Mwanyika, Pareso, Giga wachaguliwa wenyeviti wa Bunge la 13

January 28, 2026 2:55 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya Wabunge kuwapa kura za ndio ikiashiria ridhaa ya kukubaliana na maamuzi yaliyofanywa na kamati ya uongozi wa Bunge.

Dar es Salaam. Bunge la Tanzania limewachagua wabunge watatu kuwa wenyeviti wa Bunge la 13 ambao wataratibu mijadala, na kuhakikisha nidhamu na taratibu za Bunge zinafuatwa ili shughuli za kutunga sheria na kuisimamia Serikali ziende kwa ufanisi

Wabunge hao waliopewa dhamana leo Januari 28, 2026 ni pamoja na Deo Mwanyika Mbunge wa jimbo la Njombe Mjini (CCM) , Cecilia Pareso, Mbunge wa Viti Maalum (CCM) pamoja na Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya CCM.

Hiki ni kipindi cha tatu mfululizo kwa Giga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kushika nafasi hiyo wakati Mwanyika akiishika kwa mara ya pili na kwa Pareso ikiwa ni mara ya kwanza.

Spika wa Bunge, Mussa Zungu aliendesha mchakato wa kuwapata viongozi hao kwa kuendesha zoezi la kura ya jumla ya sauti iliyowataka wabunge kujibu ndio au hapana ambapo idadi kubwa ya wabunge walisema ndiyo wakionyesha kuunga mkono hoja na kuwakubali viongozi hao wateule.

“Wanaoafiki kwamba Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mheshimiwa Deo Mwanyika na Mheshimiwa Cecilia Pareso wathibitishwe kuwa wenyeviti wa Bunge waseme ndiyo,” amehoji Spika Zungu, huku wabunge wakishangilia na kupiga makofi kuashiria kuafiki kwao.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Spika Zungu amesema kuwa uchaguzi wa wenyeviti hao unafanyika kwa mujibu wa Kanuni ya Saba ya Kanuni za Bunge za mwaka 2025, inayotamka kuwepo kwa wenyeviti watatu wa Bunge, wenye jukumu la kuongoza vikao kwa kufuata maelekezo ya Spika au Naibu Spika kwa mujibu wa kanuni.

Kwa mujibu wa Zungu mchakato wa uteuzi wa wenyeviti hao ulianiza katika Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo ilipendekeza majina ya wabunge wasiozidi sita kutoka miongoni mwa wenyeviti na makamu wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge, kwa kuzingatia jinsia na pande za muungano. 

Kwa mujibu wa Kanuni ya 13, fasili ndogo ya nne, endapo Kamati ya Uongozi itapendekeza idadi ya majina inayolingana na nafasi zilizopo, Bunge halitapiga kura ya kichwa bali litathibitisha kwa kura ya sauti, chini ya kanuni ya 95. 

“Kwakua nafasi za wenyeviti wa Bunge ni tatu, na kwakua kamati ya uongozi imependekeza majina matatu, bunge hili katika kikao chetu cha leo Januari 28, 2026 linaombwa kuwathibitisha wabunge hao ili kupata uamuzi wa Bunge,” amefafanua Zungu.

Kwa upande wa wateule hao wamepokea nafasi hizo kwa kuwashukuru Wabunge kwa kuunga mkono uteuzi wao na kuahidi kutumikia nafasi hiyoo kwa weredi na uaminifu kwa mujibu wa kanuni zinazowaongoza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks