Serikali yapendekeza kushusha ada ya leseni za maudhui mtandaoni kwa asilimia 50

August 20, 2021 8:54 am · Medlini
Share
Tweet
Copy Link

Kanuni hizo pia zinakataza kuchapisha au kutangaza habari zinazoingilia faragha ya mtu na utu wa mtu kwa namna yoyote ile au kuchapisha picha au video mtandaoni bila idhini ya wamiliki wa maudhui hayo ikiwa ni moja ya hatua za kulinda hakimiliki za watengeneza maudhui nchini. Picha| Daniel Samson.


  • Inapendekeza kupunguza ada ya leseni ya maudhui ya mtandaoni kutoka Sh1 milioni hadi Sh500,000.
  • Pia ada ya maombi ya leseni na kuhuisha leseni nayo kupungua.
  • Wamiliki wa redio na televisheni za mtandaoni kupata msamaha.

Dar es Salaam. Serikali imependekeza kupunguza ada ya leseni ya maudhui ya mtandaoni kwa asilimia 50, jambo ambalo linaloweza kuwapa ahueni wamiliki wa vyombo vya habari mtandaoni zikiwemo blogu. 

Mabadiliko hayo ya ada yanakusudiwa kufanywa kupitia kanuni za maudhui mtandaoni za mwaka 2020 ambazo ziko chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta namba 306.

Katika rasimu ya mabadiliko ya kanuni hizo ya mwaka 2021 ambayo imetolewa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Serikali inapendekeza kupunguza ada ya leseni ya maudhui ya mtandaoni ya kila mwaka kutoka Sh1 milioni ya awali hadi Sh500,000.

Hiyo ni sawa na punguzo la asilimia 50 au nusu ya ada iliyokuwa inalipwa awali ambayo baadhi ya wadau walikuwa wakiilalamikia kuwa ni kubwa ikilinganishwa na uwezo wa waanzilishi wa vyombo vya habari vya mtandaoni.

Pia katika mabadiliko hayo, Serikali itapunguza ada ya maombi ya leseni hadi Sh50,000 kutoka Sh100,000 ya awali huku ada ya kuhuisha leseni kila baada ya miaka mitatu itapungua hadi 100,000.

Awali, watoa huduma za maudhui walitakiwa kulipa Sh1,000,000 ili kuhuisha leseni zao, sasa wataokoa Sh900,000. 

Ikiwa mabadiliko hayo  ya kanuni za maudhui mtandaoni  yatapita, basi yatawafaidisha zaidi wamiliki wa redio na televisheni za mtandaoni kwa sababu wao watapa msahama na hawatalipa fedha yoyote kuendesha shughuli zao mtandaoni.

Katika kanuni za 2020, wamiliki wa televisheni na redio za mtandaoni walitakiwa kulipa ada ya leseni ya Sh200,000 kila mwaka na Sh200,000 kuhuisha leseni zao kila baada ya miaka mitatu.

Ili kuboresha maudhui na vyombo vya habari vya mtandaoni, Serikali imetoa rasimu ya mabadiliko ya kanuni hizo ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na baadhi ya wadau wa habari na maudhui ya mtandaoni wakieleza kuwa zinaminya uhuru wa vyombo na uhuru wa kujieleza.

Pia, Serikali imewaalika wadau wa habari kutoa maoni katika rasimu ya marekebisho ya kanuni hizo kabla haijazipitisha.

“Maboresho hayo yatazifanya Kanuni hizo ziendane na maendeleo ya teknolojia pamoja na kuongeza wigo wa upatikanaji wa habari kwa wananchi,” ameeleza John Mapepele, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Habari. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW