BOT : Hatujatoa kibali kuruhusu shughuli za LBL
- Yasisitiza juu ya hatua za kisheria kuendelea kuchukuliwa dhidi ya maafisa wa LBL waliokamatwa.
- Watu binafsi na taasisi zasisitizwa kutojihusisha utoaji wa huduma za fedha bila kibali kutoka Benki Kuu.
Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema haijafanya mazungumzo wala kutoa maelekezo yoyote ya kupewa leseni au kuruhusiwa kwa kampuni inayoitwa Leo Beneath London (LBL), tofauti na taarifa mbalimbali zinazosambaa mitandaoni.
Taarifa ya Emmanuel Tutuba, Gavana wa benki hiyo iliyotolewa leo Februari 25, 2025 inaeleza kuwa kampuni hiyo itachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
“Hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi ya maafisa wa kampuni ya LBL kwa kujihusisha na ulaghai ikiwemo kupokea amana, kutoa riba na kufanya uhaulishaji wa fedha bila leseni ya Benki Kuu ya Tanzania,” imesema taarifa ya Tutuba.
Taarifa ya BoT inakuja wakati ambapo kumekuwa na taarifa kutoka Jeshi la Polisi kuhusu kukamatwa wa viongozi wa kampuni hiyo kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Dar, Geita Mbeya, na Morogoro.
Uchambuzi wa Nukta Habari umebaini watu waliokamatwa wakihusishwa na tuhuma hizo wamefikia 50 ambapo Jijini Dar es Salaam watu 26 walikamatwa, Mbeya ( 5 ), Geita (12) na Morogoro watu saba.

Maafisa 50 tayari wamekwisha kamatwa, jijini Dar es Salaam watu 26 walikamatwa, Mbeya ( 5 ), Geita (12) na Morogoro watu saba, Picha | Global Publishers.
Watu hao wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa Sheria ya Mfumo wa Malipo ya Fedha ya mwaka 2015, kifungu namba 14 pamoja na Sheria ya Utakatishaji fedha ya mwaka 2022 kifungu namba 12.
Wakati jeshi la polisi likiendelea na ukamataji, BoT imewataadhalisha wananchi kuepuka kujihusisha na taasisi, kampuni au mtu binafsi ambaye anatoa huduma za kifedha bila kuwa na leseni kutoka benki hiyo au wasimamizi wengine wa huduma za fedha.
Pia imewaonya watu na taasisi ambazo zinatumia jina la Benki Kuu kuuhadaa umma katika vitendo vyao vya kihalifu, na kuwasihi waache kufanya hivyo mara moja kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakaye keuka taratibu na kuendesha huduma za kifedha kinyume na sheria.
Aidha, BoT imewahimiza wananchi wanaotaka kupata huduma za kifedha kutumia taasisi zenye leseni ambazo orodha yake inapatikana kwenye tovuti ya Benki Kuu (www.bot.go.tz) au wasimamizi wengine wa sekta ya fedha nchini.
Latest