Fahamu magonjwa matano yanayosabisha vifo vingi duniani

July 14, 2026 5:19 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Magonjwa hayo ni pamoja na saratani na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

Dar es Salaam. Licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na huduma za afya duniani mamilioni ya watu bado hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa mengi ambayo yangeweza kuzuilika au kudhibitiwa endapo yangetambuliwa mapema na wagonjwa kupata matibabu kwa wakati.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyoambukiza (Non-Communicable Diseases (NCDs) yanachangia takribani asilimia 74 ya vifo vyote duniani. 

Hiyo ni sawa na kusema katika kila vifo 10, saba vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza suala linaloacha mjadala mpana juu wa mustakabali wa afya duniani.

Ingawa magonjwa haya huhusishwa zaidi na watu wenye umri mkubwa, Wizara ya afya nchini Tanzania inayataja magonjwa hayo kuwa tishio kubwa kwa afya ya Watanzania kutokana na kuongezeka kwa wagonjwa.

Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa alibainisha hivi karibuni kuwa vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza nchini vimeongezeka kutoka chini ya asilimia 25 katika miaka ya 1980 hadi kufikia asilimia 39 mwaka 2021.

Mchengerwa aliyasema hayo Juni 24, 2026 wakati akifungua mkutano wa tatu wa kimataifa wa PEN-Plus Afrika 2026 jijini Dar es Salaam akiwataka wadau wa sekta ya afya kufanya jitihada za pamoja kuyapunguza.

Kwa mujibu wa WHO yafuatayo ni magonjwa matano yanayosababisha vifo vingi zaidi duniani, sababu zake kuu, watu walio kwenye hatari kubwa pamoja na hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kujikinga.

1. Magonjwa ya moyo na mishipa ya damu

Magonjwa ya moyo na mishipa ya damu ndiyo yanayoongoza kwa kusababisha vifo duniani, yakigharimu maisha ya takribani watu milioni 19 kila mwaka.

Magonjwa ya moyo na mishipa ya damu hutokea pale moyo au mishipa ya damu inaposhindwa kufanya kazi ipasavyo.

 Hali hii mara nyingi husababishwa na mishipa kuziba au kuwa nyembamba kutokana na mrundikano wa mafuta mabaya (cholesterol), jambo linalopunguza mtiririko wa damu kwenda kwenye moyo au ubongo.

Matokeo yake yanaweza kuwa mshtuko wa moyo, kiharusi au kushindwa kwa moyo kufanya kazi na matatizo mengine yanayoathiri mfumo wa mzunguko wa damu.

Sababu kuu zinazoongeza hatari ya magonjwa haya ni pamoja na shinikizo la damu lisilodhibitiwa, kiwango kikubwa cha mafuta mabaya (cholesterol) kwenye damu, kisukari, uvutaji wa sigara, unene uliopitiliza, kutofanya mazoezi na ulaji wa vyakula vyenye chumvi nyingi, mafuta mengi na sukari nyingi.

Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa watu wanaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa hatari ya kupata magonjwa haya kwa kula lishe bora, kufanya mazoezi angalau dakika 150 kwa wiki, kuacha kuvuta sigara, kudhibiti uzito na kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.

2. Saratani

Saratani ni chanzo cha pili kwa kusababisha vifo duniani, ikichangia takribani vifo milioni 10 kila mwaka.

Ugonjwa huu hutokea pale seli za mwili zinapoanza kukua bila mpangilio na kuenea katika tishu au viungo vingine vya mwili.

Uvutaji wa tumbaku ndiyo sababu kubwa inayoweza kuzuilika ya saratani. Sababu nyingine ni matumizi ya pombe kupita kiasi, unene uliopitiliza, kutofanya mazoezi, lishe isiyo bora, pamoja na maambukizi ya virusi kama HPV vinavyohusishwa na saratani ya mlango wa kizazi na virusi vya Hepatitis B na C vinavyoweza kusababisha saratani ya ini.

WHO inakadiria kuwa bila kuimarishwa kwa hatua za kinga na uchunguzi wa mapema, idadi ya visa vipya vya saratani inaweza kufikia karibu milioni 35 kwa mwaka ifikapo mwaka 2050.

Saratani ni chanzo cha pili cha vifo duniani, huku wataalamu wakisisitiza umuhimu wa uchunguzi wa mapema na matibabu ya haraka ili kuongeza nafasi ya kupona. Picha|Canva.

3. Magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji

Magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji, ikiwemo ugonjwa wa kuziba kwa njia za hewa (Chronic Obstructive Pulmonary Disease (COPD)) na baadhi ya aina za pumu sugu, husababisha takribani vifo milioni nne kila mwaka duniani.

