Mambo 6 yaliyotawala mazungumzo ya Rais Samia, Lissu
- Wamegusia kuhusu ustawi wa Tanzania na Katiba Mpya.
- Pia kushambuliwa kwa Lissu mwaka 2017.
- Umuhimu wa kujenga maelewano na maridhiano ya kitaifa.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo mafupi na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu nchini Ubelgiji kuhusu ustawi wa Tanzania ikiwemo umuhimu wa kuwa na Katiba Mpya.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Zuhura Yunus mazungumzo hayo yamefanyika baada ya Rais Samia kukubali maombi ya kiongozi huyo wa Chadema kukutana naye jijini Brussels jana Februari 16, 2022.
Zuhura katika taarifa yake amesema katika mazungumzo ya wawili hao walijikita katika masuala mbalimbali yenye maslahi na ustawi wa Tanzania.
Muda mfupi baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo, Lissu kupitia ukurasa wake wa Twitter ameweka wazi mambo kadhaa waliyozungumza na Rais ambaye yuko Ubelgiji kwa ziara ya kiserikali akitokea nchini Ufaransa.
Jambo la kwanza ambalo Lissu amemuomba kiongozi huyo mkuu wa nchi ni kumfutia kesi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu ambao wanaokabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kula njama ya kutenda kosa na kufadhili fedha kwa ajili ya vitendo vya ugaidi.
“Nimemwambia Mheshimiwa Rais kwamba afanye analoweza kufanya kwa mamlaka yake kama Rais ahakikishe kwamba hii kesi inaondolewa mahakamani,” amesema Lissu huku akibainisha kuwa hakuna sababu ya kuendelea na hiyo kesi kwa sababu haina afya kwa Taifa.
Mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni Halfan Bwire Hassan, wa pili ni Adamu Hassan Kasekwa, wa tatu Mohamed Abdillahi Ling’wenya na wa nne Freeman Aikael Mbowe.
Lissu amemuomba Rais kuruhusu kufanyika kwa mikutano ya vyama vya siasa kama Katiba ya Tanzania inavyoagiza ili kutoa haki kwa raia ya kujumuika katika shughuli za vyama vya siasa.
“Nimemwambia Mheshimiwa Rais afute zuio la vyama vya siasa hasa vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara pamoja na maandamano kama ambavyo sheria za Tanzania zinavyoruhusu,” amesema Lissu.
Amesema katika mikutano hiyo, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama vitoe ulinzi kwa wahusika.
Soma zaidi:
- Ndugai ahitimisha safari ya miaka tisa ya ubunge wa Lissu
- Lissu arejea Tanzania, apokewa na maelfu ‘airport’
Jambo la tatu kwa mujibu wa Lissu ni kuhusu Katiba Mpya na mfumo mpya wa kidemokrasia wa uchaguzi kwa ajili ya Tanzania utakaohakikisha inaundwa Tume huru ya Uchaguzi na kuhakikisha haki za watu wanaoshiriki uchaguzi zinazingatiwa.
“Agenda yangu ya nne ni inayonihusu mimi pamoja na wenzangu ambao tumelazimika kuikimbia nchi yetu kwa sababu ya vitisho dhidi ya maisha yetu zaidi kuhusiana na mimi mwenyewe.
“Nimemwambia Mheshimiwa Rais kwamba kwa vile ana mamlaka ya kuhakikisha ninapata haki zangu nilizonyimwa baada ya kushambuliwa Septemba 7, 2017,” amesema Lissu.
Kuhusu Watanzania waishio uhamishoni, Lissu amemuomba Rais atamke kuwa wanakaribishwa nyumbani na watakuwa salama endapo watarudi.
Pia Lissu ametaka wale wote waliohusika katika shambulio dhidi yake mwaka 2017 wawajibishwe kwa mujibu wa sheria. Pia amezungumza suala la kuvuliwa ubunge na kunyimwa stahiki zake, akieleza kwamba hayo yamefanyika kinyume na sheria.
Aidha, katika mazungumzo hayo, Lissu amegusia suala la Wabunge 19 wa Viti Maalum ambao wanadaiwa ni kutoka Chadema ambao amesema hawako bungeni kihalali kwani tayari walishavuliwa uanachama wao.
“Kwa sasa siyo wanachama wa Chadema, kuendelea kuwalipa fedha za umma ni kufanya ufujaji,” amesema Lissu.
Lissu amesema suala la mwisho amemuomba Rais kuwaongoza Watanzania kuiponya nchi kutoka katika majeraha na makovu hasa ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na miaka sita iliyopita.
“Nimemwambia Mheshimiwa Rais kuwa ni yeye ana jukumu na ana fursa ya kuisaidia nchi yetu kuponya majeraha yote hayo, vilio, kufuta machozi wote ambao wanalia,” amesema Lissu katika mtandao wa Twitter.
Join me in my Space! https://t.co/LC5iGAhASu
— Tundu Antiphas Lissu (@TunduALissu) February 16, 2022
Lissu amesema Rais Samia amemueleza kuwa ameyapokea na kwamba atayafanyia kazi yote waliyozungumza.
Muda mfupi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na kufanya mazungumzo na Lissu, viongozi na wananchi hasa watumiaji wa mitandao ya kijamii wamepongeza hatua hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Wakili Albert Msando kupitia ukurasa wake wa Instagram amesema “Tuna Rais bora sana. Hatumlinganishi na yeyote. Sio lazima. Kila mmoja ana kipawa chake. Mh. Mama Samia Suluhu Hassan tutamuelewa tukitaka kuelewa.”
Aidha, Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kuwa hatua ya Rais Samia kukubali kukubali kukutana na Lissu ni ya kupongezwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Nickson Simon ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa, “Tutofautiane mawazo na mitizamo lakini tunaungana kitaifa Rais @SuluhuSamia na @TunduALissu katika ujenzi wa Taifa,”
Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamis Kagasheki amesema kila jambo na wakati wake na mazungumzo ni nguzo ya maelewano.
Latest