Yafahamu matunda yanayoweza kutibu na kukupa kinga ya maradhi
- Ni pamoja na komamanga na parachichi
- Wataalamu wa afya wanasema yana uwezo wa kutoa tiba na kinga dhidi ya maradhi.
- Washauri kupata vipimo kabla ya kuanza kutumia matunda.
Dar es Salaam. Maradhi ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, na bila shaka umewahi kuumwa ama kuona watu wengine wakipitia changamoto mbalimbali za kiafya zitokanazo na sababu tofauti.
Mara nyingi tufikwapo na maradhi, hospitali huwa kimbilio la kwanza kwa ajili ya kupata msaada wa matibabu kulingana na tatizo husika, lakini uwataalamu wa afya wanabainisha kuwa, pamoja na ufanisi wa dawa za viwandani baadhi huacha athari hasi katika mwili.
Usilolifahamu ni kuwa baadhi ya matunda yanaweza kukupa manufaa makubwa kiafya ikiwemo tiba bora pamoja na kinga ya magonjwa mbalimbali, jambo litakalo kukupunguzia gharama na muda mwingi unaotumia kujiuguza au kuuguza.
Kwa mujibu wa Shule ya udaktari ya Chuo Kikuu cha Havard (Havard University Medical School) kilichopo nchini Marekani, aina zote za matunda zina virutubisho vinavyoweza kutoa kinga dhidi ya magonjwa.
“Ingawa matunda yote huwa na virutubishi vingi vya kinga ya magonjwa, matunda mengine yamepewa kipaumbele zaidi katika ulimwengu wa lishe kutokana na kuwa na faida nyingi,” kimesema chuo hicho.
Najua unazifahamu faida za kiafya za kula matunda lakini katika makala hiii utafahamu zaidi aina ya matunda yanayoweza kutumika na jinsi yanavyotumika kutibu magojwa mbalimbali.
Komamanga
Shule ya udaktari ya Chuo Kikuu cha Harvard kinasema komamanga lina uwezo wa kusaidia kudhibiti shinikizo la damu(blood pressure), lehemu (cholesterol) na kiwango cha sukari mwilini.Hii ni kutokana na uwepo wa vitamini C,K, potasiamu, nyuzi nyuzi, na kemikali zenye nguvu zinazopatikana katika mbegu za tunda hilo.
Ili kupata faida hizo za kiafya tovuti ya healthfy inashauri matumizi yasiyozidi kikombe kimoja cha sharubati (juisi) ya tunda hilo kwa siku, kabla, baada au wakati wa mlo
Zinazohusiana
Matunda yenye asili ya uchachu (citrus)
Daktari Kelvin Loti kutoka hospitali ya Kibamba anasema Matunda yenye asili ya uchachu kama machungwa, limao na zabibu yana wingi wa vitamini, nyuzu nyuzi, potasiam na kalsiam ambayo inauwezo mkubwa wa kupambana aina mbalimbali za magonjwa ikiwemo magonjwa ya moyo na wingi wa sukari mwilini.
Tovuti ya Healthifyme inasema ulaji uliopitiliza wa iana hii ya matunda inaweza kuleta athari kwenye mwili wa binadamu ikiwemo kuongezeka kwa asidi mwilini, mapigo ya moyo kuongezeka na maumivu ya tumbo.
“Kwa hiyo kwa siku usidishe matunda mawili au matatu…juisi usitumie zaidi ya milimita 240 (sawa na kikombe kimoja na nusu),”imesema tovuti hiyo.
Matunda yenye asili ya maji
Mtaalamu huyo wa afya anaeleza kuwa matunda yenye asili ya maji maji kama tikitimaji, tango na machungwa husaidia kupunguza maumivu ya kichwa, kutoa nafuu kwa magonjwa ya njia ya mkojo UTI na figo.
“Matunda haya huwa na vitamin C kwa wingi kwa hiyo kama kuna bakteria kwenye njia mkojo au kwenye figo huwa wanakufa au wanatolewa kwa njia ya mkojo,”amesema
Licha ya utamu wa matunda uliopo kwenye matunda haya daktari Kelvin amesema si vyema kutumia matunda matunda zaidi ya matano kwa siku.
“Na hayo matunda matano usile kwa wakati mmoja, unaweza kula asubuhi, lingine ukala mchana na jioni,” ameongeza daktari huyo.

Mbali na kutibu magonjwa matunda yenye asili ya uchachu kutibu magonjwa yanasaidia sana kuboresha ngozi na kuifanya iwe na muonekano mzuri.Picha|Healthifyme.
Parachichi
Licha ya tunda hili kupendwa na watu wengi Daktari anasema lina uwezo mkubwa wa kutoa kinga na tiba ya baadhi ya magonjwa ikiwemo presha na magonjwa ya moyo.
“Parachichi lina mmea asilia iitwayo ‘sitosterol’ unaosaidia kupunguza hatari ya ugonjwa moyo,”imesema tovuti ya afya ya Medical News Today.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na tovuti hiyo parachichi linaweza kutibu presha ya kupanda na kushuka kutokana na wingi wa virutubisho vilivyopo katika tunda hilo, unachotakiwa kufanya ni kulitumia kila siku kama sehemu ya mlo wako.
Daktari atoa angalizo
Daktari Kelvin anatahadharisha si vema kutumia matunda haya kama tiba bila kupima na kufuata ushauri wa daktari.
Anashauri ni vyema mgonjwa kujua hali yake ya kiafya athari za ugonjwa husika katika mwili wake kabla ya kuanza kutumia matunda kama tiba.
“Hii ni tiba kamili ila kama umeshapatwa na ugonjwa matunda hayawezi kukusaidia kwa kiwango kikubwa…hata kutibu kwake siyo kwa haraka,” ameongeza Kelvin.
Mtaalamu huyo wa afya amesisitiza kuwa kutembelea kituo cha afya kabla ya kuanza utaratibu wa kutumia matunda unamsaidia mgonjwa kujua hatua ya ugonjwa ulio nao na kupata uangalizi na ushauri zaidi wa kitabibu.