Magonjwa haya hutokea pale njia za hewa au mapafu yanapoharibika au kuvimba kwa muda mrefu, hali inayofanya upumuaji kuwa mgumu.

 Baadhi ya magonjwa ya kundi hili ni ugonjwa sugu wa kuziba kwa njia za hewa (COPD) na pumu ambapo wagonjwa wengi hupata kukohoa kwa muda mrefu, kubanwa na kifua na upungufu wa pumzi. 

Sababu kubwa zinazochangia magonjwa haya ni uvutaji wa sigara, uchafuzi wa hewa, matumizi ya kuni na mkaa katika mazingira yasiyo na uingizaji mzuri wa hewa, pamoja na kuvuta kemikali au vumbi katika maeneo ya kazi.

Wataalamu wanashauri kupunguza matumizi ya tumbaku, kutumia nishati safi majumbani, kuboresha ubora wa hewa na kutumia vifaa vya kujikinga katika mazingira yenye vumbi au kemikali ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa haya.

4. Kisukari

Kisukari ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha vifo vingi duniani, kikihusishwa na zaidi ya vifo milioni mbili kila mwaka, ikiwemo vifo vinavyotokana na madhara yake kama ugonjwa wa figo.

Ugonjwa huu hutokea pale mwili unaposhindwa kuzalisha insulini ya kutosha au kushindwa kuitumia ipasavyo, hali inayosababisha kiwango cha sukari kwenye damu kuongezeka.

Insulini inaposhindwa kufanya kazi, kiwango cha sukari kwenye damu huongezeka na kusababisha madhara katika viungo mbalimbali vya mwili. 

Hatari ya kupata kisukari huongezeka kutokana na unene uliopitiliza, ulaji wa vyakula vyenye sukari na mafuta mengi, kutofanya mazoezi, historia ya familia pamoja na kuongezeka kwa umri.

Hata hivyo, uchunguzi wa mapema, matumizi sahihi ya dawa, lishe bora, mazoezi ya mara kwa mara na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya vinaweza kusaidia kudhibiti ugonjwa huu na kuzuia madhara makubwa.

5. Magonjwa sugu ya figo

Magonjwa sugu ya figo husababisha kati ya vifo milioni 1.5 na 1.6 kila mwaka duniani, huku idadi hiyo ikiendelea kuongezeka.

Magonjwa sugu ya figo hutokea pale figo zinapopoteza uwezo wake wa kuchuja taka na maji ya ziada kutoka kwenye damu taratibu kwa kipindi kirefu. 

Kadiri ugonjwa unavyoendelea, taka hujikusanya mwilini na kuongeza hatari ya matatizo makubwa ya afya, ikiwemo kushindwa kabisa kwa figo kufanya kazi. 

Katika hali nyingi, magonjwa haya husababishwa na kisukari na shinikizo la damu lisilodhibitiwa huku sababu nyingine zikiwa ni matumizi ya muda mrefu ya baadhi ya dawa bila ushauri wa daktari, maambukizi ya figo, unene uliopitiliza na sababu za kurithi.

Kisukari na shinikizo la damu lisilodhibitiwa ni sababu kuu zinazochangia magonjwa sugu ya figo duniani. Picha| Canva.

Kwa mujibu wa WHO, vifo vinavyotokana na magonjwa ya figo vimeongezeka kwa karibu asilimia 95 tangu mwaka 2000 jambo linaloonesha umuhimu wa uchunguzi wa mapema, matibabu ya haraka na udhibiti mzuri wa magonjwa yanayoweza kuathiri figo.

Licha ya magonjwa haya matano kuwa miongoni mwa yanayosababisha vifo vingi zaidi duniani, wataalamu wa afya wanaeleza kuwa sehemu kubwa ya hatari inaweza kupunguzwa kwa kufanya mabadiliko ya mtindo wa maisha.

Hatua muhimu zinazopendekezwa ni pamoja na kula lishe bora yenye matunda na mboga za kutosha, kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara, kuacha kuvuta sigara, kuepuka matumizi mabaya ya pombe, kudhibiti uzito wa mwili, pamoja na kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini magonjwa mapema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
14 Jul, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
14 Jul, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia: Kalamu yangu ina hatari, sijawahi kusaini mtu kunyongwa

Rais Samia: Kalamu yangu ina hatari, sijawahi kusaini mtu kunyongwa

Nukta TV

Rais Samia: Matumizi jina Samia, likiwa kila mahali inachosha, tafuteni wengine

Rais Samia: Matumizi jina Samia, likiwa kila mahali inachosha, tafuteni wengine

Nukta TV

Rais Samia: Waendelee kusema hakuna haki, hakuna aliye juu ya sheria zetu

Rais Samia: Waendelee kusema hakuna haki, hakuna aliye juu ya sheria zetu

Nukta TV