Wanakijiji wanavyosota kusaka maji usiku Mwanza-2
- Wasio na uwezo wa kifedha wapata tabu kupata maji.
- Serikali yaanza kutekeleza miradi ya maji vijijini.
Mwanza. Katika makala iliyopita tulijadili kwa kina kuhusu tatizo la maji katika Wilaya ya Misungwi na namna wananchi wanavyoamka usiku kusaka maji hayo katika kisima kimoja kinachotumiwa na zaidi ya watu 1,000. Leo tunaendelea na sehemu ya mwisho.
Maji ni gharama
Pamoja na vijana hao kujipatia ajira ya kusambaza maji lakini baadhi ya wakazi wa Kata ya Usagara wanasema ni gharama hasa kipindi hiki ambapo maisha yamepanda.
Neema Jeremiah anasema baadhi ya watu hasa wazee hawawezi kufika kisimani na wakati mwingine hawana fedha ya kununulia maji na si wazee tu hata watu wengine hawawezi kutembea umbali mrefu kufuata maji.
“Kifupi maji ni gharama, kwa kuwa kama usipotembea kuyafuata itakulazimu kuyanunua na huwezi kukwepa kwakuwa maji ndio kila kitu,” anasema Neema.
Baadhi ya watu hasa wazee hawawezi kufika kisimani na wakati mwingine hawana fedha ya kununulia maji na si wazee tu hata watu wengine hawawezi kutembea umbali mrefu kufuata maji. Picha | Mariam John.
Mkakati wa Serikali kuondoa changamoto ya maji vijijini
Wakala wa Usambazaji wa maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imekusudia kutatua changamoto ya maji katika kata ya Identemya baada ya kuanza utekelezaji wa mradi wa maji kwenye kata hiyo wenye thamani ya zaidi ya Sh5.5 bilioni.
Mradi huo ukikamilika utanufaisha wakazi katika vijiji sita vya kata hiyo ambavyo ni Kigongo, Bukumbi, Isamilo, Chole, Mayolwa na Mwasonge.
Meneja wa Mradi wa maji Kigongo, Zubeda Said anasema kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 60 ambapo baada ya kukamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha maji lita 680,000 kwa upatikanaji wa vifaa hususani mabomba ya chuma ambayo yalitakiwa kununuliwa nje ya nchi.
“Mkandarasi aliongezewa muda wa miezi sita hadi Juni mwaka huu anatakiwa awe amekabidhi kazi na maji yawepo kwenye vituo,” anasema Said.
Mpaka sasa zaidi ya Sh1.6 bilioni sawa na asilimia 30 ya fedha zote zimeshalipwa kwa malipo ya awali ya kazi.
Hata hivyo, ametaja mlolongo mrefu wa upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa mradi huo unachangia kwa kiasi kikubwa mradi kutokamilika kwa wakati ambapo kwa muda ulioongezwa huenda usikamilike.
Soma zaidi:
-
Shida juu ya shida: Uhaba wa maji unavyokwamisha vita ya Uviko-19 Singida
-
Wanakijiji wanavyosota kusaka maji usiku Mwanza
Safari bado ndefu
Pamoja na changamoto ya fedha lakini pia eneo ambapo chujio la maji linatakiwa kujengwa, mmiliki amegoma kuliachia mapaka atakapolipwa fidia.
“Kanuni ya utekelezaji wa maji inasema maji hayauzwi yanayonunuliwa ni yale ya dukani na pale kunapotekelezwa mradi wa maji eneo ambapo mradi utapita mwenye eneo anatakiwa atoe bure lakini hapa imekuwa tofauti baada ya kuanza kujenga chujio mwenye eneo alilalamika na kwenda kufungua kesi ambapo hadi sasa bado kuna mgogoro,” anasema Said.
Changamoto nyingine aliyoitaja ni upatikanaji wa mabomba ya chuma ambayo hayazalishwi nchini hadi nje ya nchi pamoja na ucheleweshwaji wa fomu za malipo.
Amewataka wakazi wa vijiji hivyo kutunza miundombinu ya maji ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kueleza ipo tabia ya baadhi ya wafugaji kurusu mifugo yao kuingia kwenye vyanzo vya maji hali inayosababisha viharibike mara kwa mara.
Changamoto nyingine ni baadhi ya wanakijiji kushindwa kutumia maji ya bomba hasa kipindi cha mvua ambapo wanalazimika kutumia ya kisima au mvua ili kupunguza gharama za kulipia.
“Unakuta mradi umekamilika na umeanza kutumika badala ya wananchi kwenda kutumia wanakinga ya mvua au kuchota kisimani hali inayosababisha kupunguza mapato, kwakuwa miradi inatumia fedha na zinatakiwa zirudi,” anasema.
Wanawake kwa wanaume wakichota maji kwenye kisima kilichopo Kijiji cha Usagara ambacho ni tegemeo pekee cha huduma hiyo Picha | Mariam John.
Wananchi wasikate tamaa neema ipo
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Misungwi, Machibya Kashinje anasema Serikali inapambana kuhakikisha inaondoa changamoto ya maji vijijini baada ya kuanza utekelezaji wa mradi huo wa Kigongo na ule wa Butimba wilayani Nyamagana.
Miradi hiyo ikikamilika kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo itaondoa changamoto ya maji kwenye maeneo hayo ambayo licha ya kuwa yapo karibu na Ziwa Victoria.
“Tunafahamu kwamba kuna changamoto ya maji kwenye kata hizo mbili lakini tayari Serikali imeanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji unaojengwa Butimba ambao ukikamilika utapeleka maji kwenye maeneo ya Usagara, Fella na Kanyerere,” anasema Kashinje.
Anasema lengo la Serikali la kumtua mama ndoo kichwani limekaribia kufikiwa ambapo hivi karibuni Meneja wa Ruwasa pamoja na Mhandisi wa Mamlaka ya Maji Safi na usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa), walifanya tathmini katika maeneo yenye changamoto ya maji ikiwemo Misungwi.
Tathmni hiyo itasaidia kuainisha maeneo ambayo vituo vya maji vitakapojengwa baada ya mradi wa maji Butimba na Usagara kukamilika.
Latest