Benki Kuu yatoa onyo kwa wanaokanyaga, kurusha hovyo noti
- Itawachukuliwa hatua watu watakaobainika kutumia vibaya noti.
- Ni pamoja wanaozitumia kama mapambo na kuwatunza watu harusini.
- Yasema vitendo vinachangia noti kuchakaa mapema.
Dar es Salaam. Kama wewe ni mmoja wa watu wenye tabia ya kuwatunza watu fedha kwa kuzirusha na kuzikanyaga katika shughuli mbalimbali ikiwemo harusi, fahamu kuwa uko hatarini kuchukuliwa hatua za kisheria.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema itawachukuliwa hatua watu watakaobainika kutumia vibaya noti za fedha ya Tanzania kwa njia yoyote ikiwemo wanaozirusha hovyo na kukanyaga.
Hatua hiyo inakuja baada ya kubainika kuwa kuna wimbi la vitendo vya matumizi mabaya ya noti katika shughuli mbalimbali za kijamii hususani sherehe za harusi.
“Watu wamekuwa na tabia ya kutunza wahusika wa matukio kwa kuwarushia noti zinazoanguka sakafuni na muda mwingine kukanyagwa, kuziviringisha katika maumbo mbalimbali na kutumia kama mapambo, kuweka kwenye mwili wa mtu ulio loa jasho na matukio yote yanayofanana na hayo,” imeeleza BoT katika taarifa yake iliyotolewa leo Oktoba 28, 2021.
Gavana wa Benki Kuu, Profesa Florens Luoga imesema vitendo hivyo vinaendelea kutokea licha ya BoT na viongozi mbalimbali wa Serikali kwa nyakati tofauti kuvikemea kwani matendo haya yanatweza fedha ya Tanzania ambayo ni moja ya tunu za taifa letu.
“Hivyo basi, BoT inawaonyo wananchi ambao bado wanakaidi onyo hili ambalo limetolewa mara kadhaa kuhusu namna sahihi ya kutunza noti za Tanzania zinazokuwa mikononi mwao kwa kuzitumia kinyume na maadili pamoja na matakwa ya kisheria.” Imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, BoT imewashauri washiriki katika matukio yote ambayo yanahusisha matumizi ya fedha kuandaa vyombo maalum vya kuweka fedha hizo badala ya kufanya vitendo ambavyo havikubaliki.
Wananchi wamehamasishwa kutoa taarifa mara moja kwa Benki Kuu au vyombo vya usalama pale wanapobaini matumizi yasiyo sahihi ya fedha z ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
“Tukitunza fedha zetu tunachangia kuzifanya zitumike kwa muda mrefu na hivyo kuipunguzia Serikali gharama za kuchapisha noti na kutengeneza sarafu mpya ili kusaidia ukuaji wa uchumi wa nchi yetu,” amesema Prof Luoga.
Latest
