Wabunge walia na mmomomnyoko wa madili, Serikali yapendekeza mwarobaini
- Waitaka Serikali kuchukua hatua za haraka ikiwemo kusimamia maadili na kutoa elimu kwa jamii.
Dar es Salaam. Suala la mmomonyoko wa maadili limeibuka bungeni baada ya Wabunge kutoa maoni mchanganyiko huku Serikali ikibainisha mikakati ya kukabiliana nalo.
Hoja hizo za Wabunge zimeibuka baada ya Dk Dorothy Gwajima, Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kuwasilisha bajeti yake bungeni jana Juni 1, 2026 iliyotoa picha halisi ya mapambano dhidi ya mmomonyoko huo wa maadili.
Mbunge wa Jimbo la Katavi, Thomas Maganga wakati akichangia hotuba hiyo aliwataka viongozi wa dini kutumia nguvu wanazotumia kuikosoa Serikali kupambana na mmomonyoko wa maadili unaoendelea kuathiri jamii.
“Viongozi wa dini mnafanya kazi kubwa sana ya kuikosoa Serikali sana, mnatumia nguvu kubwa mno ya kuikosoa Serikali nguvu hiyo hiyo mnayotumia tumieni kukosoa mmomonyoko wa maadili msifanye mambo kwa mafumbo mafumbo,” alieleza Maganga.
Maganga amesema kama hakutakuwa na utashi wa kisheria na kutoa nafasi kwa vyombo kusimamia maadili, kuna uwezekano mkubwa Taifa likakosa nguvu kazi hasa kwa vijana wa kiume.
Mbunge huyo aliyetumia vitabu vya dini kama mwongozo wake amependekeza iundwe taasisi ya kushughulikia wanaokiuka maadili kama ilivyo kwa taasisi ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya lakini akasema bila kufanya hivyo itakuwa ni kazi ya bure.
Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Fadhili Ally Liwaka akichangia hotuba hiyo amesema kuwa vijana wanapozungumza maadili ni vyema hoja ya malezi na madili izungumzwe ili kuyakuza maadili mema katika jamii iwe kwa viongozi au jamii ya kawaida.
Suala la mmonyoko wa maadili limekuwa likiwapasua vichwa viongozi wengi wa Serikali kutokana na kuongezeka kwa utandawazi na matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii yaliyopo nchini.
Mara kadhaa Dk Gwajima amekuwa akijitokeza hadharani kukemea baadhi ya wasanii au Wananchi wanaokiuka maadili ya kitanzania na kuwatupia zigo Jeshi la Polisi kwa wale wanaokaidi kurekebishwa.
Sanjari na jitihada za waziri huyo, hivi karibuni Serikali ilizindua Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mmmonyoko wa Maadili wa miaka 10 kuanzia mwaka 2026/27 hadi 2036/ 37 kwa lengo la kulinda, kuimarisha, na kurejesha maadili mema na utamaduni wa Kitanzania.
Serikali yaanika mikakati
Waziri Gwajima wakati akiwasilisha hotuba yake alitoa rai kwa Jamii kushiriki katika kulinda maadili kwa ajili ya manufaa ya vizazi vijavyo.
“Nitoe rai, kwa jamii kwamba suala la maadili sio ajenda ya Serikali peke ya yake bali ni ajenda ya Taifa kwa ujumla, hivyo ni wajibu wetu sote kulinda maadili ya Taifa letu.
…Taifa ni letu na maadili ni ya kwetu kama ilivyoainishwa katika misingi ya DIRA 2050 kuwa na Taifa linalohifadhi, kukuza na kulinda maadili na tamaduni chanya kwa lengo la kuimarisha umoja na utambulisho wa kitaifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema Gwajima.
Pamoja na rai hiyo, Gwajima amebainisha kuwa Serikali imeanza kufanya utambuzi wa baadhi ya matukio yanayochochea mmomonyoko wa maadili na watuhumiwa watakaohusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Pia, Serikali imesema itaendelea na utekelezaji wa Mwongozo wa Maadili na Utamaduni wa Mtanzania (2022) pamoja na Mwongozo wa Uzingatiaji wa Maadili katika Kazi za Sanaa (2023).
Miongozo hiyo imekusudiwa kuimarisha maadili, kulinda misingi ya utamaduni wa Taifa na kudhibiti maudhui ya kazi za sanaa yanayochochea mmomonyoko wa maadili usioendana na mila na desturi za Kitanzania.