Uraia pacha waibua mjadala mpana bungeni

June 1, 2022 5:20 am · David
Share
Tweet
Copy Link
  • Kwa upande wa serikali imejipanga kutoa hadhi maalumu
  • Wabunge wahoji kwanini Serikali iogope kuwapa uraia pacha wananchi wake

Dar es salaam. Suala la uraia pacha limeibuka tena bungeni leo baada ya Wabunge kutoa maoni mchanganyiko huku baadhi wakihoji sababu za Serikali kuendelea kusita kuwapatia Watanzania waishio nje ya nchi haki hiyo.

Kwa sasa, Serikali ya Tanzania imeweka mpango wa kuwapa hadhi maalumu Watanzania wanaoshi nje ya nchi (Diasporas) ili watambuliwe rasmi lakini baadhi ya watu wanaona utaratibu huo bado utawanyima fursa muhimu raia hao.

Wabunge wameibua mjadala wa uraia pacha leo Mei 31, 2022 wakati wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliyowasilishwa na Balozi Liberata Mulamula. 

Wizara hiyo inapanga kutumia Sh208.3 bilioni katika mwaka wa fedha wa 2022/23.

Balozi Mulamula amesema mpango huo unatoa fursa kwa Watanzania waishio nje kuja nyumbani na kuwekeza katika sekta mbalimbali na kufanya shughuli kwa uhuru. 


Soma:


Wabunge wachachamaa juu ya uraia pacha

Baadhi ya Wabunge wamesema kutokuwapa Watanzania hao uraia pacha ni kupoteza kizazi cha raia wake wanaoishi nje ya nchi ambao ni muhimu katika kutuunganisha na mataifa mengine. 

“Kukiacha kizazi cha Tanzania kukaa nje bila uraia pacha Mheshimiwa Naibu Spika naona kwamba tunapoteza kizazi chetu ambacho kinakaa ughaibuni,” amesema Tasika Mbogo, Mbunge wa Viti Maalumu.

Akichangia mada hiyo,  Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby amesema kwa nini Serikali inasita kuridhia uraia pacha huku akitaka itoe semina ya kina kuhusu suala hilo kwa sababu bado halijaeleweka vizuri kwa watu.

“Uraia pacha ni muhimu kwa nchi yoyote hata kama kunakuja hilo neno la hadhi maalumu au chochote…..Wizara ya Mambo ya Nje hawajawai kufanya semina ituambie je kuna shida gani kwenye uraia pacha?,” amehoji Shabiby.

“Mimi nakuomba (Waziri Mulamula)  unapokuja kuhitimisha hapa uje utuambie hiyo inayoitwa hadhi maalumu ni kitu gani hasa humo ndani kuna vitu vya namna gani,” amesema Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba.

Michango ya Wabunge iliyotolewa leo ni muendelezo wa mjadala mpana kuhusu uraia pacha ambao Watanzania wanaoishi nje ya nchi wamekuwa wakiupigania ili kufaidika na fursa zilizopo nchini.

Hata hivyo, Serikali imeendelea kutekeleza mchakato wa mabadiliko ya Sera ya Mambo ya Nje, ambapo moja ya jambo ambalo linategemewa kuwepo kwenye sera hiyo ni  Watanzania waishio nje ya nchi kupata hadhi maalum” itakayowawezesha kupata fursa mbalimbali wanazopoteza wanapochukua uraia wa nchi nyingine, ikiwemo umiliki wa mali zisizohamishika, kama vile ardhi.

Katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26), Watanzania waishio nje ya nchi wamejumuishwa katika mipango ya kuipatia Serikali fedha kupitia uwekezaji.

Uganda, Kenya na Rwanda ndiyo nchi pekee za Afrika Mashariki ambazo zinaruhusu uraia pacha.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW