BoT yabakiza riba ya benki kuu 5.75% ikitarajia uchumi kukua
Dar es Salaam. Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania imebakiza kiwango cha riba kuu kuwa asilimia 5.75 kutokana na matazamio chanya ya ukuaji wa uchumi na udhibiti wa mfumuko wa bei.
Kiwango hicho cha Riba ya Benki Kuu (CBR) kitatumika katika robo ya nne ya mwaka inayoishia Desemba 2025 baada ya kushuka kidogo kutoka asilimia 6 mapema Julai 2025.
Kwa muda zaidi ya robo nne tangu Aprili 2024 kiwango cha CBR kiliendelea kubaki kwa asilimia 6.
Katika mkutano wake na wanahabari jijini Dar es Salaam, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba amesema makadirio ya benki hiyo yanaonesha kuwa uchumi utaendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha.
Amesema uamuzi wa kubakiza kiwango hicho cha CBR umetokana na tathmini iliyofanyika kuhusu mwelekeo wa mfumuko wa bei ambao unatarajiwa kubakia ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5.
Mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara ulikuwa asilimia 3.4 mwezi Agosti 2025, ndani ya lengo la nchi la asilimia 3 hadi 5 na vigezo vya mtangamano wa kiuchumi kwa EAC na SADC.
Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, uchambuzi wa takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) uliofanywa na Nukta Habari unabainisha kuwa mfumuko wa bei umeendelea kuwa imara kati ya asilimia 3.0 na asilimia 3.4.
“Makadirio ya Benki Kuu yanaonesha kuwa mfumuko wa bei utaendelea kubaki ndani ya lengo, kutokana na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na kibajeti, uwepo wa chakula cha kutosha, na utulivu wa thamani ya Shilingi,” amesema Tutuba jijini Dar es Salaam wakati akisoma taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC).
Mwenendo huo, amesema, utachagizwa pia na uwepo wa umeme wa uhakika, na kupungua kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia.
Bosi huyo wa BoT amesema uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa asilimia 5.4 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 5.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2024 ukichangiwa zaidi na shughuli za uchimbaji madini, kilimo, huduma za fedha na bima, ujenzi, na shughuli za uzalishaji viwandani.
Uchumi kukua kwa 6%
“BoT inakadiria uchumi kuendelea kuimarika, ukikua kwa zaidi ya asilimia 6 katika robo ya pili na ya tatu ya mwaka 2025. Matarajio haya yanachagizwa na uwekezaji unaofanywa na Serikali pamoja na sekta binafsi, na ongezeko la mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi,” amesema Tutuba.
Makadirio hayo chanya ya ukuaji wa uchumi yanakuja licha ya Tanzania kuwepo katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu 2025.
Tutuba amesema BoT imeangazia viashiria vyote ikiwemo uchaguzi na kueleza kuwa hautakuwa na athari katika uchumi kwa kuwa shughuli zote za kiuchumi na kisiasa zinaendelea vema na benki zina ukwasi wa kutosha.
Latest



