Nukta Africa yang’ara tuzo za EJAT 2025, yanyakua tuzo nne
- Washindi wa tuzo hizo ni pamoja na Daniel Samson, Esau Ng’umbi na Kelvin Makwinya.
Dar es Salaam. Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa imeendelea kuthibitisha ubora wake katika tasnia ya habari nchini baada ya kuibuka na tuzo nne na waandishi wake watatu kungara katika Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2025.
Tuzi hizo zilizotolewa usiku wa kuamkia leo, Mei 30, 2026 huandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa lengo la kutambua na kuthamini wanahabari wanaofanya kazi kwa ubora na weledi pamoja na kukuza utoaji wa habari zenye manufaa kwa jamii na zinazochangia maendeleo na mabadiliko chanya nchini Tanzania.
Kwa mwaka huu tuzo hizo ziliingiza vipengele vipya ikiwemo tuzo ya taasisi binafsi ya habari iliyofuata sheria na kanuni kwa ufanisi zaidi ambapo Nukta Afrika ilishindanishwa na vyombo vingine vitano na kuibuka mshindi wa pili ikitanguliwa na Azam Media.
Pamoja na hiyo, Nukta Africa ilinyakuwa tuzo nyingine ya umahiri katika kuripoti masuala ya ugonjwa wa seli mundu (sicke cell).
Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen, amesema mafanikio hayo ni matokeo ya uwekezaji wa muda mrefu katika mifumo ya kiutawala na uendeshaji wa taasisi, ambao sasa umeanza kuzaa matunda na kutambuliwa na wadau wa ndani na nje ya kampuni.
Aidha, Dausen amesema tuzo hiyo pia ni uthibitisho kuwa ushauri na mafunzo ambayo Nukta Africa imekuwa ikiyatoa kwa vyombo vya habari na taasisi za mawasiliano na uhusiano kwa umma yanatekelezwa kwa vitendo ndani ya taasisi hiyo.
“Hatuwezi kufundisha jambo ambalo sisi wenyewe hatulifanyi. Tuzo hii ni ushuhuda kwamba Nukta Africa inazingatia misingi ya utawala bora na viwango vya kimataifa, na inaonesha namna ambavyo timu yetu, ambayo kwa kiasi kikubwa ni vijana, imejifunza kufanya kazi kwa kuzingatia viwango hivyo vya kimataifa,” amesema Dausen.

Waandishi wang’ara
Mbali na mafanikio ya kampuni, waandishi watatu wa Nukta Africa ambao ni Daniel Samson, Esau Ng’umbi na Kelvin Makwinya, walitajwa kuwa miongoni mwa washindi wa tuzo mbalimbali za EJAT.
Daniel Samson, Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Nukta Africa, alishinda tuzo ya maudhui bora ya mtandaoni katika kundi la vyombo vya habari vya mtandaoni.
Katika mahojiano na Nukta Habari Samson, ambaye amekuwa akishiriki tuzo hizo kwa miaka minne mfululizo, amesema tuzo hiyo inampa hamasa ya kuendelea kutumia majukwaa ya kidijitali kufikisha maudhui yenye manufaa kwa jamii.
“Ina maana kubwa sana kwangu kama mwandishi wa habari kwani inanipa hamasa ya kuendelea kutumia majukwaa ya mtandaoni, yakiwemo mitandao ya kijamii na tovuti mbalimbali, kuelimisha na kubadilisha jamii,” amesema Samson.
Kwa upande wake, Esau Ng’umbi aliyetwaa tuzo ya Mwandishi Bora Kijana wa Mwaka 2025 na pia kushika nafasi ya pili katika kipengele cha maudhui bora ya mtandaoni amesema ushindi huo ni heshima kubwa kwake na uthibitisho kwamba kazi za waandishi vijana zinatambulika na kuthaminiwa.
Naye Kelvin Makwinya, aliyeshiriki tuzo hizo kwa mara ya kwanza na kushika nafasi ya pili katika kipengele cha uandishi bora wa habari za elimu amesema ushindi huo umempa motisha ya kufanya kazi kwa bidii.
“Mafanikio haya yamenipa motisha ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuongeza ubora katika kazi zangu za kila siku,” ameeleza Makwinya.
Kuhusu Nukta Africa
Nukta Africa ni kampuni ya habari na teknolojia inayojihusisha na utafiti wa masuala ya habari, utoaji wa mafunzo kwa wanahabari na uzalishaji wa maudhui ya kidijitali yanayotumia takwimu.
Kupitia majukwaa yake ya Nukta Habari, Nukta TV, Jiko Point, Nukta Fakti na Nukta The Podcast, kampuni hiyo imeendelea kutoa maudhui yenye ubora na yanayolenga kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Kwa zaidi ya miaka mitano, Nukta Africa imechangia kukuza kizazi cha waandishi wa habari mahiri kupitia mafunzo ya uandishi wa habari za takwimu, habari za kidijitali na uthibitishaji wa taarifa.
Hii ni mara ya sita kwa waandishi wa Nukta Africa kuingia katika orodha ya washindi wa tuzo hizo zinazotambuliwa kuwa miongoni mwa tuzo za juu zaidi katika tasnia ya habari nchini.
Mafanikio ya mwaka huu yanaifanya kampuni hiyo kuandika historia mpya tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018 kwa kuibuka na tuzo nyingi zaidi katika mashindano ya EJAT.