za usafirishaji wa bidhaa na watu kutoka nchi moja kwenda nyingine.


Malori yakisubiri kukaguliwa katika mpaka wa Tanzania na Kenya wa Horohoro mkoani Tanga Oktoba 2021. Picha| Gift Mijoe.

Serikali yaingilia kati

Hata hivyo, Waziri Dk Nchemba amesema kuwa Serikali itawasiliana na mamlaka za Kenya ili kutatua changamoto ya malori ya mizigo yanayovuka kupeleka bidhaa nchini humo kutumia muda mrefu kupata vibali vya kuvuka mpaka wa Horohoro-kuingia Kenya.

Waziri huyo aliyekuwa njiani kwenda Mombasa, Kenya kwenye Mkutano wa mawaziri wa fedha wa nchi za EAC amebaini kuwa ucheleshwaji wa huduma ya forodha kwa Kenya unatokana na nchi hiyo kutoanza kutumia  Mfumo wa Pamoja wa Huduma ya Forodha (Single Custom Territory) kama walivyokubaliana.

“Magari ya Kenya hayapati changamoto hiyo ya foleni kwa kuwa tayari Tanzania wanatumia mfumo huo ambapo mizigo yote ya Kenya hupata vibali ikiwa huko huko nchini Kenya, kabla ya kufika katika mpaka huo wa Horohoro na malori kupita bila tatizo,” amesema Dk Nchemba kupitia taarifa ya Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja.

Amesema kuwa atawasiliana na waziri mwenzake wa fedha wa Kenya ili kuanza kutekeleza makubaliano ya kuweka mfumo huo wa pamoja na forodha kwa kuwapeleka watumishi wa nchi hiyo upande wa Tanzania ili kuharakisha usafiri na usafirishaji wa mizigo kutoka Tanzania.

Hatua hiyo itasaidia kuwaondolea adha wafanyabiashara na madereva wanaotumia mpaka huo kufanya biashara zao.


Soma zaidi:


Ushirikiano wa nchi hizo mbili katika shughuli za kibiashara una umuhimu mkubwa kwa na vikwazo vyovyote vile vinaweza kupunguza kasi ya wanawanchi kujiletea maendeleo.

Kenya inashika nafasi ya tano kwa uwekezaji nchini Tanzania ikitanguliwa na mataifa mengine kutoka nje lakini ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki Kenya ni ya kwanza. 

Kenya imewekeza miradi 513 yenye thamani ya Dola za Marekani 1.7 bilioni (Sh3.9 trilioni) ambayo imetoa ajira zipatazo 51,000 za Watanzania. 

Aidha, zipo kampuni 30 za Tanzania ambazo zimewekeza mtaji ndani ya Kenya wenye thamani ya Ksh19.33 bilioni (Sh410.8 bilioni) na kutoa ajira kwa watu 2,640.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW