Si kweli : Serikali imeongeza likizo ya wanafunzi kwa siku 7
- Serikali yakanusha, yasema shule zitafunguliwa Julai 6, 2026 kama ilivyokua awali.
- Nukta Fakti yabaini dosari katika barua ikiwemo muundo wa kiutawala, jina na sahihi ya kiongozi mwenye thamana pamoja na ukakasi kwenye sababu za kuongezwa kwa likizo.
Dar es Salaam. Leo katika mitandao ya kijamii kumeibuka mjadala mpana baada ya kusambaa kwa taarifa inayodai kuwa Serikali imeongeza likizo kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa siku saba, jambo ambalo sio la kweli.
Taarifa hiyo iliyotolewa leo Julai 1, 2026 kupitia chapisho feki la barua yenye mfanano na barua kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ikieleza kuwa shule zitafunguliwa Julai 13, 2026 badala ya Julai 6 mwaka huu kama ilivyopangwa awali.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa sababu za kuongeza kwa likizo hiyo ni kuwawezesha wanafunzi na walimu kupata mada wa kutosha wa mapumziko.
“Ofisi ya Rais TAMISEMI inapenda kuwajulisha kuwa, kutokana na uchovu wa likizo kwa wanafunzi, walimu na watumishi wote wa elimu baada ya kipindi kirefu cha mapumziko, imeamua kuongeza siku 7 baadae ya shule kufunguliwa,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.

Hata hivyo, timu ya wathibitishaji wa taarifa ya Nukta Fakti imebaini taarifa hiyo sio halali na haijatolewa na mamlaka husika, hivyo wananchi waipuuze.
Mambo yaliyobainika katika taarifa hiyo
Nukta Fakti imebaini dosari kadhaa katika barua hiyo ikiwemo muundo wa kiutawala na ukakasi katika sababu zilizoorodheshwa pamoja na jina na sahihi ya kiongozi mwenye dhamana aliyetoa taarifa husika.
Barua inayosambaa inaonyesha imetoka ‘Ofisi ya Rais Tamisemi’ hata hivyo kwa sasa Tamisemi haiko chini ya Ofisi ya Rais bali Ofisi ya Waziri Mkuu.
Barua pia inaonekana kusainiwa na Waziri wa Elimu, lakini jina na sahihi vilivyopo ni vya Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene M. Mlahabwa, ambaye si Waziri wa Elimu na hana dhamana hiyo.
Kwa sasa, Waziri wa Elimu ni Adolf Mkenda na Naibu Waziri ni Wanu Hafidh Amer na Katibu Mkuu ni Profesa Carolyne Nombo.
Vilevile barua inadai kuwa uamuzi wa kuongeza likizo umetokana na “uchovu wa likizo” kwa wanafunzi, walimu na watumishi wa sekta ya elimu baada ya kipindi kirefu cha mapumziko, hoja ambayo haina mashiko wala uhalisia wa kiutawala.
Wizara ya Elimu kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii imekanusha taarifa hiyo, ikibainisha kuwa si ya kweli na kwamba waraka huo haujatolewa na Tamisemi. Katika ufafanuzi wake, wizara imesisitiza kuwa “Taarifa hii si sahihi, ipuuzwe.”