Polisi yawakamata Mbowe, Lissu wakidhibiti maandamano Dar es Salaam

September 23, 2024 12:09 pm ยท Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limewakamata watuhumiwa 14 wakiwemo viongozi wawili wa juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa tuhuma za kukiuka agizo la kutofanya maandamano, ikiwa ni mwendelezo wa kudhibiti wafuasi wa chama hicho waliopanga kuandamana kuishiniza Serikali kukomesha mfululizo wa matukio ya kutekwa na kuuawa kwa watu nchini.

Mapema leo asubuhi polisi walimkamata Makamu Mwenyekiti Bara Tundu Lissu nyumbani kwake Tegeta na baadaye majira ya Saa 4 asubuhi walimkamata Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe akiwa maeneo ya Magomeni baada ya kuwasili kuanza maandamano.

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Jumanne Muliro amewaeleza wanahabari jijini Dar es Salaam leo kuwa limewakamata watuhumiwa 14 wakiwemo Mbowe na Lissu waliokaidi tamko la polisi wakiwa wanendelea kuyapanga na kutaka kufanya maandamano hayo aliyepigwa maarufuku.ย 

Muliro amesema miongoni mwa watu wengine waliokamatwa katika operesheni hiyo ni kada mashuhuri wa Chadema Godbless Lema.

โ€œWamekamatwa pia watuhumiwa wengine ambao walikua wakiendelea kuhamasisha na kujaribu kufanya hayo maandamano akiwemo mtu aliyefahamika kwa jina la Peter Lazaro, Shehe Omar Fakhi, Revocatus Theodori, Paulo Musi, Shabani Kinda, Abubakar Abedi, Emmanuel Ntobi, Sylivester Gasper, Rahel Bundala, Mary Nungu, Bakari Salum na Mary Habibu,โ€ amesema Kamanda Muliro.

Lissu asubuhi alieleza kuwa magari matatu ya polisi yaliyojaa maafisa wenye mavazi ya kukabiliana na ghasia yako nje ya makazi yake na walimuarifu kuwa anatakiwa kupelekwa kwa Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai mkoa wa kipolisi wa Kinondoni.

โ€œNajiandaa kwenda,โ€ amesema Lissu.

Muda mfupi baadaye Chadema ilieleza kupitia mtandao wa X kuwa Lissu amekamatwa na polisi kisha kuondoka nae bila kueleza kituo cha polisi wanakompeleka.ย 

Mbowe yeye amekamatwa eneo la Magomeni mara baada ya kufika na kuanza kuongea na wanahabari. Mwanahabari wetu ameshuhudia polisi wakimzuia Mbowe kuongea na wanahabari kisha kumkamata na kumuingiza kwenye gari la polisi na kuondoka naye.ย 

Polisi wa kuzuia ghasia wakifanya doria katika eneo la Ilala Boma jijini Dar es Salaam kudhibiti maandamano yaliyoitishwa na chama kikuu cha upinzani nchini Chadema. Picha|Fatma Hussein/Nukta.

Jana Septemba 22, Mbowe alieleza kupitia mtandao wa X kuwa wataendelea na mpango wa maandamano na kuwataka wafuasi wa chama hicho kujitokeza kuandamana hata kama viongozi hao watakamatwa au kuuawa.ย 

Hata hivyo, maandamano hayo ya Chadema yalipigwa marufuku na polisi wakisema ni haramu kwa kuwa yamelenga kuleta uvunjifu wa amani.ย 

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha ITV Jumapili usiku Muliro alisema kuwa baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho walitoa matamko kwa nyakati tofauti yanayoashiria uvunjifu wa amani na kwamba yeyote atakayeandamana โ€œhatua kali za kisheriaโ€ zitachukuliwa dhidi yake.ย 

Hata hivyo, bado polisi hawajaweka bayana matamko hayo ya viongozi wa Chadema.

โ€œBaadhi ya matamko ya viongozi hao wa juu yalitupelekea sisi kutoa tamko kwamba maandamano haya sio ya amani kama wao wanavyoyatangaza, sasa matamko gani, tutakutana nayo mahakamani,โ€ amesema Muliro.

Tangu jana usiku hadi kufikia leo asubuhi barabara zote zinazoelekea kwenye makazi ya mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya taifa, zilikuwa zimefungwa huku watumiaji wakisimamishwa, kukaguliwa na kuulizwa shughuli zinazohusiana na maandamano.

Kwa mujibu wa Chadema mke wa Mbowe, Dk Lilian Mtei naye alizuiwa kutoka nyumbani kwake Mikocheni na polisi.

Hatua ya kukamatwa kwa viongozi wakuu wa Chadema inafuata baada ya msimamo wao wa kutositisha maandamano waliyoyatangaza Septemba 11, 2024 yenye azma ya kuishiniza serikali kuchukua hatua baada ya mfululizo wa matukio ya watu kutekwa na kuuawa akiwemo kada na mjumbe wa sekretarieti ya chama hicho, Ally Kibao.ย 

Marufuku hiyo ya Polisi dhidi ya maandamano hayo imekumbana na ukosoaji wa Chadema ambayo inasisitiza haki yake ya kukusanyika kwa amani kama ilivyoainishwa katika sheria za vyama vya siasa za nchi.ย 

Tangu mwishoni mwa juma polisi waliimarisha ulinzi kwa kufanya doria katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam. Mitaa yote ambayo Chadema walipanga kuanzia maandamano ya Ilala Boma na Magomeni Mapipa ilikuwa shwari majira ya asubuhi huku polisi wakiwa na silaha za moto, mabomu ya machozi na vifaa vingine vya kuzuia vurugu wakifanya doria.

Kuanzia Saa 12:30 asubuhi hakukuwa na dalili zozote za watu kuandamaana. Katika eneo la Ilala Boma magari ya polisi yasiyopungua matano na gari la kumwagia maji ya washawasha yalikuwa yamepakiwa karibu na kituo cha mabasi yaendayo haraka hukua polisi wakiwasaka walionekana kuwa na nia ya kuandamana.ย 

Licha kuweka ulinzi mkali katika maeneo yote ya jiji la Dar es Salaam, Eunis Nko, ambaye alijitambulisha kama dada wa mmoja wa watu waliotekwa, Deusdeth Soka, alijitokeza katika eneo la Ilala Boma akiwa na masikitiko na majonzi.

Amesema kuwa Serikali ingetumia nguvu inayotumika kuzuia maandamano kuwatafuta ndugu zao, ingekuwa jambo lenye kuleta amani kwa wananchi.

โ€œKila mmoja anaishi kama ndege sasa hivi, hatujui usalama wetu, na ni jukumu la Jeshi la Polisi kutulinda raia na mali zetu. Sijui kaka zangu wako wapi, halafu leo unanambia ninyamaze, ninyamaze vipi? Tupeni maiti basi! Wangeweza kutulinda kama hivi, wangetupa maiti za kina Soka. Wanipe maiti ya kaka yangu, niipeleke Moshi nikazikeโ€ฆ

โ€ฆAcha tufie barabarani, mimi kama mwanamke, acha nifie barabarani kumtafuta kaka yangu yuko wapi. Hii nguvu inayotumika kuzuia maandamano ingetumika wakati huo, tungejua kaka zetu wako wapi,โ€ amesema kwa huzuni.

Imeandikwa na Davis Matambo na Fatma Hussein.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW