Ufahamu ugonjwa wa nimonia, dalili, matibabu na jinsi ya kujikinga
- Mwaka 2019, ugonjwa huu ulisababisha vifo vya watoto 740,180 walio chini ya umri wa miaka mitano.
- Ugonjwa huu unaweza kuathiri pafu moja au yote mawili.
Dar es Salaam. Nimonia ni miongoni mwa magonjwa hatari ya mfumo wa upumuaji yanayoathiri mamilioni ya watu duniani, hususan watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Shirika la Afya Duniani (WHO), linabanisha kuwa mamilioni ya watoto hupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo kila mwaka.
Mathalani mwaka 2019, ugonjwa huu ulisababisha vifo vya watoto 740,180 walio chini ya umri wa miaka mitano, sawa na asilimia 14 ya vifo vyote katika kundi hilo la umri.
Nchini Tanzania, takwimu za Wizara ya Afya za mwaka 2024 zinaonesha kuwa visa 245,490 vya ugonjwa huo viliripotiwa kwa watoto walio chini ya miaka mitano.
Nimonia ni ugonjwa gani?
Kwa mujibu wa WHO, nimonia ama Pneumonia ni aina ya maambukizi ya ghafla katika mfumo wa upumuaji yanayoathiri mapafu, hususan kwenye vifuko vidogo vya hewa vinavyojulikana kama alveoli.
Katika hali ya kawaida, vifuko hivyo hujazwa na hewa wakati mtu anapovuta pumzi na kusaidia kuingiza oksijeni kwenye damu.
Hata hivyo, mtu anapopata nimonia, vifuko hivyo vinaweza kujaa maji maji au usaha kutokana na maambukizi, hali inayopunguza uwezo wa mapafu kufanya kazi ipasavyo.
Matokeo yake ni mgonjwa kupata shida ya kupumua, kukohoa na wakati mwingine kushindwa kupata oksijeni ya kutosha mwilini.
Ugonjwa huu unaweza kuathiri pafu moja au yote mawili na kumpata mtu wa umri wowote, ingawa watoto wadogo, wazee na watu wenye kinga dhaifu wako katika hatari kubwa zaidi ya kupata madhara makubwa.

Visababishi vya ugonjwa wa nimonia
Daktari Rashidi Issa kutoka Zanzibar anaeleza kuwa nimonia inaweza kusababishwa na aina mbalimbali za bakteria, virusi na fangasi.
Anasema miongoni mwa bakteria wakuu wanaosababisha ugonjwa huo ni ‘Streptococcus pneumoniae’ na ‘Haemophilus influenzae’ aina b (Hib).
WHO inavitaja visababishi vingine vya ugonjwa hu kuwa virusi (vimelea) vya ‘Respiratory Syncytial Virus (RSV)’ pia ni miongoni mwa visababishi vya nimonia ambavyo huwaathiri zaidi watoto wadogo.
Mbali na bakteria na virusi, nimonia inaweza pia kusababishwa na fangasi aina ya ‘Pneumocystis jirovecii’. Fangasi hao huathiri zaidi watoto wachanga wenye maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na wanahusishwa na takribani robo ya vifo vya nimonia miongoni mwa watoto wachanga wenye maambukizi hayo.
Kwa upande mwingine, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC) kinabainisha kuwa watu wenye magonjwa sugu wako katika hatari kubwa zaidi ya kupata nimonia. Magonjwa hayo ni pamoja na magonjwa sugu ya moyo, ini na mapafu, pamoja na kisukari.
Dalili za nimonia zinazopaswa kupewa tahadhari
Dk Issa anasema dalili za nimonia zinaweza kuanza taratibu au kujitokeza ghafla, kutegemea aina ya maambukizi na hali ya afya ya mgonjwa.
Baadhi ya dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kikohozi kikavu, kupumua kwa shida, homa na joto la mwili kupanda.
Katika hatua za awali, mgonjwa anaweza kupata dalili zisizo kali, lakini kadri hali inavyoendelea, matatizo ya kupumua yanaweza kuongezeka.
Vile vile, uchovu mkubwa na mwili kukosa nguvu, kutokwa na jasho jingi, kukosa hamu ya kula, wakati mwingine kuchanganyikiwa, hasa kwa wazee.
Kwa watoto, Dk Issa anasema, dalili zinaweza kujumuisha sehemu ya chini ya kifua kuvutika na kuingia ndani wakati wa kuvuta pumzi, pamoja na kusikika kwa mlio wa filimbi wakati wa kupumua, hasa wakati wa kuvuta hewa ndani, kushindwa kunyonya au kula vizuri, kupumua kwa haraka, kuwa mlegevu kuliko kawaida.
Je, nimonia inaambukiza?
Nimonia yenyewe si lazima iwe ugonjwa unaoambukizwa moja kwa moja kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Hata hivyo, baadhi ya vimelea vinavyosababisha ugonjwa huo vinaweza kuenea kupitia hewa au matone ya majimaji yanayotoka wakati mtu anapokohoa au kupiga chafya.
Mtu anapokutana na vimelea hivyo anaweza kupata maambukizi ya mfumo wa upumuaji, ambayo kwa baadhi ya mazingira yanaweza kuendelea na kusababisha nimonia ingawa matibabu hutegemea chanzo cha maambukizi na ukubwa wa ugonjwa.
“Mara nyingi magonjwa ya mfumo wa hewa huwa yanaambukiza, na njia mojawapo ya maambukizi ni kupitia hewa. Hata hivyo, nimonia haiwekwi moja kwa moja katika kundi la magonjwa yanayoambukiza kupitia hewa…
…Ni mara chache sana wahudumu wanaowahudumia wagonjwa wa nimonia hupata ugonjwa huo, kwa sababu nao hukutana na visababishi vinavyoweza kumfanya mgonjwa kupata nimonia,” anaeleza Dk Issa.
Jinsi ya kujikinga
Ili kuzuia ugonjwa huu WHO inapendekeza watoto kupatiwa chanjo dhidi ya magonjwa kama Hib, pneumococcus, surua na kifaduro, lishe bora na unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya kwanza ya maisha husaidia kuimarisha kinga ya mwili na kupunguza hatari ya kupata ugonjwa huo.
Hatua nyingine ni kupunguza uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba kwa kutumia nishati safi, kuzingatia usafi, hasa katika makazi yenye msongamano wa watu.