Maoni mchanganyiko Serikali ikipendekeza kufuta ada kidato cha tano, sita
- Inakusudia kuanza utaratibu huo mwaka wa fedha wa 2022/23.
- Wazazi wasema itawapunguzia mzigo wa kusomesha.
- Wadau wa elimu washauri Serikali kuongeza ruzuku ya shule na kuvikumbuka vyuo vya kati.
Dar es Salaam. Huenda taswira ya elimu ya sekondari nchini Tanzania ikachukua muonekano mpya, baada ya Serikali kupendekeza kufuta ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita kwa shule za Serikali katika mwaka wa fedha 2022/23 huku wadau wa elimu wakisema hatua hiyo itapunguzia wazazi mzigo wa kusomesha.
Huo ni muendelezo wa Serikali kuboresha elimu baada ya kuanza kutoa elimu bila malipo kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari (kidato cha I Hadi IV).
Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba aliyekuwa akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/23 alisema wanafunzi wa kidato cha V na VI wapo 147,705 watahitaji Sh10.3 bilioni hivyo Serikali katika kuwapunguzia gharama inakusudia kufuta ada kwa wanafunzi hao.
“Napendekeza kufuta ada kwa wanafunzi wa kidato cha V na VI. Kwa hatua hiyo, elimu bila ada ni kuanzia shule za msingi mpaka kidato cha sita,” alisema Dk Nchemba Juni 14 mwaka huu bungeni jijini Dodoma.
Pendekezo hilo limepokelewa kwa hisia tofauti na wazazi, walimu na wadau wa elimu nchini huku wengi wakisisitiza kuwa ni hatua muhimu katika maendeleo ya elimu nchini.
Wazazi ambao wana watoto wanaosoma au wanaotarajia kuwapeleka watoto wao kidato cha tano wamesema itawapunguzia mzigo hasa katika kipindi hiki ambacho gharama za maisha zipo juu.
“Hili lilikuwa changamoto hasa kwa wakati huu ambapo gharama za maisha zipo juu, wazazi na walezi wengi wasingemudu kuwapeleka watoto wao shule lakini hili litasaidia ambapo mzazi atalazimika kununua sare pekee za shule na mahitaji mengine,” amesema Petro Pendo, mkazi wa Buhongwa, jijini Mwanza.
Awali mzazi alikuwa nabeba gharama zote za ada na mahitaji ya mtoto wake anapokuwa shuleni, jambo ambalo baadhi ya wazazi wanaosomesha watoto katika shule za Serikali wanaona ni mzigo.
Hellen Mtereko, Mkazi wa Mwanza amesema kufutwa kwa ada kutasaidia wanafunzi kusoma kwa bidii na wazazi watakuwa hawana sababu za kutowapeleka watoto wao shule kutokana na kupunguziwa sehemu ya gharama.
“Sasa hakutakuwa na visingizio tena vya mzazi kushindwa kumpeleka mtoto wake shule,” amesema Mtereko.
Uboreshaji wa miundombinu katika shule ya sekondari Kisimiri wachangia kuongezeka kwa ufaulu.Picha| Valentine Tarimo.
“Na vifaa shule watusaidie”
Baadhi ya wazazi wameiomba Serikali isiishie kwenye ada bali ibebe na jukumu la kugharamia vifaa vya shule kwa wanafunzi kwa sababu bei zake ziko juu.
“Utakuta ada ya shule iko chini lakini mahitaji yanayohitajika mtoto kwenda nayo yako juu hivyo niombe hili waliangalie kwa jicho la tatu,” amesema Petro Pendo, mkazi wa jijini Mwanza.
Walimu watia neno
Kwa mujibu wa Rashid Gewe, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwanza, unafuu huo utakaotolewa na Serikali iwe chachu ya wazazi kufuatilia kwa karibu maendeleo ya masomo ya watoto wao ili waweze kutimiza ndoto zao.
