Hawa hapa wagombea ubunge 2025 waliopita bila upinzani CCM

July 30, 2025 4:19 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na Ridhiwani Kikwete, Salma Kikwete, Dk. Doto Biteko, na wengine wawili kutoka visiwani Zanzibar.

Dar es salaam. Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikitangaza uteuzi wa awali wa wagombea wa nafasi za ubunge kwa majimbo yote 272 ya Tanzania Bara na Visiwani, wapo baadhi ya wagombea akiwemo Ridhiwani Kikwete wamepita bila mpinzani ndani ya chama hicho. 

Mchakato huo ulihusisha wagombea zaidi ya 5,000 waliojitokeza kuwania ubunge huku zaidi ya 30,000 wakichukua fomu kuwania nafasi za udiwani.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla  akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi za Chama hicho jijini Dodoma Julai 29, 2025 alisema uteuzi huo umefanywa kwa kuzingatia sifa, uwezo wa mgombea, na mahitaji ya kisiasa ya majimbo husika.

Kati ya wagombea walioteuliwa wapo ambao wamekosa nafasi katika hatua hiyo ya awali na wengine watachuana katika mchakato wa kura za maoni kutoka kwa wajumbe ili kumpata mgombea mmoja atajayepeperusha bendera ya CCM.

Licha ya hofu ya wajumbe kuendelea kutawala baina ya wagombea walioteuliwa, Nukta Habari imefanya uchambuzi na kubaini wagombea watano walioteuliwa peke yao kwenye majimbo yao na hivyo kuwafanya watembee kifua mbele wakisubiri kupigiwa kura za ndio au hapana kutoka kwa wajumbe na baadaye kuidhinishwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwaajili ya kupigiwa kura.

Je, ni kina nani hawa? 

Moja kati ya wagombea hao ni Ridhiwani Kikwete, mtoto wa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Ridhiwani aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2014 kupitia uchaguzi mdogo katika Jimbo la Chalinze, mkoani Pwani, baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Saidi Bwanamdogo. 

Tangu wakati huo, Ridhiwani amehudumu kama mbunge wa jimbo hilo kwa vipindi viwili mfululizo. 

Wakati wenzake wakisubiri kura za maoni za wajumbe ndani ya chama ili kumpata mgombea mmoja Ridhiwani yeye atasubiri kura za ndio au hapana  ili kukiwakilisha chama chake katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.

Mwingine ni Salma Kikwete, Mke wa Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete nae hajabaki nyuma. Mama Salma aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Mchinga mkoani Lindi mwaka 2020. 

Katika kipindi chake cha kwanza cha ubunge, amekuwa mstari wa mbele katika masuala ya elimu, afya na ustawi wa jamii.

Mwaka huu, hajapata mpinzani katika hatua ya uteuzi wa awali ndani ya CCM iwapo wajumbe watampa kura ya ndio huenda ikawa njia nyeupe ya yeye kuendelea na ubunge kwa muhula wa pili.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Mashaka Biteko, ameendelea kudhihirisha ushawishi wake ndani ya CCM na kwa wananchi wa Jimbo la Bukombe, ambako amekuwa mbunge tangu mwaka 2015. 

Akiwa mmoja wa wanasiasa vijana waliopanda ngazi za kisiasa kwa kasi, Dk. Biteko hajapata mpinzani katika uteuzi wa awali wa mwaka 2025 na hivyo kupita kama mgombea pekee wa CCM jimboni humo.

Hamad Hassan Chande naye yupo katika orodha hiyo. Chande ambaye ni mbunge wa sasa wa Jimbo la Kojani lililopo Zanzibar, alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2020. 

Katika kipindi chake cha ubunge, amekuwa akihusishwa na juhudi mbalimbali za maendeleo na usimamizi wa masuala ya kijamii kisiwani Pemba.

Kupitia mchakato wa ndani ya CCM mwaka huu, Chande hajakumbana na ushindani wowote, hivyo ameteuliwa kama mgombea wa ccm pekee katika jimbo analowania.

Na anayekamilisha orodha ya watu watano ni Hemed Suleiman Abdulla, ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Abdulla amekuwa Mbunge wa Jimbo la Kiwani tangu mwaka 2020. 

Mbali na nafasi yake ya kisiasa kitaifa, amekuwa akihudumu kwa karibu na wananchi wa jimboni kwake. Na hivyo kufanya safari yake ya kisiasa kupata msukumo zaidi baada ya kuteuliwa tena bila upinzani ndani ya CCM kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka huu.

Je, unadhani ni nini hasa ambacho kimewafanya wagombea hawa wapite moja kwa moja bila kuwa na upindani ndani ya chama? 

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks