Juu zaidi: BoT yapandisha riba ya benki kuu hadi 6.25%
- Kiwango kipya kilichopangwa na Kamati ya Sera ya Fedha ya BoT ni cha juu tangu mfumo mpya wa kudhibiti mfumuko wa bei uanze kutumika zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Dar es Salaam. Kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) kimepanda hadi asilimia 6.25 katika robo ya tatu ya mwaka 2026, ikiwa ni kiwango cha juu kuwahi kurekodiwa tangu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ianze kutumia mfumo huo mpya katika kudhibiti mfumuko wa bei na kukuza uchumi nchini.
Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya BoT leo Julai 3, 2026 imepandisha kiwango cha riba hiyo kuu kwa kuongeza asilimia 0.50 kutoka asilimia 5.75 iliyotumika kwa robo nne tangu Julai mwaka 2025. Kiwango cha juu zaidi cha CBR kabla ya hiki kipya kitakachotumika kuanzia Julai hadi September 2026, ni asilimia 6% kilichotumika kati ya Aprili 2024 hadi Juni 2025.
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amewaeleza wanahabari na mabosi wa taasisi za kifedha jijini Dar es Salaam kuwa hatua hiyo imefikiwa ili kudhibiti mfumuko wa bei unaochochewa na gharama kubwa za nishati, mbolea, na usafirishaji katika soko la kimataifa, zilizosababishwa na vita inayoendelea Mashariki ya Kati.
CBR ni riba ambayo hutumika na BoT kufanya biashara kati yake na benki za biashara au baina ya taasisi hizo za kifedha nchini.
“MPC ina imani kuwa marekebisho hayo ya CBR yanatosha kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya kiwango kinacholengwa cha asilimia 3 hadi asilimia 5, huku yakichochea ukuaji wa uchumi,” amesema Tutuba.
Kamati hiyo anayoiongoza, amesema inatarajia kuwa mfumuko wa bei wa chakula utakuwa katika kiwango cha wastani kutokana na usambazaji wa chakula wa kutosha kutokana na mavuno mazuri ya msimu wa 2025/26.
Mfumuko wa bei bado chini
Mfumuko wa bei umeendelea kuwa chini licha ya kuongezeka kwa bei ya nishati na gharama za uchukuzi kutoka na vita inayoendelea baina ya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Kwa zaidi ya miaka miwili sasa, mfumuko wa bei nchini umebaki ndani ya wigo wa kiwango cha kati ya asilimia 3 na asilimia 5 kama ilivyotarajiwa na Serikali.
Tutuba amesema athari za viwango vya kubadilishia fedha kwa mfumuko wa bei zinatarajiwa kuwa ndogo kutokana na mapato makubwa ya mauzo ya nje ya dhahabu, utalii, na bidhaa za kilimo katika nusu ya pili ya mwaka 2026.
Mwezi Mei 2026, mfumuko wa bei wa jumla nchini ulikuwa 4.2%, kiwango cha juu zaidi kurekodiwa katika kipindi cha miaka mitatu, kikipanda kutoka 4% mwezi Aprili, kwa mujibu wa uchambuzi wa takwimu uliofanywa na Nukta Habari.
Uchumi kukua kwa zaidi ya asilimia nusu ya pili 2026
Mapema Julai mosi, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) nchini Tanzania ilishusha kidogo bei za mafuta licha ya shinikizo linaloendelea kutoka kwa wabunge, upinzani na umma wakitaka bei hizo zishushwe kwa kiasi kikubwa ili kupunguza gharama za maisha.
Mwezi uliopita, Wizara ya Fedha ilidumisha makadirio ya ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo kuwa 6.3% mwaka 2026, ikipanda kutoka 5.9% iliyorekodiwa mwaka 2025, huku kukiwa na vihatarishi vinavyoendelea kusababishwa na mgogoro wa sasa wa Iran.
Tutuba amesema MPC ililiridhishwa na ukuaji imara wa uchumi licha ya changamoto zinazotokana na madhara ya kiuchumi katika soko la dunia kama vile mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati.
“Ukuaji wa Pato Halisi la Taifa (GDP) kwa Tanzania Bara unakadiriwa kuwa karibu asilimia 6 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026, ukichangiwa na utendaji mzuri katika sekta za kilimo, ujenzi, uchimbaji madini, huduma za kifedha, na usafirishaji,” amesema Tutuba akibainisha kuwa katika nusu ya pili mwaka 2026 uchumi unatarajiwa kukua kwa zaidi ya asilimia 6.