Watoto wadogo katikati ya safari ya kuisaka elimu madarasa ya awali Tanzania
- Wazazi wawandikisha watoto chini ya miaka mitatu ili kusaka pesa.
- Walimu wasema wanapokea watoto hao kwa makubaliano na wazazi.
- Wadau wa elimu watofautiana kuhusu elimu hiyo.
Dar es Salaam. Hata uwe na usingizi wa aina gani kila ifikapo saa 12 asubuhi ni lazima ushtuke, si kwa kupenda ila ni kutokana na kilio cha mtoto anayelazimishwa kuamka kwa ajili ya kwenda shule.
Huwezi kumkaripia wala kumwambia apunguze kelele kwa sababu ni mtoto wa miaka miwili tu anayejaribu kuendana na mabadiliko ya maisha yake ya kuingia kwenye mfumo wa elimu.
Huyo ni Glory Baraka anayeishi na wazazi wake Kijitonyama jijini Dar es Salaam, walioamua kumuandikisha katika madarasa ya awali akiwa na miaka miwili tu ili wapate nafasi ya kuendelea na majukumu yao ya kutafuta pesa.
“Imenilazimu nimpeleke shule ili nikiwa naenda kwenye majukumu yangu asizurule ovyo mtaani au kunifuata kwenye kazi zangu,” anasema Irene Peter, mama mzazi wa Glory.
Mama huyo mwenye mtoto mmoja anayefanya biashara ya matunda na mafuta kati ya Mabibo na Makumbusho jijini hapa ni miongoni mwa wazazi wengi wanaowapeleka watoto shule wakiwa katika umri mdogo, jambo linaloibua maswali mengi kuhusu makuzi, ustawi na saikolojia ya watoto hao wanapokuwa wakubwa.
Kumekuwa na mjadala mpana kuhusu umri ambao mtoto anatakiwa aanze darasa la awali huku baadhi ya wazazi wakiwapeleka watoto wenye umri chini ya miaka mitatu na wengine wakipinga utaratibu huo.
Sera ya Elimu ya mwaka 2014 inashauri mtoto mwenye umri wa miaka mitano kujiunga na elimu ya awali kwa muda wa miaka miwili kabla ya kuanza elimu ya msingi.
Hata hivyo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi Elimu na Utamaduni (UNESCO) linalopendekeza mtoto kusoma darasa la awali kuanzia miaka mitatu mpaka miaka sita.
Kumekuwa na sababu mbalimbali za wazazi kuwapeleka watoto wao wadogo madarasa ya awali ikiwemo kubanwa na majukumu ya kiuchumi na hivyo kukosa muda wa kukaa na watoto wao.
Baadhi wanasema mtoto mdogo akikaa nyumbani kwa muda mrefu anakosa fursa ya kukutana na kucheza na wenzake.
Hamadi Kilango ni mzazi wa Ivan Kilango (3) aliyelazimika kumpeleka mtoto wake shule akiwa na miaka 2 na nusu ili acheze na wenzake.
Soma zaidi:Watoto wadogo katikati ya kuisaka elimu madarasa ya awali Tanzania-2
“Niliona watoto wenzie wote hapa mtaani wameenda shule na mwanangu anakosa wa kucheza naye hivyo nikaona tumpeleke tu na yeye,” anasema Kilango mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam.
Ivan hutumia saa moja kufika shuleni ambapo huchukuliwa nyumbani na gari la shule saa 12:30 asubuhi na kuanza masomo saa 08:00 asubuhi mpaka saa nane mchana.
Akiwa shuleni, Ivan pamoja na watoto wengine wenye umri sawa na wake hufundishwa kuhesabu, kuchora, na michezo mbalimbali.
Kwa utaratibu wa shule yake, ikifika saa 4 asubuhi hupewa uji na kutakiwa kulala kwa saa mbili mpaka saa 7 mchana wanapotakiwa kuamka na kucheza mpaka watakapokuja kuchukuliwa na usafiri wa kuwarudisha makwao.
Hali ikoje Tanzania
Ripoti ya Takwimu Muhimu za Elimu kwa mwaka 2022 (BEST 2022), zinazotolewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), inaeleza kuwa kuna wanafunzi milioni 1.5 waliandikishwa katika madarasa ya awali 19,284 mwaka jana.
