Maoni mchanganyiko: Serikali ikipiga marufuku wanafunzi chini ya darasa la tano kukaa bwenini
- Yasema utaratibu huo unawanyima fursa watoto kukosa upendo wa wazazi wao na kujengewa maadili mema.
- Makambi ya taaluma nayo yapigwa marufuku
- Baadhi wabariki uamuzi huo na wengine waitaka Serikali iutazame upya.
Dar es Salaam. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepiga marufuku utaratibu wa wanafunzi wa awali hadi darasa la tano kukaa bwenini na kusitisha makambi ya elimu, jambo lililoibua mitazamo tofauti ya wadau huku baadhi wakisema litasaidia wazazi kuwa karibu na watoto wao.
Kamishna wa Elimu nchini Tanzania, Dk Lyabene Mtahabwa amepiga marufuku hiyo kupitia Waraka wa Elimu namba 2 wa mwaka 2023 unaohusu utoaji wa huduma ya kulaza wanafunzi katika mabweni kwa ngazi ya elimu ya awali na shule ya msingi.
Waraka huo umeeleza kuwa huduma za bweni kwa wanafunzi wenye umri mdogo huwanyima watoto fursa ya kushikamana na familia na jamii zao, kujenga maadili na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya familia na jamii zao.
Kitendo ambacho husababisha madhara ya muda mrefu na mfupi ikiwemo watoto kukosa upendo kwa wazazi wao na kusababisha kutokuwa sehemu ya familia ya jamii husika.
“Huduma za bweni zitolewe kuanzia darasa la tano na kuendelea, hairuhusiwi kutoa huduma ya bweni kwa wanafunzi wa elimu ya awali na darasa la kwanza hadi la nne isipokuwa kwa kibali maalumu kitakachotolewa na Kamishna wa Elimu baada ya kupokea maombi rasmi kutoka kwa mdau husika, “ inasomeka sehemu ya waraka huo.
Waraka huo ambao umeanza kutekelezwa Machi Mosi mwaka huu, unakuja wakati ambao kumekuwa na mijadala tofauti tofauti kuhusu ulazima wa wanafunzi wenye umri mdogo kukaa katika shule za bweni.
Zinazohusiana
-
Ni umri gani sahihi kumpeleka mtoto katika madarasa ya awali?
-
Watoto wadogo katikati ya kuisaka elimu madarasa ya awali Tanzania-2
Watanzania wanasemaje?
Baadhi ya Watanzania wameonyesha kufurahishwa na uamuzi huo huku wakishauri Serikali kuondoa kabisa utaratibu wa wanafunzi wa shule za msingi kukaa bwenini tofauti na sasa ambapo wanaoruhusiwa ni kuanzia darasa la tano.
Malisa Godlisten ambaye ni mtetezi wa haki za binadamu kupitia ukurasa wake wa Instagram amesema kuwaweka wanafunzi wa shule ya msingi bwenini ni kuwadhulumu haki yao ya malezi kwani wakati mwingine watoto hao hufanyiwa vitendo vya ukatili.
“Shule za bweni zibaki kwa sekondari tu, angalau wanaweza kujitambua, hata wakifanyiwa ukatili wanaweza kuripoti. Lakini shule za msingi Big NO (hapana). Ikiwezekana mwakani Serikali ifute bweni hata kwa hayo madarasa mawili yaliyobakia (la 6 na 7),” amesema Malisa.
Wakati wengi wakipongeza uamuzi huo baadhi yao wamesema jambo hilo litazamwe upya kwani shughuli za utafutaji ndiyo huwalazimisha wazazi kuwapeleka watoto bwenini wakiwa wadogo na si vinginevyo.
“Kuna mimi nipo mbali na nyumbani utafutaji wangu unafanya nimpeleke mtoto boarding(bwenini) hakuna anaependa mwanae akae shule ila ni mazingira yanafanya iwe ivo kwangu ili jambo liangaliwe upya, “ ameandika mmoja wa watumiaji wa mtandao wa Instagram Genesis Luicer
Kwa mujibu wa wanasaikolojia na wataalamu wa elimu na makuzi ya watoto, kumpeleka mtoto shule akiwa katika umri mdogo kunaweza kumsababishia akili yake kudumaa au kukataa kabisa kuendelea na shule siku za mbeleni.
“Akili ya mtoto inakuwa kwa hatua mbalimbali, kumuwahisha shule ni kama kuruka steji ya ukuaji wa mtoto, mwisho wa siku unakuta akili ya mtoto inadumaa au anachukia kabisa shule,” anasema Patrick Motto mwanasaikolojia kutoka Shirika la Brac Tanzania.
Mbali na kudumaa huko kwa akili, Motto anasema ikiwa mtoto atatumia muda mwingi shuleni na kukosa kabisa muda wa kucheza kutadumaza hata ukuaji wa mwili.
Naye Mwanasaikolojia Flolian Buhohela anasema mtoto aliye chini ya umri wa miaka mitatu anatakiwa kutumia muda mwingi akiwa na wazazi wake ili aweze kupata malezi, kujifunza maadili na tabia njema.
“Unapompeleka mtoto shule akiwa mdogo anaenda kujifunza tabia mpya ambazo hatuwezi kujihakikishia kwamba ni tabia njema au tabia mbaya ambazo pengine wazazi watashindwa kuzirekebisha hapo baadaye,” anasema Buhohela.
Mbali na kuzuia wanafunzi chini ya darasa la tano kukaa bwenini Serikali imepiga marufuku makambi ya taaluma ambayo yanatajwa kuhatarisha maadili pamoja na usalama wa afya za wanafunzi.
Hata hivyo njia hiyo ya makambi imewahi kuwa chanzo cha wanafunzi kufanya vizuri kitaaluma katika baadhi ya maeneo ikiwemo Mkoa wa Simiyu na Dodoma ambayo yalikuwa yakihamasishwa na aliyekuwa Mkuu wa Mikoa hiyo kwa nyakati tofauti Antony Mtaka.
Latest