Tundu Lissu kuishtaki Tigo, Tanzania mahakama za kimataifa
- Asema mwenendo wa kesi iliyopo Uingereza umetoa mwanya wa kuwafahamu watu wasiojulikana waliotaka kumuua mwaka 2017.
Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu amepanga kuishitaki Serikali ya Tanzania na kampuni ya mawasiliano ya Tigo baada ya kuibuka tuhuma kuwa taasisi hiyo ilitoa taarifa zake kwa Serikali wiki chache kabla ya jaribio la mauaji mwaka 2017.
Jana gazeti la Uingereza la The Guardian liripoti mwenendo wa kesi katika mahakama moja nchini Uingereza ambapo mfanyakazi wa zamani wa kampuni hiyo Michael Clifford alieleza kuwa alifutwa kazi baada ya kukamilisha uchunguzi wa ndani uliobainisha kuwa baadhi ya wafanyakazi walitoa taarifa za Lissu saa 24 siku saba za wiki kwa mamlaka kinyume na sheria.
Taarifa hizo zilihusisha kuonyesha mahali alipokuwa Lissu wakati wote.
Lissu alinusurika kifo Septemba 2017 baada ya watu wasiojulikana kumpiga risasi 16 katika sehemu mbalimbali za mwili wake jijini Dodoma alipokuwa amerejea kutoka bungeni.
Katika mkutano wake na wanahabari jijini Dar es Salaam leo, Lissu amesema mwenendo wa kesi hiyo ni habari kubwa kwa kuwa imetoa mwanya wa kuwafahamu watu waliohusika katika jaribio la kumuua wakati akiwa mbunge.
“Tutakwenda huko waliko na majeshi ya kutosha ya wanasheria wa kimataifa na tukienda huko nimewaambia walianzishe leo. Leo nimezungumza na na Bob Amsterdam (mwanasheria wake) nimemwambia ana mamlaka kamili ya kulianza dhidi ya Tigo na Serikali ya Tanzania,” amesema.

Lissu wakati akiongea na wahahabari jijini Dar es Salaam leo. Kiongozi huyo wa upinzani amesema kuwa tukio alilofanyiwa mwaka 2017 ni la kigaidi. Picha|Fatuma Hussein/Nukta.
Hatua ya kwenda kwenye mahakama ya kimataifa, Lissu amesema inatokana na yeye kutokuwa na imani na mahakama za ndani katika kuendesha shauri hilo.
Hata hivyo, kiongozi huyo machachari na mkosoaji mkubwa wa Serikali, hakueleza ni lini watafungua kesi hiyo nchini Uingereza inayofufua upya mgogoro kati yaLissu, Polisi na Serikali.
‘Tunataka majina ya wasiojulikana’
Lissu amesema kesi iliyoibua tuhuma hizo za kutoa data za wateja bado inaendelea na ndiyo kwanza imeanza kusikilizwa hadharani. Matarajio yao, Clifford aliyewahi kuwa askari polisi wa Uingereza ataendelea kutoa ushahidi na matarajio yao ni kuwa ataendelea kusema mengi zaidi.
“Tutailazimisha Tigo ituambie ilikuwa inawasiliana na kina nani. Nani wa Serikali ya Tanzania aliyeomba mawasiliano yangu yafuatiliwe kwa Saa 24 kwa siku. Tigo itataja majina. Nani aliwaambia na lini?,” amesema Lissu ana kuongeza kuwa wanataka majina ya wasiojulikana kwa miaka saba.
Katika utetezi wake katika nyaraka za mahakama, Millicom iliyokuwa inaimiliki Tigo zamani kabla ya kuuzwa miaka miwili iliyopita, imeeleza kuwa mtumishi huyo hakufutwa kwa kubaini tukio hilo la uvujishaji taarifa bali kwa taratibu nyingine za kampuni.
Tigo Tanzania haijajibu maombi ya kujibu tuhuma hizo na hatua hiyo iliyotangazwa na Lissu.