Idadi hiyo ya wanafunzi wa madarasa ya awali kwa mwaka 2022 imeongezeka kwa asilimia 11 kutoka idadi ya wanafunzi milioni 1.39 waliandikishwa mwaka 2021.
Kati ya wanafunzi hao asilimia 50.8 ni wasichana wenye umri kati ya miaka mitatu hadi miaka sita.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa Mkoa wa Mwanza unaongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi wa madarasa ya awali Tanzania. Mkoa huo uliandikisha wanafunzi 113,430 mwaka jana.
Wanafunzi hao waliopo mkoani Mwanza ni sawa na asilimia 7 tu ya wanafunzi wa awali waliopo nchini, huku asilimia 51 ya wanafunzi hao wakiwa ni wasichana.
Mikoa mingine iliyoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wa shule za awali ni pamoja na Kagera yenye wanafunzi 104,816, ikifuatiwa na mkoa wa Mara wenye wanafunzi 94,989.
Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2021 kinachotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kuongezeka kwa idadi hiyo ya wanafunzi waaliandikishwa elimu ya awali kunatokana na jitihada za Serikali za kuboresha elimu ya msingi.
“Ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi katika elimu ya awali lilitokana na jitihada za Serikali za kuendelea kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ikiwemo ugharamiaji wa elimumsingi bila ada pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu,” inaeleza sehemu ya kitabu hicho.
Wakati uandikishaji katika madarasa ya awali ukishuka, bado Serikali na wadau wa elimu watakuwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha kunakuwa na uwiano mzuri wa mwalimu na wanafunzi katika madarasa hayo. Picha|Mtandao.
Watoto wa umri gani wanaoandikishwa zaidi?
Uchunguzi mdogo uliofanywa na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) katika shule tano za madarasa ya awali jijini Dar es Salaam umegundua kuwa kati ya watoto 10 wanaondikishwa shule za awali (Nursery school), watatu wanakuwa chini ya umri wa miaka mitatu ambao hashauriwi na sera ya elimu.
Baadhi ya walimu wanaofundisha shule hizo ambao hawakupenda majina yao kutajwa wamekiri kupokea watoto wenye umri chini ya miaka mitatu kwa makubaliano na wazazi wao.
“Kwa kawaida hatupokei watoto chini ya umri wa miaka mitatu ila kwa makubaliano maalum na mzazi au tukiona mtoto ana uwezo wa kuongea na kujifunza,” anasema mwalimu huyo wa shule ya awali.
Mwalimu huyo anaeleza kuwa mbali na kujifunza kwa kuimba na kuchora, wanafunzi wa shule ya awali kwenye darasa lake hukaa shulei kwa saa 8 mpaka 10.
Soma zaidi:Vyakula vinavyoimarisha kumbukumbu, uelewa wa kimasomo kwa watoto
Kati ya saa hizo, watoto hupata muda wa kujifunza, kucheza na kupumzika kwa saa 2 kabla ya kurudishwa makwao na usafiri wa unaotolewa na shule au wazazi kuja kuwachukua watoto.
Ili kuhakikisha ubora wa taaluma wanayotoa kwa watoto hao, mwalimu huyo huwapatia kazi za nyumbani ambazo wanatakiwa kuzifanya na kuja nazo siku inayofuata.
“Tunawapa homework (kazi za nyumbani) lakini pia wakiwa shuleni wanasoma masomo mbalimbali kama kuchora, kuandika na kuhesabu,” anasema mwalimu huyo.
Wakati hayo yakiendelea katika baadhi ya shule za binafsi za awali, shule za Serikali hutumia saa 4 mpaka 6 kwa wanafunzi wake kukaa darasani ambapo hujifunza, kupata kifungua kinywa (uji au chai) na kuwaruhusu warudi nyumbani.
“Masomo ambayo tunawafundisha ni kuwasiliana, kuhusiana, afya na michezo ila hatuwapi homework (kazi za nyumbani) wakimaliza warudi nyumbani kwao,” anasema mwalimu mmoja wa darasa la awali lilipo katika moja ya shule zilizopo jijini hapa.
Nini kinatokea endapo mtoto atapelekwa mapema shuleni? Fuatilia (hapa)sehemu ya pili ya makala haya ambayo inaeleza kwa undani kuhusu suala hilo
Nyongeza na Daniel Samson
Tangazo