Jeshi la Polisi lajipanga kuimarisha usalama kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024

September 12, 2024 5:32 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Jeshi la Polisi limetakiwa kuhakisha amani inakuwa mstari wa mbele.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limesema limejipanga kuhakikisha usalama wa wananchi wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27 mwaka huu na uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Kauli hiyo ya Jeshi la Polisi inakuja wakati kukiwa na vuguvugu la maandamano na ripoti za wananchi kutekwa na wengine kuuwawa hali inayotishia usalama kuelekea kipindi cha uchaguzi.

Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Camillus Wambura aliyekuwa akiongea katika mkutano mkuu wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi uliofanyika leo Septemba 12, 2024 mkoani Kilimanjaro amebainisha kuwa pamoja na jukumu la msingi la kulinda usalama wa raia wakati wa uchaguzi, jeshi la hilo limejikita pia kuimarisha usalama barabarani.

“Katika kuimarisha usalama barabarani nchini mikakati ya kuzui kupunguza ajali za barabarani ikiwemo kutoa elimu ya usalama barabarani  kwa watumiaji wa barabara, kufanya doria za barabarani…

…Ukaguzi wa magari na uhakiki wa leseni za madereva, kuwa na utaratibu wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani imepangwa vizuri,” amebainisha hayo IGP Wambura.

Aidha, IGP Wambura amesema kuwa kwa sasa hali ya usalama nchini ni shwari na kuwapongeza polisi, vyombo vya usalama na raia wapenda amani kuwezesha hilo na kuitaka jamii kuishi katika maadili mema ili kupunguza uhalifu huku Jeshi la Polisi likiendelea kujiimarisha.

“Jeshi la Polisi limejiimarisha vyema katika mikakati ya kuzuia uhalifu ili kuepuka madhara ya kuwashughulikia wahalifu baada ya uhalifu kutokea, hapa naomba nitoe rai kwa jamii na viongozi wa dini katika kuhakikisha wanalea familia kwa kufuata mila, desturi na misingi ya dini ili kuepuka mmomonyoko wa maadili ambao kwa tathmini ya ujumla ndio chanzo kikubwa cha uhalifu unaoendelea,”amesema IGP Wambura.

Maafisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi wakiwa katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka unaofanyika Shule ya Polisi Tanzania Moshi. /Picha Police Force Tz

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Daniel Sillo amelitaka Jeshi la Polisi kuhakisha amani inakuwa mstari wa mbele ili kufikia malengo yaliokusudiwa kuimarisha usalama nchini hasa wakati wa uchaguzi.

“Nyote mnatambua kuwa mwaka huu na mwakani ni vipindi vya uchaguzi nchini ambapo mwaka huu tuna uchaguzi wa Serikali za mitaa na mwakani itakuwa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani ni matumaini yangu makubwa kuwa mkutano huu muhimu unaojumuisha makamanda wa polisi wa mikoa na vikosi amani iwe ya mbele… 

…Mtapanga mikakati wa kuimarisha usalama wakati wa uchaguzi ili wananchi waweze kutumia haki yao ya msingi na ya kikatiba ya upigaji wa kula nchini,” amesisitiza Naibu Waziri Sillo.

Mbali na kuhakikisha umma kuhusu ulinzi na usalama wakati wa uchaguzi Jeshi la Polisi limetumia mkutano huo kujadili masuala ya kisera na kuweka mikakati ya kiutendaji iliyobebwa na  kauli mbiu  isemayo “Huduma bora za kipolisi kwa umma zitapatikana kwa kubadilika kifikra, usimamizi wa sheria na matumizi ya TEHAMA.”

Mkutano huo pia unafanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Polisi Tanzania, ambayo yatafikia kilele chake Septemba 17, 2024.  

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks