Wafahamu vigogo wa CCM walioachwa uteuzi wa wagombea ubunge 2025
- Ni pamoja na wanasiasa wakongwe kama January Makamba, Mrisho Gambo na wengine.
Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imetangaza majina ya wanachama waliopita na kupendekezwa katika mchakato wa kura za maoni kwa nafasi za ubunge kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Majina hayo yametangazwa leo Julai 29, na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Amos Makalla baada ya kusubiriwa kwa zaidi ya saa 24.
Kwenye uteuzi huo wa awali wapo wanaogombea ubunge kwa mara ya kwanza, wanaoomba kuendelea kubaki madarakani na wale ambao walikwisha hudumu kama wabunge wakakaa pembeni na sasa wanataka kurejea tena.
Uchambuzi uliofanywa na Nukta TV umebaini kuna wabunge nane ambao hawajapenya katika hatua hii ya uteuzi wa awali jambo linalomaanisha sasa majimbo yao yatakuwa na sura mpya kuanzia mwakani.
Moja kati ya wanasiasa walioachwa ni January Yusuf Makamba, ambaye aliwahi kuhudumu kama Naibu Waziri wa Mawasiliano na baadaye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Makamba amekuwa Mbunge wa Bumbuli kwa vipindi vitatu mfululizo kuanzia mwaka 2010 hadi 2025 na kuhudumia wananchi wa Bumbuli kwa miaka 15.
Hata mara baada ya kutamatika kwa shughuli za Bunge Makamba alikuwa akihusishwa na nia ya kurejea katika siasa za ubunge katika uchaguzi huu wa mwaka 2025 lakini jina lake limeachwa katika mchakato huu wa awali.
Aidha, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kabla ya kuingia kwenye siasa za ubunge mwaka 2020 na kuwa mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo pia hajatokea katika orodha iliyotolewa na CCM na hivyo safari yake ya kurejea bungeni kukatizwa katika hatua za awali.
Hata hivyo, Paul Makonda aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na mtu ambaye akichuanishwa nae katika majukwaa mbalimbali ya mitandao mara baada ya kutangaza nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini, amepita pamoja na wengine sita.
Aidha, Ole Sedeka ambaye amekuwa akiwatumikia wananchi wa Jimbo la Simanjiro kwanzia mwaka 2005 hadi 2015 na baadae kurudi tena mwaka 2020 pia jina lake limeachwa katika orodha ya majina ya wagombea waliochaguliwa ndani ya chama.
Sedeka pia aliwahi pia kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira
Mwingine ni Pauline Gekul, ambaye aliingia bungeni kwa mara ya kwanza kupitia Chadema mwaka 2010 kabla ya kujiunga na CCM na kuchaguliwa tena mwaka 2015 na 2020 kupitia CCM na kutumikia Jimbo la Babati Mjini. Jina lake halijaonekana kwenye orodha.
Mbunge wa zamani wa Kisesa, Luhanga Mpina, ambaye aliwahi pia kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi katika serikali ya awamu ya tano na kulitumikia jimbo hilo kwa zaidi ya miaka 15 jina lake halijarejea katika mchakato wa 2025 licha ya matarajio ya wengi kwamba angerudi kwenye siasa za ubunge.
Licha ya kuhudumu kama Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na kama Mbunge wa Ilemela tangu mwaka 2015, Dk. Angelina Mabula, jina lake pia lipo miongoni mwa yale yaliyokatwa mapema katika mchakato wa uteuzi.
Wa mwisho ni Stephen Byabato ambaye ameongoza kama Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini kuanzia Oktoba 2020, na ametumikia kwa kipindi cha miaka mitano, hadi mwaka 2025.
Byabato pia amewahi kuhudumu kama Naibu Waziri wa Nishati na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Na wengine ni Ndaisaba Ruhoro Jimbo la Ngara, Mohamed Monni Jimbo la Chemba, Godwin Kunambi Jimbo la Mlimba, Justin Nyamoga Jimbo la Kilolo, Shanif Mansoor Jimbo la Kwimba, Idi Kassim Idi Jimbo la Msalala, Zubery Kuchauka Jimbo la Liwale, Emmanuel Ole Shangai Jimbo la Ngorongoro, Idd Mpakate Jimbo la Tunduru Kusini,
Hasani Kungu Jimbo la Tunduru Kaskazini, Vedastus Mathayo Jimbo la Musoma Mjini, Goerge Mwenisongole Jimbo la Mbozi, Nicodemas Maganga Jimbo la Mbogwe,Twaha Mpembenwe Jimbo la Kibiti, Shabani Shekilindi Jimbo la Lushoto, Innocent Kalogeres Jimbo la Morogoro kusini, Flatey Maasay – Jimbo la Mbulu vijijini, Alfred Kimea Jimbo la Korogwe Mjini pamoja naTaufiq Turkey Jimbo la Mpendae
Latest
