Vipaumbele 5 Wizara ya Elimu mwaka 2023 – 24
- Zaidi ya nusu ya fedha za bajeti kutumika kwa shughuli za maendeleo
- Yabaanisha vipaumbele vitano ikiwemo kupitia Sera ya Elimu, Sheria ya Elimu na kuanza utekelezaji wa mitaala kwa ngazi zote.
- Uhaba wa walimu na muingiliano wa majukumu vyatajwa kama changamoto za uendeshaji sekta ya elimu
Dar es Salaam, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeomba jumla ya Sh1.6 trilioni kwa ajili ya kutimiza majukumu yake kwa mwaka 2023/24 ambapo zaidi ya nusu ya bajeti hiyo ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vyuo vya ufundi stadi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda aliyekuwa akisoma hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/24, amewaambia Wabunge kuwa kati ya fedha hizo Sh1.3 trilioni zitatumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Bajeti hiyo imeongezeka kwa asilimia 5 ikilinganishwa na bajeti ya Sh1.4 trilioni ya mwaka 2023/24.Prof Mkenda aliyekuwa akiwasilisha bajeti hiyo amesema, mwaka ujao wizara yake itajikita kutekeleza vipaumbele vitano muhimu.
Kukamilisha mapitio ya Sera ya Elimu na ya Sheria ya Elimu
Mkenda amebainisha kuwa kipaumbele cha kwanza cha wizara ni kukamilisha mapitio ya Sera ya Elimu ya Mafunzo ya mwaka 2014 na mitaala ya elimu na kuanza utekelezaji wake.
“Serikali itakamilisha mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 na mitaala ya elimu pamoja na kuanza utekelezaji wake ili kuimarisha maarifa na ujuzi kwa wahitimu wa ngazi zote za elimu,” amesema Mkenda.
Itakumbukwa kuwa tayari wizara hiyo imeshatoa rasimu ya mitaala ya elimu ambayo inapaswa kuanza kutumika ambapo Watanzania na wadau wa elimu walipata nafasi ya kutoa maoni juu ya wapi pa kuboresha.
Zinazohusiana
-
Uhaba wa walimu bado wazitesa shule za msingi, sekondari Tanzania
-
Kulikoni walimu kupungua shule za msingi za Serikali Tanzania?
Vipaumbele vingine ni pamoja na kuongeza fursa na ubora kwa mafunzo ya amali (ufundi na ufundi stadi) katika elimu ya sekondari na vyuo vya amali, kuongeza fursa na ubora wa elimu ya msingi na sekondari pamoja na kuongeza fursa na ubora wa elimu ya juu na kuimarisha uwezo wa nchi katika utafiti.
Ili kuongeza fursa na ubora kwa mafunzo ya amali kwa shule za sekondari na vyuo vya ufundi, Mkenda amewaambia wabunge kuwa Serikali itafanya ukarabati wa majengo pamoja na kuziwezesha vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Serikali itaboresha vyuo vya ualimu 10 kwa kuweka karakana na vifaa katika vyuo hivyo ambavyo ni Kitangali, Ndala, Nachingwea, Kleruu, Mtwara Ufundi, Mpwapwa, Korogwe, Nakawa, Bunda na Kabanga.
Mapungufu uendeshaji sekta ya elimu
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Profesa Kitila Mkumbo amebainisha kuwa uchambuzi uliofanywa na kamati hiyo umebaini kuna mapungufu katika uendeshaji wa sekta ya elimu ambapo hakujawekwa mkakati wa kuyatatua ikiwemo muingiliano wa majukumu.
Mkumbo amebainisha kuwa kuna mgongano na muingiliano wa usimamizi wa elimu katika ngazi ya awali, shule ya msingi na sekondari kati ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
“Mgongano na muingiliano huu unajidhihirisha zaidi katika maeneo ya utawala wa elimu, ujenzi wa miundombinu na utoaji wa miongozo mbalimbali ya uendeshaji wa elimu nchini,” amesema Profesa Mkumbo.
Uhaba wa walimu watajwa
Mkumbo amebainisha kuwa Sekta ya elimu inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu kuanzia ngazi ya awali, msingi na sekondari pamoja na wakufunzi na wahadhiri katika ngazi ya vyuo vya amali na elimu ya juu
Aprili 12, 2023 Waziri wa Tamisemi Angellah Kairuki aliwaambia wabunge kuwa Serikali imetangaza nafasi 21,200 kwa kada ya walimu na afya ambapo licha ya wabunge kupongeza waliitaka Serikali kufanya jitihada za kuajiri walimu wengi zaidi.
Changamoto nyingine zilizobainika katika sekta hiyo muhimu ni uwepo wa udhaifu katika uthibiti ubora wa shule na kusababisha shule nyingi kutokakuguliwa ambapo kwa mwaka 2022/23 ni asilimia 26.4 pekee ya shule za msingi zilikaguliwa.
Latest
