Chadema kuwaburuza mahakamani waliozuia kongamano Mbeya
- Wasema tuhuma za msajili msaidizi wa vyama pamoja na hatua zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi havina msingi.
- Tundu Lissu kuongoza jopo la wanasheria kusimamia kesi hiyo.
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeazimia kuwafungulia mashtaka binafsi Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini Sisty Nyahoza pamoja na Kamisha wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Awadh Haji kwa kukwamisha kufanyika kwa kongamano lililoandaliwa na umoja wa vijana wa chama hicho.
Vijana wa Chadema walikusudia kufanya kongamano kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana Agosti 12, 2024 jijini Mbeya lakini tukio hilo baadaye lilizuiwa kwa barua kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyotolewa Agosti 8, 2024 na kusainiwa na Nyahoza.
Barua hiyo ilibainisha kuwa sababu ya kuzuia kongamano hilo ni maneno yaliyozungumzwa na moja ya viongozi wa Bavicha kuelekea kongamano hilo ambayo yangeweza kusababisha uvunjifu wa amani na vurugu na hivyo kukiuka vifungu vya 6A na 9(2) vya Sheria ya Vyama vya Siasa.
Hata hivyo, viongozi wa Chadema walishikilia msimamo wa kufanya kongamano hilo.
Mara baada ya barua kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama kutolewa, Agosti 11, 2024 Jeshi la Polisi lilitoa taarifa ya kuzuia kufanyika maandamano au kusanyiko lolote kwa kigezo cha maadhimisho ya siku ya vijana Tanzania nzima ikisisitiza kuwa itawachukulia hatua kali wote watakaokiuka zuio hilo.
Kuanzia siku hiyo hiyo Jeshi la Polisi lilianza kuwakamata wafuasi na viongozi wa Chadema waliokuwa wanaelekea Mbeya kwa kukaidi amri hiyo na hadi Agosti 12, watu 520 walikuwa wamekamatwa na jeshi hilo wakiwemo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti Bara, Tundu Lissu na Katibu Mkuu John Mnyika.
Hata hivyo, Mbowe amewaeleza wanahabari leo Agosti 14, 2024 katika ofizi za chama hicho Mikocheni jijini Dar es Salaam kuwa tuhuma zilizoibuliwa na msajili msaidizi wa vyama pamoja na hatua zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi havina msingi na ni uvunjifu wa sheria.
“Tunawataka wanasheria wa Chadema haraka wakutane, kutengeneza mashtaka ya madai dhidi ya Sisty Nyahoza kama Sisty Nyahoza… tutamburuza mahakamani Awadh Haji, Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi kama Awadh,” amesema Mbowe kwa msisitizo.
Mbowe ameongeza kuwa jopo la wanasheria wa chama hicho wataongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara Tundu Lissu ambaye amesharejeshewa leseni yake ya uwakili.
Nyahoza alipotafutwa na mwandishi wa Nukta Habari kupata maoni yake juu ya mpango huo wa Chadema kumshtaki mahakamani, amesema “hana muda” na kukata simu na baadaye alipotafutwa tena ameeleza kuwa “hakuna hiyo”.
Nukta Habari haikupata maoni ya jeshi la polisi kwa wakati baada ya simu na meseji kwenda mwa Msemaji wa jeshi hilo, David Misime kutopokelewa.
Zuio la mkutano huo na kukamatwa viongozi hao wa Chadema na wafuasi wao zaidi ya 500 kutoka zaidi ya mikoa 10 limeelezwa na wachambuzi wa siasa kuwa ni miongoni matukio makubwa yanayoashiria kukandamizwa kwa demokrasia tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani.
Rais Samia amekuwa kinara wa kuimarisha demokrasia nchini baada ya kuondoa marufuku ya mikutano na kulegeza uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Mashtaka yatayofunguliwa
Awali Tundu Lissu alipokuwa akizungumza katika mkutano huo alibanisha kuwa barua iliyoandikwa na Msajili Msaidizi wa Vyama pamoja na tamko la Jeshi la Polisi si halali kwa kuwa kwa mujibu wa sheria (Mkuu wa Polisi wa Wilaya ) OCD ndiye mtu pekee aliyepewa mamlaka ya kusitisha kusanyiko la hadhara la kisiasa.
“Kwa mujibu wa sheria za Tanzania mtu pekee anayeweza kusema ni marufuku kufanya huo mkutano wako ni OCD wa eneo husika, kwa hiyo basi hiyo piga marufuku ya Kamishna Haji ipo kinyume na sheria zilizotungwa na Bunge la Tanzania,” amesema Lissu.
Lissu ameongeza kuwa miongoni mwa mashataka yatayofunguliwa ni pamoja na kuvunjwa kwa mkutano, kupigwa na kushambuliwa kwa viongozi wa chama hicho pamoja na kukamatwa na kuwekwa mahabusu pamoja na uharibifu wa mali za chama.
Kwa mujibu wa Chadema jumla ya viongozi 26 walishambuliwa kwa kupigwa na Jeshi la Polisi ambapo Mnyika na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa Joseph Mbilinyi ndio walioathirika zaidi na vipigo hivyo na kwa sasa wanaendelea na matibabu.
Latest