ACT-Wazalendo yataka mfumo uendeshaji Air Tanzania ufumuliwe

April 10, 2023 11:50 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Yasema mfumo wa sasa wa uendeshaji ndio chanzo cha upotevu wa mabilioni.
  • Wapendekeza Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) kurejeshwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kutoka Ofisi ya Rais.
  • Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali CAG aombwa kufanya ukaguzi maalumu wa manunuzi ya ndege ya toka mwaka 2016 kubaini mapungufu.

Chama Cha ACT-Wazalendo kimeitaka Serikali kubadili haraka mfumo wa uendeshaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ili kuliepusha na hasara ambayo imekuwa ikiripotiwa kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.

Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo Zitto Kabwe, amewaeleza wanahabari wakati akiwasilisha uchambuzi wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ( CAG) leo Apirili 10 2023, kuwa mfumo wa sasa unaowalazimu ATCL kukodi ndege kutoka kwa Wakala wa Ndege wa Serikali (TGFA) ndio chanzo cha hasara kwa shirika hilo.

“Mfumo uliopo sasa ATCL haimiliki ndege. Ndege zote zilizonunuliwa na Serikali kwa fedha za walipa kodi zinamilikiwa na TGFA na kukodishwa kwa ATCL. Tunapendekeza ATCL imilikishwe ndege zote inazo kodishiwa kutoka TGFA,” amesema Zitto jijini Dar es Salaam.

Zitto amebainisha kuwa mwaka 2022 ATCL ilitakiwa kuilipa TGFA Sh63 bilioni kama gharama ya ukodishaji ndege, hivyo kuondolewa kwa utaratibu huo kutalipatia ahueni shirika hilo la ndege.

Kwa mujibu wa CAG, kwa mwaka 2021/22 ATCL ilirekodi hasara ya Sh35.23 bilioni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuingia gharama mara mbili ya malipo ya ukodishaji ndege na gharama za matengenezo kwa TGFA ambapo kama zisingekuwepo hasara ingepungua mpaka Sh9.85 bilioni.


Zinazohusiana


​​​​Sababu ya TGFA kumiliki ndege haina mashiko

ACT imesisitiza kuwa licha ya sababu mojawapo za Serikali kuipatia TGFA umiliki wa ndege ni kuepuka kukamatwa kwa ndege za Tanzania kwa sababu ATCL ina madeni mengi bado sababu hiyo  haina mashiko. Zitto amesema ndege za Tanzania zimeshakamatwa mara kadhaa ikiwepo moja inayoendelea kushikiliwa nchini Uholanzi. Mwanahabari Suleiman Msuya wa gazeti la Raia Mwema akiuliza swali wakati wa mkutano kati ya wanahabari na Chama cha ACT-Wazalendo kuhusu uchambuzi wa ripoti ya CAG jijini Dar es Salaam Aprili 10, 2023. Picha|Esau Ng’umbi.

“Ndege zinamilikiwa na Serikali lakini bado  zinakamatwa, yule mkulima alikamata ndege Afrika Kusini, na kuna ndege yetu imekamatwa nchini Uholanzi, kwa hiyo hoja ya Serikali ya kukwepa ndege kukamatwa haina mashiko tena, badala yake waipe ATCL umiliki wa ndege zote wafanye kazi wakiwa na mali,” amesisitiza Zitto.

Hata hivyo, wito huo wa ACT unakuja ikiwa imepita siku moja tu tangu Rais wa Tanzania atengue uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa TGFA Mhandisi John Nzulule kutokana na shutuma kadhaa zilizoibuliwa ikiwemo kuongezwa kwa kiasi cha Dola milioni 50 za Marekani katika ankara ya malipo ya ndege ambazo ni sawa na Sh117.18 bilioni.

Kutokana na hilo, ACT imeitaka Serikali kuirudisha TGFA katika Wizara ya Ujenzi  na Uchukuzi kutoka Ofisi ya Rais ili iwe inafanyiwa ukaguzi na CAG ili kubaini mapungufu yaliyotokea wakati wa ununuzi wa ndege zilizopo hivi sasa.

“Tunaitaka Serikali kuirejesha TGFA kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ili mamlaka ziweze kuisimamia na tunapendekeza CAG afanye ukaguzi maalumu tangu Serikali ilipoanza kununua ndege mwaka 2016, “ amesema Zitto.

Kwa Mujibu wa Zitto Kabwe aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Dk John Magufuli alihamishia TGFA chini ya ofisi ya Rais mwaka 2016 ili kuepuka ukaguzi wa hesabu za manunuzi ya ndege.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW