Wizara ya Habari yaomba kuidhinishiwa bajeti ya Sh525.32 bilioni mwaka wa fedha 2026/27
- Bajeti yaongezeka kwa asilimia 1.1 kutoka mwaka 2025/26.
- Zaidi ya Sh458 bilioni kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo na maandalizi ya matukio makubwa ya kimataifa.
Dar es Salaam .Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeomba Bunge kuidhinisha bajeti ya jumla ya Sh525.32 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya kutekeleza majukumu na vipaumbele vya wizara hiyo.
Waziri Paul Makonda aliyekuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo leo Mei 4,2026 bungeni jijini Dodoma, amesema kati ya fedha zinazoombwa, Sh39.71 bilioni zimetengwa kwa ajili ya mishahara.
“Sh28.65 bilioni matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo Sh 458.19 milioni,” amesema Makonda.
Bajeti ya mwaka 2026/27 imeongezeka kwa Sh5.66 bilioni sawa na asilimia 1.1 kulinganisha na ile ya mwaka unaoishia Juni 20,2026.
Katika mwaka wa fedha 2025/26, Wizara iliidhinishiwa Sh519.66 bilioni, ambapo Sh33.41bilioni zilikuwa kwa ajili ya mishahara, shilingi bilioni 28.07 matumizi mengineyo, na shilingi bilioni 458.19 kwa miradi ya maendeleo.
Waziri huyo ameeleza kuwa katika mwaka 2026/27, Wizara imejipanga kutekeleza maeneo mbalimbali ya kimkakati yatakayochochea maendeleo ya sekta za habari, utamaduni, sanaa na michezo nchini.
Vipaumbele vya wizara
Miongoni mwa maeneo ya kipaumbele ni kukamilisha ukarabati, ujenzi, uboreshaji na utunzaji wa miundombinu ya sekta hizo, pamoja na kukamilisha maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 yatakayofanyika kuanzia Juni hadi Julai 2027.
Aidha, Wizara imepanga kuhakikisha Tanzania inakuwa mwenyeji wa Mashindano ya 74 ya Urembo ya Dunia (Miss World), sambamba na kuendelea kuhuisha sera, sheria, mikakati, miongozo na kanuni mbalimbali kwa lengo la kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa shughuli za sekta husika.
Vipaumbele vingine ni pamoja na kuimarisha matumizi ya Kiswahili katika ngazi ya kikanda na kimataifa, kuwezesha ushiriki wa timu za taifa katika mashindano ya kimataifa, kuboresha elimu na mafunzo katika tasnia za utamaduni, sanaa na michezo, pamoja na kuimarisha mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kushiriki katika kukuza sekta hizo.
Wizara pia imejipanga kuratibu na kusimamia matamasha, shughuli na matukio makubwa ya kitaifa na kimataifa yanayohusiana na habari, utamaduni, sanaa na michezo.

Latest