TIGO yajitenga tuhuma za kutoa taarifa za Tundu Lissu
- Yasema kuwa wakati wa tukio hilo mmiliki wao wa sasa hakuwa mwanahisa.
Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya Honora Tanzania Public Limited (TIGO) imejitenga na tuhuma zilizotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu za kuvujisha taarifa zake kwa Serikali wiki chache kabla ya jaribio la mauaji mwaka 2017.
Taarifa hiyo ya Tigo imekuja siku moja baada Lissu kueleza kuwa ataishtaki kampuni hiyo pamoja na Serikali kwenye mahakama za kimataifa kwa tuhuma za kutoa taarifa ambazo zilifanikisha kushambuliwa kwa risasi nyumbani kwake Area D wakati akitoka bungeni jijini Dodoma.
Mapema Jumanne gazeti la Uingereza la The Guardian liliripoti mwenendo wa kesi katika mahakama moja nchini Uingereza baada ya mfanyakazi wa zamani wa kampuni hiyo Michael Clifford kudai kuwa alifutwa kazi baada ya kukamilisha uchunguzi wa ndani uliobainisha kuwa baadhi ya wafanyakazi wa Tigo walitoa taarifa za Lissu saa 24 siku saba za wiki kwa mamlaka kinyume na sheria.
Hata hivyo, Tigo wameeleza katika taarifa kwa umma kuwa wanatambua taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari kuhusu kesi ya ajira inayoendelea jijini London kati ya mfanyakazi wa zamani wa Millicom, ambayo ndiyo ilikuwa kampuni mama ya Tigo hadi mwaka 2022.
Tigo wamesema mmiliki wao wa sasa hakuwa mwanahisa wakati tukio linalosemekana kutendeka lilipotokea.
“Hivyo, kwa kuwa sisi sio sehemu ya shauri hili, hatuwezi kutoa maoni kuhusu undani wa kesi hii,” imesema taarifa hiyo ya Tigo kwa umma.
“Tunapenda kuchukua fursa hii kuwahakikishia wateja na wadau wetu kwa ujumla kuwa, kipaumbele chetu ni kulinda taarifa binafsi za wateja wetu kwa kuzingatia sheria na kanuni za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Uwepo wa taarifa hizo katika kesi hiyo inayoendelea mahakamani ni moja ya changamoto kwa kampuni hiyo ya mawasiliano hasa wakati huu ambapo kumekuwa na mwamko mkubwa na sheria kali ya ulinzi wa taarifa binafsi.
Baada ya taarifa hizo kuripotiwa na Lissu kufanya mkutano na wanahabari kumekuwa na mjadala mkubwa mtandaoni juu ya usalama wa taarifa za watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini baada ya kuibuka tuhuma hizo.
Latest
