Hawa hapa walioteuliwa ubunge na Kamati Kuu CCM wakitokea Chadema

August 28, 2025 11:20 am · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na Esther Matiko, Ester Bulaya,na Hawa Mwaifunga ambao hawakupenya kwenye kura za maoni za wajumbe.

Dar es Salaam. Mbivu na mbichi katika uteuzi wa wagombea ubunge kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimeshajulikana mara baada ya Halmashauri Kuu ya chama hicho kukamilisha kazi ya kuchekecha majina yaliyopigiwa kura za maoni na wajumbe ili kupata wawakilishi wa majimbo kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025.

Macho na masikio ya Watanzania wengi yalikuwa kwenye nafasi za ubunge ambapo matokeo yamepokelewa kwa shangwe kwa waliofanikiwa kupita huku wengine wakiangukia pua licha ya kuongoza katika kura za maoni za wajumbe.

Nafasi za kugombea hasa ubunge zimeonekana kuwa na mchuano mkali ndani ya CCM kwa mwaka wa Uchaguzi wa 2025

Ushindani huo ulitokana na ongezeko la wanachama kutaka kuwania nafasi hiyo huku wengine wakitoka katika vyama vyao na kujiunga na CCM ili kutanua mawanda ya kupata nafasi ya uongozi ngazi ya jimbo.

Miongoni mwa waliojiunga na CCM ni pamoja na baadhi ya waliokuwa wabunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambapo watano kati yao wameteuliwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyopatikana baada ya maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM Taifa, walioteuliwa ni Esther Matiko (Tarime Mjini), Ester Bulaya (Bunda Mjini), Hawa Mwaifunga (Tabora Mjini), Kunti Majala (Chemba) na Jesca Kishoa (Iramba Mashariki.) 

Itakumbukwa awali Kamati Kuu ilipitisha majina ya wagombea 11 katika uteuzi wa awali ili yaende yakapigiwe kura za maoni na wajumbe ambapo Jesca Kishoa na Kunti Majala pekee ndio walifanikiwa kuvuka katika kinyang’anyiro hicho. 

Uamuzi wa Kamati kuu umemrudisha Ester Bulaya, ambaye alishika nafasi ya tatu katika kura za maoni za wajumbe akipata kura 625 pekee, na kuachwa mbali na aliyekuwa mshindi Robert Maboto aliyepata 2,545 na Kambarage Wasira aliyepata 2,032.

Aidha, Esther Matiko aliyepata kura 196 ameteuliwa kupeperusha bendera ya CCM katika jimbo la Tarime Mjini dhidi ya Michael Kembaki aliyekuwa mshindi kwa kura 1,568 za wajumbe jimboni humo. 

Huku, Hawa Mwaifunga aliyepata kura 326 katika kura za maoni akipewa kibali dhidi ya Shaaban Mrutu aliyeshinda kwa kura 6,612.

Maamuzi ya kamati kuu yamepokelewa kwa sura tofauti na kuibua mijadala katika majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii huku baadhi ya wadau wakiunga mkono na wengine kuonyesha kutounga mkono maamuzi hayo.

Kwa sasa hatua inayofuata ni majina ya wagombea hao kupelekwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na kama hakutakuwa na mabadiliko yeyote, wao ndio watakao peperusha bendera ya CCM katika nafasi ya ubunge kwenye majimbo yao.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks