Ahueni bei ya petroli ikishuka Tanzania

February 2, 2022 8:11 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeshuka kwa Sh21.
  • Dizeli imeongezeka kwa Sh44 kwa lita.
  • Kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia kwachangia hali hiyo.

Dar es Salaam. Watumiaji wa vyombo vya moto sasa watakuwa na ahueni kidogo baada ya bei za mafuta katika baadhi ya maeneo kushuka kwa mwezi Februari ikilinganishwa na ilivyokuwa mwezi uliopita ikichangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia.

Bei mpya kikomo kwa mwezi Februari 2022 zilizotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) zinabainisha kuwa bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeshuka kwa Sh21 kwa lita huku ile ya dizeli ikiongezeka kwa Sh44 kwa lita.

Ahueni hiyo imeenda hadi katika mafuta ya taa ambayo bei yake imeshuka kwa Sh81 kwa lita.

Mbali na mafuta yaliyoingizwa kupitia Dar es Salaam, mafuta yaliyoingiziwa katika Bandari ya Tanga nazo zimeshuka bei jambo linalowaokoa pia wakazi wa maeneo hayo kutoboa zaidi mifuko yao kununua bidhaa hizo muhimu kwa ajili ya usafiri, viwanda na nishati.

Ewura inaeleza kuwa bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia bandari ya Tanga imepungua kwa Sh123 kwa lita na dizeli imeshuka kwa Sh92 kwa lita.

“Kutokana na kuisha kwa mafuta ya taa kwenye matanki ya kuhifadhia yaliyopo Tanga, waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Kaskazini wanashauriwa kuchukua mafuta ya taa kutoka katika bandari ya Dar es Salaam.

“Hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa katika mikoa hiyo itakuwa kulingana na gharama za kupokelea mafuta ya taa kupitia Bandari ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika,” imeeleza taarifa ya Ewura kuhusu bei kikomo za mafuta kwa mwezi Februari 2022. 

Mafuta yanayopitia bandari ya Tanga hutumiwa na wakazi wa mikoa ya Kaskazini mwa nchi ya Arusha, Tanga, Kilimanjaro, na Manyara.


Soma zaidi: 


Kwa Februari 2022, bei za rejareja na jumla kwa bidhaa za mafuta ya  petroli na dizeli kwa Mikoa ya Kusini (Mtwara, Lindi, and Ruvuma) zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la tarehe 5 Januari 2022. 

Hii ni kwa sababu, kwa mwezi Januari 2022 hakuna shehena ya Mafuta iliyopokelewa kupitia bandari ya Mtwara huku watumiaji wa mafuta ya taa wakitakiwa kutumia mafuta yanayopitia bandari ya Dar es Salaam.

“Mabadiliko haya ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia, gharama za usafirishaji (BPS Premium) na thamani ya shilingi ukilinganisha na dola ya kimarekani,” amesema Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje.

Taarifa ya Ewura imeeleza kuwa bei hizo mpya zinaanza kutumika kuanzia leo (Februari 2, 2022) nchini kote.

“Ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za petroli na mafuta ya taa zimepungua kwa Sh21 kwa lita (sawa na asilimia 0.89) na Sh43.80 kwa lita (sawa na asilimia 1.99), mtawalia wakati bei ya jumla ya dizeli imepanda kwa Sh13.20 kwa lita (sawa na asilimia 0.60),” amesema Chibulunje. 

Kutokana na kushuka kwa bei hizo za mafuta, wakazi wa Dar es Salaam sasa bei kikomo ya lita moja ya petroli itakuwa Sh2,480, dizeli (Sh2,338) na mafuta ya taa kwa Sh2,291.

Wakazi wa Uvinza (Lugufu) wao ndiyo watanunua petroli kwa bei ya juu kuliko wote nchini ikiwa ni Sh2,724 kwa lita kutokana na gharama mbalimbali zikiwemo za usafiri.

Enable Notifications OK No thanks