TCU yaongeza muda wa udahili kwa shahada ya kwanza 2025/2026
- Ni kuanzia Oktoba 6 na kufungwa Oktoba 10, 2025.
- Tume yasisitiza waombaji wote ambao hawakuweza kudahiliwa au waliokosa nafasi katika awamu zilizopita kutumia vyema nafasi hii kwani hakutakuwa na nafasi nyingine baada ya dirisha kufungwa.
Dar es salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza kuongeza muda wa udahili kwa ngazi ya Shahada ya Kwanza katika programu ambazo bado zina nafasi kwa mwaka wa masomo 2025/2026.
Hatua hiyo inalenga kutoa fursa kwa waombaji ambao hawakufanikiwa kupata nafasi katika awamu zilizopita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, tume imeongeza muda wa udahili kuanzia Oktoba 6 mpaka10, 2025 kufuatia maombi yaliyotolewa na Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (TAHLISO) pamoja na vyuo vikuu, ambapo imeeleza kuwa awamu hii ya tatu itakuwa ndio awamu ya mwisho ya udahili.
“Waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja na wale ambao hawakuweza kuthibitisha udahili katika awamu ya kwanza wanapaswa kuthibitisha udahili wao kuanzia tarehe 06 hadi 19 Oktoba, 2025 kwa kutumia namba maalum ya siri waliyopelekewa kupitia simu au barua pepe zao,” imeeleza taarifa hiyo.
Tume inasisitiza waombaji wote ambao hawakuweza kudahiliwa au waliokosa nafasi katika awamu zilizopita kutumia vyema nafasi hii kwa kuwa hakutakuwa na nafasi nyingine baada ya dirisha kufungwa Oktoba 10, 2025.
“Tume inawashauri waombaji watumie fursa hii vizuri kwa kutuma maombi yao ya udahili kwenye vyuo wanavyovipenda.
Aidha, Vyuo vya Elimu ya Juu nchini vinaelekezwa kuendelea kutangaza programu ambazo bado zina nafasi,” imesistiza taarifa ya Profesa Kihampa.
Kwa mujibu wa TCU, udahili katika awamu ya kwanza na ya pili umekamilika, na majina ya waliochaguliwa katika awamu ya pili yatatangazwa na vyuo husika kuanzia Oktoba 6, 2025 huku vyuo vikitarajiwa kutangaza majina ya waliodahiliwa katika awamu ya tatu ifikapo Oktoba 20, 2025.
Latest



