Wagombea wawili Chadema wauawa, polisi wakimkamata askari magereza
- Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema pia kuna taarifa za kujeruhiwa na kukamatwa kwa viongozi, wagombea, wanachama wa chama hicho.
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema viongozi wake wawili wameuawa huku kikituhumu kuwepo kwa figisu katika uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika leo zikiwemo uingizwaji wa kura kwenye vituo kinyume na taratibu.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Masuala ya Nje wa Chadema, John Mrema ameeleza katika taarifa iliyotolewa kupitia ukurasa wa X (zamani Twitter) amesema chama hicho kimepokea taarifa za vurugu na matukio ya mauaji yaliyotokea usiku wa kuamkia leo, Novemba 27, 2024.
Viongozi waliouawa, kwa mujibu wa Chadema ni pamoja na George Juma Mohamed, mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa mtaa wa Stand jimbo la Manyoni Mashariki, anayedaiwa kushambuliwa nyumbani kwake na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) usiku wa kuamkia leo. Shambulio hilo, Chadema imesema, lilisababisha mzozo mkubwa na George alifariki papo hapo baada ya kupigwa risasi na askari.
Mgombea aliyepoteza maisha ni Steven Chalamila kutoka jimbo la Tunduma ambaye alishambuliwa kwa kupigwa na mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na watu wasiojulikana na kusababisha kifo chake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Amon Kakwale amesema wanamshikilia askari mmoja wa jeshi la Magereza kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mwananchi mmoja katika tukio lililotokea Novemba 26, 2024, katika Kitongoji cha Stendi, Kata ya Mkwese, Wilaya ya Manyoni
Kakwale amesema jana wafuasi wa Chadema walivamia moja ya nyumba ambazo wafuasi wa CCM walikuwa wakifanya kikao cha ndani na kusababisha vurugu. Katika kufuatilia kilichokuwa kinajiri askari wa Jeshi la Magereza wakiwa wanawasiliana na polisi walienda eneo hilo na kisha kupokelewa na mawe.
Polisi wamshikilia askari magereza
Ili kujihami, Kakwale amesema askari hao walirusha risasi hewani kuwaonya na kuwatawanya waliokuwa wanarusha mawe hayo.
“Katika purukushani hizo, risasi moja ilimjeruhi George Juma, (41), ambaye alikuwa mgombea wa kitongoji cha Stendi kupitia Chadema. Uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea ili kufanikisha kuwakamata wale wote waliosababisha vurugu hizo,” Kakwale amesema.
Chadema imebainisha kuwa karatasi za kupigia kura zimekamatwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Chato, Kata ya Nyaruntembo, Kijiji cha Nyantimba, Mji wa Bariadi, Kata ya Malambo, Mtaa wa Nyashanda, Msalala, Kata ya Bugarama, Kijiji cha Igudija, Kilosa, na maeneo mengine katika Jimbo la Kibaha, Igunga na Segerea.
Chama hicho kimetaka TAMISEMI kutoa maelezo kwa umma kuhusu karatasi za kura zilizochafuliwa na hatua zitakazochukuliwa dhidi ya wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo hayo.
Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Mji wa Bariadi Adrian Jungu ameeleza kwenye taarifa kwa umma kuwa madai ya kuwepo kwa katarasi za kura nje ya utaratibu si ya kweli.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema wana taarifa za kujeruhiwa na kukamatwa na polisi viongozi, wagombea, wanachama na wapenzi wa chama hicho katika maeneo mbalimbali ya nchi “walipokuwa wakijitahidi kukamata na kuzuia kuingizwa vituoni kura bandia na batili zilizopigwa tayari kuwabeba wagombea wa CCM.”
“Tunataka watu wetu hawa waachiwe haraka na bila masharti yeyote,” amesema Mbowe.
Chadema imeelezea kukerwa na mauaji yaliyotokea na imewataka polisi kuchukua hatua haraka kukamata wahusika na kuwafikisha mahakamani.