Fahamu kuhusu homa ya ini muuwaji wa kimya kimya

July 28, 2025 3:42 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Kila sekunde 30 mtu mmoja hupoteza maisha kwa sababu ya ugonjwa huu.
  • Takriban watu 6,000 huambukizwa homa ya ini kila siku duniani kote. 

Dar es Salaam. Leo, dunia nzima inaungana kuadhimisha Siku ya Homa ya Ini Duniani si kwa ubaya ila ni katika hali ya kujitafakari na kuweka mipango ya kutokomeza kabisa ugonjwa huu unaoua kimya kimya ambapo kila baada ya sekunde 30 mtu mmoja hupoteza maisha.

Homa ya ini ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyoshambulia ini la binadamu. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya leo Julai 28, 2025 imesema kuna aina tano kuu za virusi hivyo ambazo ni A, B, C, D, na E.

Kati ya aina hizi, virusi vya homa ya ini B na C ndivyo vinavyoongoza kusababisha ugonjwa mkali wa homa ya ini, na huenezwa kupitia damu au majimaji ya mwili.

Ugonjwa huu umekuwa tishio kubwa kwa afya ya umma duniani, kwani ndio chanzo kikuu cha saratani ya ini.

Mbaya zaidi, huendelea kukua pole pole bila dalili za moja kwa moja, hadi unapotishia maisha.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), kila baada ya sekunde 30 mtu mmoja duniani hufariki kwa sababu ya homa ya ini aina B au C.

Takriban watu 6,000 huambukizwa homa ya ini kila siku duniani kote na vifo vitokanavyo na ugonjwa huu vinaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Takwimu za WHO zinaonesha idadi ya vifo iliongezeka kutoka milioni 1.1 mwaka 2019 hadi milioni 1.3 mwaka 2021.

Hata hivyo, WHO inabanisha kuwa mnamo mwaka 2022, watu milioni 304 walikuwa wakiishi na maambukizi sugu ya homa ya ini aina ya B na C duniani.

Katika picha hizi unaweza kujionea kwa urahisi namna ugonjwa huu unavyoathiri afya ya ini la binadamu. Picha/ Canva.

Licha ya ukubwa wa tatizo hili, ni asilimia 45 tu ya watoto wachanga waliopokea chanjo ya homa ya ini aina ya B ndani ya saa 24 baada ya kuzaliwa. 

Wizara ya afya inabainisha kuwa watu wanaofanya ngono bila kutumia kinga na wapenzi wengi, na watumiaji wa dawa za kulevya wanaochangia sindano wapo kwenye hatari zaidi ya kuambukizwa ugonjwa huu.

Sio kila mwenye macho ya njano hutabiriwa kuwa na homa ya ini isipokuwa kuwa na macho ya njano kwa baadhi ya watu ni dalili moja wapo ya kuwa na ugonjwa huu. Picha/ Canva.

Vile vile, watoto wachanga wanaozaliwa na mama mwenye maambukizi ya homa ya ini, pamoja na watu walio na wenza waliothibitika kuwa na virusi vya ugonjwa huo.

Kulingana na wizara hiyo, njia kuu za maambukizi hutofautiana kulingana na aina ya virusi. 

Aina ya A na E huenea kupitia chakula au maji yaliyochafuliwa na kinyesi chenye virusi, ilhali aina ya B, C na D husambaa kupitia damu, majimaji ya mwili, kushiriki sindano au vifaa vyenye ncha kali na kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua.

Muonekano wa virusi vinavoharibu ini la binadamu na kusababisha homa kali ya ini. Picha/ Canva.

Mbali na virusi, sababu nyingine zinazochangia uharibifu wa ini ni pamoja na matumizi ya dawa za hospitali bila ushauri wa kitaalamu, matumizi ya dawa za asili au miti shamba zisizosajiliwa, pamoja na unywaji wa pombe kupita kiasi.

Siku ya Homa ya Ini Duniani huadhimishwa kila mwaka Julai 28, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu homa ya ini, ambayo ni uvimbe wa ini unaosababishwa na virusi na unaweza kupelekea ugonjwa mbaya wa ini pamoja na saratani ya ini.

Ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha kuwa anafanya vipimo mapema ili kujikinga na janga hili. Picha/Canva.

Homa ya ini ni ugonjwa unaoua kimya kimya, lakini unaweza kuzuilika ni wajibu wetu kuchukua hatua, kupima afya zetu, kutumia kinga na kuelimishana.

/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
25 May, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
25 May, 2026
No active movers today
Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
MIKOA 5 YA KIPOLISI INAYOONGOZA KWA MAKOSA BARABARANI

MIKOA 5 YA KIPOLISI INAYOONGOZA KWA MAKOSA BARABARANI

Nukta TV

SERIKALI YAKAMILISHA MAZUNGUMZO MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA

SERIKALI YAKAMILISHA MAZUNGUMZO MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA

Nukta TV

🔴LIVE: KAPINGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA 2026/2027 BUNGENI.

🔴LIVE: KAPINGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA 2026/2027 BUNGENI.

Nukta TV