Riba ya benki kuu Tanzania yabakia 6% kwa mara ya nne mfululizo

April 4, 2025 3:26 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Uamuzi huo unalenda kuukinga uchumi dhidi ya athari zinazoweza kutokea kutokana na vikwazo vya kibiashara na migogoro inayoendelea duniani.

Dar es Salaam. Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) imeamua kiwango cha riba ya benki kuu kuendelea kuwa asilimia sita katika robo ya pili ya mwaka 2025 ili kuchochea ukuaji wa uchumi nchini wakati Tanzania ikiendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya sera za kiuchumi na kibiashara katika soko la dunia.

Hii ni mara ya nne kamati hiyo imeendelea kubakiza kiwango hicho katika asilimia 6. Mara ya kwanza kiwango hicho kilianza kutumika robo ya pili ya mwaka 2024 baada ya kupanda kidogo kutoka asilimia 5.5 kilichoanza robo ya kwanza mwaka 2024 wakati mfumo mpya wa sera ya fedha ulipoanza kutumika rasmi. 

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dk Yamungu Kayandabila amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam kuwa uamuzi wa kamati kutobadili Riba ya Benki Kuu (CBR) unalenga kuhakikisha kiwango cha ukwasi kinaendelea kuwa cha kutosha katika uchumi  na kudhibiti mfumuko wa bei kubaki chini ya lengo la asilimia tano. 

Hata hivyo, Dk Kayandabila amesema kuwa kutokutabirika kwa sera za biashara na migogoro ya kisiasa duniani vinaweza kuathiri mwelekeo wa mfumuko wa bei na ukuaji wa uchumi katika kufikia malengo yake.

“Uamuzi huu wa kamati unalenga kuukinga uchumi dhidi ya athari zinazoweza kutokea kutokana na vikwazo vya kibiashara na migogoro ya kisiasa duniani,” amesema Dk Kayandabila.

Itakumbukwa hivi karibuni Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza viwango vipya vya ushuru kwa bidhaa zinazoingizwa nchini humo uamuzi unaokusudia kuwafanya Wamarekani kununua zaidi bidhaa zinazozalishwa nchini humo.

Uamuzi huo huenda ukaathiri nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania kutokana na kupungua kwa mauzo ya bidhaa nchini Marekani ambapo kwa sasa bidhaa zote kutoka nchini zitatozwa ushuru wa asilimia 10.

Kwa mujibu wa Kayandabila kamati hiyo ilibaini kuimarika kwa shughuli za kiuchumi katika nchi zilizoendelea na zile zinazoibukia kiuchumi jambo linalotarajiwa kuendelea katika robo zijazo za mwaka 2025.

Bosi huyo wa BoT amesema kuna viashiria chanya vya ukuaji wa uchumi katika ngazi ya dunia na ndani ya nchi ambavyo kwa sehemu kubwa ni mwendelezo wa ukuaji uliorekodiwa katika robo ya mwisho ya mwaka 2024. 

Naibu Gavana wa BoT Dk Yamungu Kayandabila alipokuwa akiwasilisha ripoti ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya benki hiyo kwa wanahabari na viongozi wa benki leo Aprili 4, 2024. Picha l BoT

Ripoti za uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinabainisha kuwa mwaka 2024 uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa asilimia 5.4 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024 na unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.6 katika robo ya tatu na asilimia 5.7 katika robo ya mwisho ya mwaka.

Aidha, Tanzania iliripoti ongezeko la ukwasi katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 kutokana na ongezeko la matumizi ya Serikali pamoja na kupungua kwa fedha taslimu nje ya mfumo wa benki jambo lililosaidia kupunguza mahitaji ya mikopo kutoka Benki Kuu. 

Ukwasi bado changamoto benki ndogo

Dk Kayandabila amesema MPC ilibaini kuwa baadhi ya benki ndogo zimeendelea kukumbana na changamoto ya kupata ukwasi kwa gharama nafuu na hivyo kuchangia riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki kubaki karibu ya wigo wa juu wa riba ya Benki Kuu (CBR).

Katika kudhibiti mfumuko wa bei, amesema wanatarajia mfumuko wa bei utaendelea kuwa tulivu katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 ukibakia katika viwango vya kati ya asilimia 3.2 na asilimia 4 ambayo ni ndani ya lengo la ukomo asilimia 5.

Katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara ulikuwa wastani wa asilimia 3.2 na huko Zanzibar mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 4.8 mwezi Februari 2025 kutoka asilimia 5.3 mwezi Januari 2025, kutokana na kupungua kwa bei za chakula. 

Wanahabari pamoja na viongozi wa taasisi za kifedha ikiwemo mabenki wakimsikiliza Naibu Gavana wa BoT aliyekuwa akiwasilisha kiwango cha riba cha BoT kwa robo ya pili ya mwaka 2025 / Picha l BoT

Matarajio ya kuimarika kwa mfumuko wa bei, amesema yanatokana na uwepo wa chakula cha kutosha, utulivu wa thamani ya Shilingi dhidi ya fedha za kigeni, umeme wa uhakika na kushuka kwa bei za bidhaa katika soko la  la dunia hususan mafuta ghafi. 

“Mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa wastani wa asilimia 12.7, ambapo sehemu kubwa ya mikopo hiyo ilielekezwa kwenye shughuli binafsi hususan biashara ndogo na za kati, ikifuatiwa na shughuli za kilimo, biashara na uzalishaji viwandani,” ameongeza Dk Kayandabila.

Bosi huyo wa BoT amesema thamani ya Shilingi inatarajiwa kuendelea kuwa imara katika robo ya pili ya mwaka 2025 kutokana na kuimarika kwa urari wa malipo ya kawaida, ongezeko la mapato ya fedha za kigeni nchini na uwepo wa akiba ya kutosha ya fedha za kigeni. Hadi sasa, amesema kuna akiba ya fedha inayofikia zaidi ya Dola za Marekani bilioni 5.6, kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kwa miezi minne na nusu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks