Tanzania yazindua mfuko wa Sh2 bilioni kusaidia watengeneza maudhui

January 30, 2026 3:12 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Watakao nufaika ni watengenezaji maudhui katika sekta mbalimbali zikiwemo utalii, michezo, maendeleo ya jamii, muziki, filamu.
  • Pamoja na sanaa nyingine za ubunifu, pia watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuendesha shughuli zao za kiuchumi.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imezindua mfuko wa Sh2 bilioni kwa lengo la kuwawezesha watengeneza maudhui ya kidijitali nchini, ikiwa ni hatua ya kuimarisha uchumi wa ubunifu na matumizi ya teknolojia ya kidijitali.

Akizungumza Januari 29, 2026, jijini Dodoma, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema mfuko huo unalenga kuwasaidia wabunifu wa maudhui kuboresha ubora wa kazi zao na kuwawezesha kujipatia kipato endelevu kupitia majukwaa ya kidijitali.

“Nchi yetu kwa wingi wa vijana tuliokuwa nao, lazima iwepo mikakati mbadala ya kuwezesha na kutengeneza fursa ili vijana hao waweze kupiga hatua,” amesema Makonda.

Makonda amefafanua kuwa mpango huo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Rais Samia kukuza sekta ya ubunifu, hususan kwa vijana wanaotumia teknolojia za kidijitali kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.

Kwa mujibu wa waziri  watakaonufaika ni watengeneza maudhui katika sekta mbalimbali zikiwemo utalii, michezo, maendeleo ya jamii, muziki, filamu pamoja na sanaa nyingine za ubunifu, na wanaofanya shughuli zao kupitia mitandao ya kijamii kuendesha shughuli zao za kiuchumi.

“Iwe ni Tiktok, iwe ni Instagram, iwe ni Facebook, iwe ni Youtube, iwe ni programu yeyote ambayo unaifanya Serikali imeamua kukuwezesha ili kutimiza ndoto yako,” amefafanua Makonda.

Mpango huo wa Serikali unakuja katika wakati ambao vijana wengi wanakabiliwa na ukosefu wa ajira huku wengi wao wakikimbilia fursa za kidijitali zinazokuja kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia duniani kupitia makampuni kama vile Facebook, Instagram na Tiktok.

Matumizi ya mitandao yaongezeka

Ripoti ya takwimu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya robo ya nne ya mwaka 2025 (Septemba hadi Desemba) inaonyesha kuwa Watanzania milioni 58.1 wamefikiwa na huduma za intaneti. Kati ya hao, milioni 28.5 wanatumia simu janja kuunganishwa na huduma hizo.

Hivyo, ujio wa fursa hiyo ni nafasi muhimu kwa vijana wa kitanzania ambao ni asilimia 34.5 ya watanzania wote kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi 2022 watakaoweza kunufaika na uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi. 

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kimataifa la Takwimu, ‘Data Reportal,’ hadi kufikia mwaka 2025 Facebook ndiyo mtandao wa kijamii unaotumiwa zaidi nchini Tanzania ukiwa na watumiaji milioni 6.79. Hili ni ongezeko la asilimia 19.5 ikilinganishwa na mwaka 2024, ambapo idadi ya watumiaji ilikuwa milioni 5.68. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 9.7 ya Watanzania wote waliopo nchini kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Kwa upande wa Instagram Tanzania ilikuwa na watumiaji milioni 3.7 ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.7 kwa mwaka 2025 huku mitandao kama Linked, X (zamani Twitter) na Messenger watumiaji wake wakiongezeka pia.

Kwa mujibu wa Makonda zoezi la usajili wa waombaji wanaokidhi vigezo utaanza rasmi Januari 30 na kutamatika Februari 15, 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks