Waandishi watatu wa Nukta Africa kuwania tuzo za EJAT 2024/2025
- Wateule hao ni Daniel Samson ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mafunzo wa Nukta Africa, Kelvin Makwinya na Esau Ng’umbi.
- Hii ni mara ya sita kwa Nukta Africa kuingiza washindani katika tuzo za Ejat.
Arusha/ Dar es Salaam. Waandishi wa habari watatu kutoka Kampuni ya Habari na Teknolojia ya Nukta Africa wameingia katika kinyang’anyiro cha tuzo za umahiri wa uandishi wa habari kwa mwaka 2024/25 zitakazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) Mei 29 mwaka huu.
Wateule hao ni Daniel Samson ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mafunzo wa Nukta Africa, Kelvin Makwinya na Esau Ng’umbi ambao ni waandishi wa habari.
Ernest S. Sungura, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) na Katibu Mtendaji wa MCT amesema walioteliwa ni waandishi 18 pekee.
Sungura aliyekuwa anazungumza na wanahabari leo Mei 19, 2026 jijini Dar es Salaam amesema idadi ya wateule katika mashindano hayo imepungua kutokana na ubora na mabadiliko yalioletwa na mfumo mpya wa kidigitali.
“Mfumo mpya umeleta mabadiliko matatu, uchujaji wa kidigitali kabla ya majaji, tathmini bila upendeleo na kigezo cha ushahidi wa athari…,” amesema Sungura.
Mashindano hayo yamerejeshwa tena mwaka huu baada ya kusitishwa kwa mwaka mmoja yakitoa nafasi kwa waandaaji kujipanga vyema ili kuboresha mfumo wa utoaji wa tuzo hizo kwa kutumia teknolojia ya kidigitali
Sungura ameongeza kuwa awamu hii wametumia vigezo vya msingi takribani kumi katika kuchuja kazi 594 za waandishi walizozikisanya.

Hii ni mara ya sita kwa Nukta Africa kuingiza washindani katika tuzo za EJAT ambapo mwaka 2023 waliingia wateule watatu ambao ni Lucy Samson, Esau Ng’umbi na Joshua Stephen ambapo wote waliibuka kidedea kwa kushika nafasi ya kwanza, ya pili na ya tatu katika vipengele mbalimbali vilivyokuwa vikishindaniwa katika tuzo hizo.
Mwaka 2022 Nukta Africa iliingiza wateule wengi zaidi yaani wanne ambapo Daniel Samson na Suleiman Mwiru waliibuka vinara kwa kuchukua tuzo mbili kila mmoja huku Lucy Samson na Hermina Mkude wakitangazwa washindi wa tatu katika makundi waliyokuwa wakiwania.
Afisa Mwendeshaji wa Shughuli za Nukta Africa, Maphosa Banduka amesema kuwa tuzo hizo ni mojawapo ya njia ya kuwafanya waandishi wa habari kuendelea kujinoa zaidi katika maeneo mbalimbali ya matumizi ya data katika uandishi wa habari.
“Kitovu cha mafanikio haya ni mafunzo yasiyokoma. Kila siku na kila wakati tunajifunza… piatuna namna nzuri ya ‘ku-package content’ ili iweze kuwafikia walengwa kwa ubora na kuleta maana halisi kwa jamii,” ameeleza Banduka.
Kwa upande wake Kelvin Makwinya, mwandishi wa habari wa Nukta Africa ambaye ameingia katika kinyanganyiro cha tuzo hizo kwa mara kwanza amesema uteuzi umempa motisha ya kuendelea kufanya kazi kwa weledi.
“Huu ni mwaka wangu wa kwanza kwenye tasnia, nilitegemea kwa tuzo kubwa kama hizi kuwaona wabobevu pekee. Nashukuru sana kwa baraza kutambua mchango na uwezo wa waandishi wachanga,” amesema Makwinya.
Aidha, ameishukuru Nukta Africa kwa kumpa mafunzo mbalimbali ikiwemo uandishi wa habari za data na uthibitishaji wa taarifa, pamoja na kumnoa katika uzalishaji wa maudhui yenye kuzingatia usahihi, weledi na maslahi ya umma.
Naye Esau Ng’umbi aliyewahi kuwa Mratibu wa Dawati la Habari Nukta Africa amesema amefurahi kuwa miongoni mwa walioteuliwa kuwania tuzo hizo kwa mara ya pili.
“Kuchaguliwa kwenye tuzo hizi inamaanisha kuwa vyombo vya habari vya mtandaoni bado ni sehemu salama kwenye kupata maudhui na kujifunza .Nimepokea habari hii kwa furaha kubwa sana,” amesema Ng’umbi baada ya kupita kwenye chujio la EJAT.
Latest