Amesema baadhi ya wanafunzi huacha shule kwa sababu ya utoro, kujiingiza katika kazi ngumu na kupata mimba kwa sababu wazazi wao hawajaweka umakini kuwafuatilia.
Mwalimu Aldo Mhoka kutoka mkoani Iringa amesema kufutwa kwa ada ni fursa kwa Watanzania walio wengi kupata elimu na kufikia ndoto zao.
Hata hivyo, ameishauri Serikali kuweka mazingira rafiki katika vyuo vikuu na vya kati kwani hatua hiyo itaongeza wahitimu kujiunga katika ngazi hiyo ya elimu.
“Tuliona matunda kipindi wameweka elimu bure kuanzia shule ya msingi mpaka kidato cha nne, wanafunzi waliongezeka sana…nitoe maoni yangu kwa Serikali kujiandaa kwa elimu ya juu.
“…sasa wanakwenda kumaliza wengi zaidi, watahitaji kwenda chuo kikuu, hivyo Shirikisho la Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu (HESLB) wajiandae kuwapokea wanafunzi hawa na kuwapa mkopo ili watimize ndoto zao,” amesema Mhoka.
Zinazohusiana:
- HESLB kuboresha mfumo wa utoaji, urejeshaji mikopo elimu ya juu.
- Wanafunzi 25,532 wapata mikopo awamu ya kwanza
- Heslb yaanika kozi zitakazopewa kipaumbele utoaji mikopo elimu ya juu 2019-2020
Wadau wa elimu
Afisa Elimu mstaafu wa Mkoa wa Iringa, Mhandisi Joyce Baravuga amesema hatua hiyo itatoa unafuu huku akiwataka wazazi kuwahimiza watoto wao kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
“Nimefurahia sana kuondolewa kwa hiyo ada na naipongeza Serikali…kwa kweli italeta unafuu kwa watoto kuwa huru kusoma na wazazi kupata unafuu kwa sababu wengi walikuwa wanapata shida ya ada hivyo natoa wito kwa wazazi wakawahimize watoto waweze kusoma ili malengo yafikiwe,” amesema Baravuga.
Mchambuzi wa masuala ya elimu na mwandishi wa vitabu, Richard Mabala amesema baada ya hatua hiyo, Serikali iongeze ruzuku kwenye shule ili zijiendeshe kwa ufanisi.
“Ni mategemeo yangu kwamba ruzuku kwa shule itaongezeka ili kuhakikisha kwamba shule zinakuwa na pesa za kutosha kujiendesha vizuri ili kufidia pesa ambazo zingeingia kupitia ada,” amesema Mabala ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya shirika la HakiElimu.
Amewashauri wanafunzi kutumia fursa hiyo vizuri kusoma vitu wanavyopenda kwani wana nafasi ya kufaulu zaidi kuliko kusoma kwa kufuata mkumbo.
Tangazo

Hata hivyo, Mabala ameishauri Serikali kutoa mikopo hata kwa vyuo vya ufundi nchini ili kuwawezesha kudhi mahitaji wanapokuwa vyuoni kwa sababu vinapokea wahitimu wa vitado vya IV na VI.
“Sioni kwa nini mikopo hutolewa kwa ajili ya vyuo vikuu tu, mtu akimaliza elimu yake ya sekondari kwa nini asipewe mkopo kwenda Veta?, tunapoteza makundi mengi kwani njia pekee watu wanapata pesa ni chuo kikuu na siyo kila mtu anataka kwenda chuo kikuu,” amesema Mabala.
Waziri Nchemba alipokuwa akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali alisema inaangalia uwezekano wa kutoa fedha kwa vyuo vya kati ili wanafunzi wake wasome ili wanafunzi wasome katika mazingira mazuri.
“Serikali itajipanga kuangalia namna ya kusaidia vyuo vya kati kadiri hali ya uchumi itakavyotengemaa,” alisema Dk Nchemba.
Latest