ACT-Wazalendo: Bajeti ya Wizara ya Habari 2024-2025 ina matobo na mapungufu

May 20, 2024 4:17 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Yaibua hoja saba baada ya kufanya uchambuzi wa bajeti hiyo
  • Hoja hizo ni pamoja na kupanda kwa gharama za intaneti, usalama na ulinzi wa taarifa  za kimtandao wa watumiaji.

Dar es Salaam.Chama cha ACT-Wazalendo kimesema bajeti  ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya mwaka 2024/25 ina matobo, mapungufu na haiakisi mahitaji halisi ya mawasiliano ya Watanzania.

Hatua hiyo ya ACT inakuja ikiwa imepita siku tatu tangu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye aombe Bunge liidhinishe bajeti ya Sh180 bilioni kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/25.

Rahma Mwita, Mwenyekiti Kivuli wa Wizara Ya Habari, Mawasiliao na Teknolojia ya Habari ACT-Wazalendo aliyekuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam ameainisha hoja zinazoonesha mapungufu kuwa ni pamoja na kupanda kwa gharama za intaneti.

ACT imesema katika hotuba ya bajeti hiyo Serikali haijaanisha hatua za kushughulikia changamoto za intaneti ambazo ni pamoja na kupanda kwa vifurushi licha ya Serikali kupitisha Kanuni zinazosimamia vifurushi Machi, 2021.

“Hili jambo siyo la leo wala jana… mathalani GB 1 (Gigabyte moja) inanunuliwa kwa Sh2,500 mpaka 3,000 na kasi ya kuisha kwake ni kubwa zaidi,” amesema  Waziri Kivuli Rahma.

Kwa kutambua umuhimu wa intaneti kuelekea uchumi wa kidigitali, ACT imeitaka Serikali kuanzisha mchakato wa kutengeneza upya Sera ya Mawasiliano kwa kuwashirikisha wadau, kupunguza gharama za kikodi na kutoa huduma ya intaneti katika maeneo ya umma ikiwemo shule na sokoni.


Soma zaidi:Bajeti Wizara ya Habari, Mawasiliano, Teknolojia ya Habari yapungua kwa asilimia 14


Ukosefu wa uhakika wa huduma za mawasiliano na mtandao wa simu Vijijini 

Kwa mujibu wa Rahma, Wizara ya Habari kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) haijafanya jitihada zozote kuongeza maeneo yanayofikiwa na huduma za mawasiliano pamoja na mtandao wa simu (Geographical coverage) jambo linalowafanya baadhi wa wananchi kukosa mawasiliano ya simu, intaneti, matangazo ya runinga (Tv) na redio.

Idadi ya Watanzania inayofikiwa na huduma hizo inabaki kuwa asilimia 69 sawa na ile iliyorekodiwa mwaka 2022  jambo linalowakosesha baadhi ya wananchi huduma hizo.

“ACT Wazalendo tunatoa rai kwa Serikali katika mwaka huu na miaka ijayo ihakikishe UCSAF inatengewa fedha za kutosha ili kuimarisha mtandao wa mawasiliano nchini,” amesema Rahma.

Deni la Serikali kwa vyombo vya Habari

Suala la deni la Serikali kwa vyombo vya habari ni miongoni mwa hoja zilizopewa uzito katika uchambuzi uliofanywa na ACT ambapo wameitaka Serikali kutenga angalau asilimia 0.04 ya bajeti ya wizara ya kulipa Sh19 bilioni wanayodaiwa hadi kufikia Aprili mwaka huu.

Itakumbukwa kuwa Mei 17, 2024  Waziri Nape wakati akijibu hoja za wabunge kuhusu deni hilo alisema Serikali inaangalia namna nzuri ya kuyalipa madeni hayo

Licha ya ahadi hiyo na ile iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ya Julai, 2021 ya kulipa sehemu ya deni hilo, bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari mwaka ujao haijaainisha jitihada zozote za kulipa deni hilo.

Usalama na ulinzi wa taarifa za kimtandao kwa watumiaji

Ili kupunguza malalamiko ya wananchi kuhusu matukio ya wizi wa simu, utapeli wa kimtandao, na ulaghai ACT Wazalendo imeitaka Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kuzitambua biashara za mtandaoni kisheria ili kupunguza wimbi la  matukio hayo.

Chama hicho kimebainisha kuwa Pamoja na Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kuimarisha mfumo ya kuzuia vitendo hivyo bado matukio hayo yamekuwa yakijirudia huku kukiwa na mwitikio mdogo kutoka kwa vyombo vya usalama ikiwemo Jeshi la Polisi katika kuyashughulikia.

“TCRA na Jeshi la Polisi kitengo cha makosa ya kimtandao washirikiane kwa karibu zaidi kuharakisha upatikanaji wa watu wanaofanya utapeli mtandaoni na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria haraka,” amesema Rahma wakati akitolea ufafanuzi hoja hiyo. 

Hoja nyingine zilizoibuliwa na ACT Wazalendo ni pamoja usalama na ulinzi wa taarifa za kimtandao kwa watumiaji na uwepo wa Sheria kandamizi zinazotishia Uhuru wa Habari nchini.

Chama hicho kimedai mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, Sura 229 yaliyofanywa na Bunge hayajatumia lugha rafiki itakayowawezesha watumiaji wake kuelewa kwa urahisi pia hayajashirikisha wadau kama inavyohitajika.  

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Mikakati ya Serikali kuhakikisha walimu wa VETA wanapata ajira na mikopo

Mikakati ya Serikali kuhakikisha walimu wa VETA wanapata ajira na mikopo

Nukta TV

Mama Salama alivyombana Wanu kuhusu maslahi ya walimu wanaojitolea

Mama Salama alivyombana Wanu kuhusu maslahi ya walimu wanaojitolea

Nukta TV

Kwanini uchafuzi wa mazingira ni tishio kwa afya ya binadamu na uchumi

Kwanini uchafuzi wa mazingira ni tishio kwa afya ya binadamu na uchumi

Nukta TV