TCU yafungua dirisha udahili vyuo vikuu 2026/27, yaonya matapeli
- Dirisha hilo la awamu ya kwanza litadumu kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia Julai 10 hadi Agosti 10, 2026.
Dar es Salaam. Vijana wenye mpango wa kujiunga na elimu ya juu nchini watakuwa na mwezi mmoja wa kupambania ndoto zao baada ya tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kufungua dirisha la maombi ya udahili kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Dirisha hilo la awamu ya kwanza linalotarajiwa kuanza Julai 10 hadi Agosti 10, 2026 ambapo watu wote wanaotaka kujiendeleza kielimu watatakiwa kuwasilisha maombi ya udahili kwenye vyuo wanavyovipenda.
Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, aliyekuwa akizungumza na wanahabari, amesema dirisha hilo linawahusu waombaji wenye sifa za kujiunga kupitia makundi matatu wakiwemo waliomaliza kidato cha sita.
Sehemu kubwa ya kundi hili ni lile ambalo lilipata matokeo wiki hii ambao kwa mujibu wa Baraza la Mitihani (Necta) ufaulu wao kwa mwaka 2026 uliongezeka hadi kufikia asilimia 99.94.
“Kundi la pili ni wenye sifa stahiki za Stashahada kwa maana ya diploma au sifa nyingine linganifu, na kundi la tatu ni wenye sifa stahiki za cheti cha awali kinachotolewa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania,” amesema Prof Kihampa.
Mambo ya kuzingatia kabla ya kuomba
Kabla ya kuwasilisha maombi, TCU imewataka waombaji kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo kusoma kitabu cha mwongozo wa udahili ili kujiridhisha kuwa wanakidhi vigezo vya programu wanazokusudia kuomba kabla ya kuwasilisha maombi yao.
Aidha, mwombaji anatakiwa kutuma maombi moja kwa moja katika vyuo vikuu anavyohitaji kupitia mifumo ya kielektroniki ya kila chuo kulingana na taratibu zilizowekwa na taasisi husika.
Kabla ya kufanya hivyo mwombaji anashahuriwa kuhakikisha ametembelea tovuti za vyuo hivyo ili kupata taarifa za kina kuhusu programu za masomo, masharti ya udahili na utaratibu wa kutuma maombi kabla ya kufanya uchaguzi wa masomo.
Kwa waombaji wenye uraia wa Tanzania walio na vyeti kutoka nje wanatakiwa kupata ithibati ya ulinganifu wa vyeti hivyo kutoka TCU kabla ya kuomba udahili.
Aidha, vyeti vya elimu ya sekondari vinapaswa kuthibitishwa na Necta pamoja na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).
Epuka madalali
Ilikuepuka udanganyifu na kutapeliwa TCU imewataadharisha waombaji kujiepusha na watu wanaojitambulisha kama mawakala au washauri wanaoweza kusaidia kupata nafasi za udahili.