Ahueni: Bei za mafuta ya petroli zashuka Tanzania

August 7, 2019 8:46 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Bei ya rejareja ya petroli imeshuka kwa Sh160 kwa lita.
  • Wakazi wa Dar es Salaam sasa watanunua lita moja kwa Sh2,151 kutoka Sh2,312 ya Julai.
  • Bei hizo zinaanza kutumia leo, Agosti 7, 2019.
  • Wakazi wa Uvinza (Lugufu) wao ndiyo watanunua petroli kwa bei ya juu kuliko wote chini ikiwa ni Sh2,556 kwa lita.

Dar es Salaam. Watumiaji wa vyombo vya moto sasa watakuwa na ahueni baada ya bei za mafuta mwezi Agosti kushuka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na ilivyokuwa mwezi uliopita ikichangiwa na kuporomoka kwa bei ya nishati katika soko la dunia.

Bei mpya kikomo zilizotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) zinabainisha kuwa bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeshuka kwa Sh160 kwa lita huku ile ya dizeli ikipungua kwa Sh102 kwa lita.

Ahueni hiyo imeenda hadi katika mafuta ya taa ambayo bei yake imeshuka kwa Sh81 kwa lita.

Mbali na mafuta yaliyoingizwa kupitia Dar es Salaam, mafuta yaliyoingiziwa katika Bandari za Mtwara na Tanga nayo yameshuka bei jambo linalowaokoa pia wakazi wa maeneo hayo kutoboa zaidi mifuko yao kununua bidhaa hizo muhimu kwa ajili ya usafiri, viwanda na nishati.

Ewura inaeleza kuwa bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia bandari ya Tanga imepungua kwa Sh134 kwa lita, dizeli imeshuka kwa Sh105 kwa lita na mafuta ya taa nayo yakishuka kwa Sh163 kwa lita. Mafuta hayo hutumiwa na wakazi wa mikoa ya Kaskazini mwa nchi ya Arusha, Tanga, Kilimanjaro, na Manyara.

Wakazi wa mikoa ya Kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma wao nao watashuhudia punguzo la bei za rejareja kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa japo ahueni hiyo ikiwa chini kidogo na ile wanayoipata wenzao wanaotumia mafuta yanayoingiziwa Dar es Salaam na Tanga.

Bei kikomo ya rejareja kwa petroli iliyoingizwa kupitia bandari ya Tanga imeporomoka kwa Sh105 kwa lita huku dizeli nayo ikipungua kwa Sh124 kwa lita.


Soma zaidi: Maumivu:Bei za mafuta zapaa


Taarifa ya Ewura imeeleza kuwa bei hizo mpya zinaanza kutumika kuanzia leo (Agosti 7, 2019) nchini kote.

“Vilevile, ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za petroli, dizeli na mafuta ya taa (yaliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam) zimepungua kwa Sh159.09/lita (sawa na asilimia 7.27) na Sh102.10/lita (sawa na asilimia 4.90) na Shilingi 81.01/lita (sawa na asilimia 3.96), mtawalia,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Nzinyangwa Mchany.

Kutokana na kushuka kwa bei hizo wakazi wa Dar es Salaam sasa bei kikomo ya lita moja ya petroli itakuwa Sh2,153 kutoka Sh2,312 ilivyokuwa Julai mwaka huu.

Wakazi wa Uvinza (Lugufu) wao ndiyo watanunua petroli kwa bei ya juu kuliko wote nchini ikiwa ni Sh2,556 kwa lita kutokana na gharama mbalimbali zikiwemo za usafiri.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...