Polisi yachunguza Mbunge Ole Sendeka kushambuliwa kwa risasi Manyara
- Alishambuliwa akiwa kwenye gari katika Kijiji cha Ngabolo Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara.
- Timu ya maafisa wa Jeshi la Polisi imeanza kuchunguza tukio hilo.
- Wananchi wataka ulinzi uimarishwe kuelekea uchaguzi.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limesema linachunguza tukio la Mbunge wa Simanjiro mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana akiwa ndani ya gari pamoja na dereva wake.
Msemaji wa Jeshi hilo David Misime katika taarifa yake iliyotolewa leo Machi 30, 2024 amesema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 29 mwaka huu katika Kijiji cha Ngabolo Wilaya ya Kiteto mkoani humo lakini hakuna aliyepata madhara.
“Polisi wanafuatilia tukio hilo kwa karibu sana kwani uchunguzi ulishaanza mara baada ya kupokea taarifa.
“Timu ya wataalamu wa uchunguzi wa matukio yaliyohusisha matumizi ya risasi kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma, imetumwa kwenda kushirikiana na timu ya Mkoa wa Manyara kuchunguza tukio hilo,” imeeleza taarifa ya Misime.
Misime amesema kuwa lengo ni kubaini waliohusika na tukio hilo na baada ya uchunguzi kukamilika watatoa taarifa kamili.
Ole Sendeka akihojiwa na televisheni ya mtandaoni ya Ayo TV leo Machi 30, 2024 amesema mpaka sasa hajawatambua watu waliomshambulia.
Soma zaidi:CAG : Wagonjwa wa afya akili hawatambuliwi Tanzania
Mbunge huyo amesema zaidi ya risasi nne zilishambulia gari hiyo lakini yeye na dereva wake wako salama na hawakupata majeraha yoyote.
Mara baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo hapo jana baadhi ya wananchi wametoa maoni mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii wakihoji hali ya usalama wa raia pamoja viongozi wao hususani katika kipindi hiki ambapo Tanzania inajiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Madiwani pamoja na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.
“Sasa kwa hali hii viongozi wetu wapo salama kweli? na kwenye uchaguzi itakuwaje jamani tunaomba muongeze ulinzi kwa raia, mali zao na ulinzi wa nchi kwa ujumla…asante,” amesema mtumiaji wa mtandao wa Instagram anayefahamika kwa jina la Lupendo Kulindwa.
Itakumbukwa kuwa Januari mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alivitaka vyombo ulinzi kuwa macho kuimarisha ulinzi na usalama hususan katika kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea katika uchaguzi.
“Mwaka huu na mwakani tunaelekea kwenye chaguzi za nchi yetu na hapa ndipo usalama mkubwa wa nchi unapoangaliwa kwa ukaribu zaidi. Niwaombe sana Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWT) kujipanga…
“…Jeshi na vikosi vyote vya ulinzi na usalama vikae tayari kwa hali yoyote itakayojitokeza,” alisema Rais Samia aliyekuwa akihutubia katika Mkutano wa Saba wa Mkuu wa Majeshi (CDF) na Makamanda wa mwaka 2024 jijini Dar es Salaam.