CCM yabadili katiba kuruhusu uteuzi majina zaidi ya matatu wagombea ubunge, udiwani
- Ni baada ya pendekezo hilo kupitishwa kwa asilimia 99.8 ya kura za wajumbe, CCM yasema mabadiliko hayo ni kwa ugombea ubunge tu kwa mwaka huu.
Dar es salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanya mabadiliko ya katiba yake yanayoiruhusu kamati kuu kupitisha majina zaidi ya matatu katika uteuzi wa awali wa majina ya wanaogombea nafasi ya udiwani, ubunge au ujumbe wa baraza la wawakilishi kwa tiketi ya chama hicho.
Uamuzi huo umefikiwa leo Julai 26, 2025 mara baada ya wajumbe 1,912 kupiga kura za ndio.
Wajumbe hao ni kati ya ,931 waliotakiwa kupiga kura ambapo waliohudhuria na kupiga kura ni 1,915 na kwa mujibu wa matokeo, ni kura tatu pekee ndizo ziliharibika na hakuna kura ya hapana.
Hatua hiyo imefanya azimio hilo kupita kwa asilimia 99.8 na kufikia matakwa ya katiba ya CCM ambayo inataka uamuzi wa mabadiliko ya katiba ufanyike mara baada ya kupitishwa kwa kura ya theluthi mbili ya wajumbe wa Mkutano Mkuu.
Zoezi la upigaji kura limeongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kupitia mkutano maalumu uliofanyika kwa njia ya mtandao.
Kwa mujibu wa Samia uamuzi wa kufanya marekebisho ya katiba ya CCM umefikiwa mara baada ya kupokea idadi kubwa ya watia nia za ugombea katika majimbo na hivyo wameona ni muhimu wakangeza idadi ili kutoa nafasi kwa wagombea wengi kadiri ya wajumbe watakavyoamua.
“Kuna maeneo yana wagombea wengi, 39 hadi 40, kwaiyo tumeona kwenda na watatu kati ya watu wengi hao si jambo la busara. Papo hapo Kamati kuu imebanwa na katiba hatuwezi kuongeza majina, kwaiyo tumeamua kurudi kwenu kuja kuomba ridhaa ya kubadilisha katiba kuongeza maneno kama kamati kuu itakavyoona inafaa,” ameeleza Mwenyekiti wa CCM.
Hapo awali Kamati Kuu ya Halmashauri ya CCM Taifa ilikuwa na mamlaka ya kufanya uteuzi wa awali wa majina ya wanachama wanaogombea nafasi ya ubunge na Ujumbe wa baraza la wawakilishi yasiyozidi matatu ili waende wakapigiwe kura za maoni.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Rais Samia, mabadiliko hayo hayatahusisha watiania wa ugombea wa Udiwani kwa mwaka huu ambao Kamati ya Siasa ya Halmashauri ya CCM ya mkoa ilipewa mamlaka ya kufanya uteuzi wa majina yasiyozidi matatu kwa nafasi ya kupigiwa kura za maoni kwenye kata kwa kuwa mchakato wao umeshaanza.
“Kwa madiwani mchakato utakwenda kama ulivyo, kwa wabunge ndio marekebisho haya yataanza kufanya kazi” amesisitiza Rais Samia.
Hii si mara ya kwanza kwa CCM kufanya mabadiliko ya katiba yake kwa mwaka huu, itakumbukwa kuwa mwezi Januari 2025, CCM ilifanya mabadiliko ya katiba ambapo moja ya maeneo yaliyofanyiwa marekebisho ni kufanya vikao kwa njia ya mtandao pale itakapo lazimika.
Hata hivyo, wakati CCM inafanya mabadiliko ya katiba ya chama chake, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza rasmi kuwa zoezi la upigaji kura la Uchaguzi Mkuu wa Tanzania litafanyika siku ya Jumatano, Oktoba 29, 2025. Ambapo kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 28, kabla ya siku ya kupiga kura.
Je, kuongezeka kwa idadi ya majina ya wagombea watakaopigiwa kura, kutaleta ahueni na na kupunguza hofu kwa watia nia juu ya ukatwaji wa majina iliyochangiwa na mijadala mbalimbali iliyokuwa ikiibuliwa katika majukwaa ya mitandao ya kijamii? Ni jambo la kusubiri.
Latest



