Zaidi ya Sh49 bilioni kutatua changamoto ya maji maeneo nje ya jiji la Mwanza

July 11, 2024 11:54 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Maeneo yatakayonufaika ni pamoja na wilaya ya Misungwi katika kata za Usagara na Wilaya ya Magu katika kata ya Kisesa.
  • Kukamilika kwa chanzo hicho kutazalisha lita za ujazo milioni 48 zitakazonufaisha zaidi ya wakazi 450, 000.

Mwanza. Zaidi ya Sh49 bilioni zimetengwa kwa ajili ya usambazaji wa maji kutoka kwenye chanzo cha maji cha Butimba kilichopo jijini Mwanza kwenda kwenye maeneo yaliyo nje ya jiji hilo ili kupunguza changamoto ya maji wanayokumbana nayo wakazi wa maeneo hayo.

Usambazaji wa maji katika maeneo hayo mkoani Mwanza unaodhaminiwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa kushirikiana na Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira (Mwauwasa).

Kupitia mradi huo maeneo ya wilaya ya Misungwi katika kata za Usagara na Wilaya ya Magu katika kata ya Kisesa zitaondokana na shida ya maji.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda aliyekuwa akizungumza na wakazi watakaonufaika na mradi huo Leo Julai 11, 2024 amesema kuwa shida ya maji katika maeneo hayo itaisha mwaka 2025.

“Hadi kufikia mwaka kesho, changamoto ya maji katika kata ya Usagara na maeneo mengine yaliyo nje ya jiji la Mwanza yatakuwa yamefikiwa na mradi huo na wananchi hawatakuwa wanahangaika na suala hilo,” amesema Mtanda.


Soma zaidi:Si kweli: video zinazoonesha mnyama wa baharini mwenye kichwa cha ng’ombe


Kukamilika kwa chanzo hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha lita za ujazo milioni 48 zitakazonufaisha zaidi ya wakazi 450, 000 wanaoishi maeneo ya milimani na nje ya jiji la Mwanza.

Mradi mwingine unaotekelezwa mkoani humo ni ni ule wa Mamlaka ya maji vijijini (RUWASA) katika eneo la Kigongo ambaoumefikia asilimia 30.

Huenda kukamilika kwa mradi huo kukaleta ahueni kwa wananchi wa maeneo hayo hususani wakazi wa kata ya Usagara na Misungwi waliokuwa wakikabiliwa na uhaba wa maji hususani kipindi cha kiangazi.

Baadhi yao walilazimika kuamka alfajiri na kutoboa mifuko yao zaidi ili kupata huduma hiyo muhimu kwa afya ya binadamu kama anavyoeleza Nyanzala Kafumu mkazi wa kijiji cha Nyangh’omango wilayani Misungwi.

“Kama huwezi kuamka alfajiri kwenda kuchota maji, itakulazimu kuandaa Sh2, 000 hadi 2,500 ili kupata maji  kwa wale wanaouza ambapo kwa ndoo moja ni Sh500,” amesema Nyanzala.

Baadhi ya wakazi kijiji cha Nyangh’omango wakichota maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya nyumbani. Picha|Mariam John.

Mkazi Mwingine, Peter Deus amesema kwa sasa mji wa Nyangh’omango na Usagara unapanuka kwakuwa na idadi kubwa ya watu wanaoishi kwenye maeneo hayo huku wawekezaji wakiwekeza vitu vingi ikiwemo shule, vyuo na viwanda lakini changamoto iliyopo ni ukosefu wa maji.

“Hatuna maji, kama haujachimba kisima nyumbani kwako basi utalazimika kusubiri yanayouzwa na vijana ambao wamejipatia ajira kwa kuuza maji, vinginevyo utalazimika kuyafuata umbali mrefu,” amesema Deus.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW