BoT yabakiza riba ya benki kuu 5.75%
- Imebakiza kiwango hicho kwa mara ya pili na kufanya kitumike kwa robo tatu za mwaka mfululizo.
- Yasema inatarajia ukuaji imara wa uchumi na mfumuko wa bei utabaki thabiti.
Dar es Salaam. Kamati ya Sera ya Fedha imepanga Riba ya Benki Kuu (CBR) kubaki asilimia 5.75 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026 kutokana na matarajio chanya ya ukuaji wa uchumi na mwenendo thabiti wa mfumuko wa bei.
Hii ni mara ya pili kamati hiyo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kubakiza riba ya benki kuu katika kiwango hicho cha asilimia 5.75 tangu ilipotangaza Julai 2025. CBR ni kiwango cha riba kinachotumiwa na BoT kufanya biashara na benki nyingine za biashara.
Katika mkutano wake na mabosi wa benki na wanahabari jijini Dar es Salaam, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema uamuzi wa kubakiza CBR katika kiwango hicho ulizingatia kwamba mfumuko wa bei unatarajiwa kubaki ndani ya kiwango kinacholengwa cha asilimia 3–5.
Mfumuko wa bei nchini Tanzania umeendelea kuwa imara kwa kipindi cha mwaka mmoja kikiwa chini ya asilimia 4. Malengo ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwa mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma yawe ndani ya wigo wa kati ya asilimia 3.0 hadi 5.0.
“Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) inatarajia hali ya uchumi kuwa nzuri na kwa hivyo kutokubadili Riba ya Benki Kuu (CBR) kusaidia ukuaji imara wa uchumi,” amesema Tutuba.
Tutuba amesema kamati hiyo ilibaini kuwa uchumi wa Tanzania mwaka 2025 ulikuwa imara kwa kukua kwa kasi ya takriban 5.9 kulingana na makadirio ya ukuaji wa asilimia 6, ukichagizwa zaidi na kilimo, madini na ujenzi.
Kwa mujibu wa BoT ukwasi wa fedha za kigeni ulikuwa wa kutosha katika robo ya nne ya mwaka 2025, hasa kutokana na mapato yanayotokana na mauzo ya korosho, utalii, na dhahabu.
“Matokeo yake, thamani ya Shilingi ya Tanzania ilibaki imara dhidi ya Dola ya Marekani (USD), ikionyesha kuimarika kidogo kwa takriban asilimia 0.8 kufikia mwishoni mwa robo,” amesema Tutuba.
Akiba ya fedha za kigeni, amesema, ilikuwa juu ikifikia zaidi ya Dola za Marekani bilioni 6.3, kiwango kinachotosha kuingiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa miezi 4.9, juu ya kiwango pendekezwa cha miezi minne.
BoT inatarajia kuwa akiba ya kigeni itakuwa ni ya kutosha katika robo ya kwanza ya mwaka 2026 kutokana na utendaji mzuri wa mauzo ya nje na bei za wastani za mafuta ya petroli na dizeli.
Latest