Bajeti ya Wizara ya Fedha yafikia Sh18.17 trilioni, fedha za maendeleo zikipungua
- Bajeti yaongezeka kwa asilimia 14.4.
- Fedha za maendeleo zapungua kwa asilimia 2.2.
- Dk. Nchemba aanika vipaumbele vitano vya Wizara ya Fedha 2024/25.
Dar es Salaam. Wizara ya Fedha imeliomba Bunge liidhinishe kiasi cha Sh 8.13 trilioni kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 14.4 huku fedha za maendeleo zikipungua.
Mwaka 2023/2024 wizara hiyo iliidhinishiwa Sh15.87 trilioni zilizowezesha utekelezaji wa vipaumbele nane ikiwemo kujenga, kuboresha, kufungamanisha na kuhuisha mifumo ya Tehama ya usimamizi wa mapato na matumizi ya Serikali.
Bajeti ya wizara hiyo Kwa mwaka wa fedha utakaoanza Julai 2024 imeongezeka kwa Sh 2.3 trilioni huku zaidi ya asilimia 90 ya bajeti hiyo ikipangwa kulipa deni la Serikali.
“Kati ya kiasi hicho, Sh17.63 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikijumuisha huduma ya deni la Serikali Sh13.13 trilioni, mishahara Sh 946.45 bilioni, matumizi mengineyo Sh 937.30 bilioni kwa mafungu ya wizara na taasisi zake,” amesema Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2024/25 bungeni Dodoma leo Juni 4, 2024.
Aidha, huduma za mfuko mkuu imetengewa Sh 2.61 trilioni na matumizi ya maendeleo shilingi 544.05 bilioni kwa mwaka ujao wa fedha.
Fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo zitakazofanywa na wizara hiyo ni asilimia 2.9 tu ya bajeti nzima.
Licha ya kiwango kidogo kilichotengwa, fedha hizo za maendeleo zimepungua kwa asilimia 2.2 kulinganisha na Sh 556.38 bilioni iliyotengwa kwa mwaka 2023/2024.
Hiyo ni sawa na kusema fedha hizo za maendeleo kwa mwaka 2024/25 zimepungua kwa Sh12.33 bilioni jambo linaloweza kuathiri utekelezaji wa maendeleo kwa wizara na taasisi zilizo chini yake.
Soma zaidi:Tanzania kushirikiana na Korea kujenga chuo cha anga
Vipaumbele vya wizara 2024/25
Dk. Nchemba amewaambia wabunge kwa mwaka 2024/25 wizara yake itatekeleza vipaumbele vitano ikiwemo kukusanya mapato ya Sh 44.19 trilioni.
“Vipaumbele vya mafungu ya wizara ni kama ifuatavyo, kutafuta na kukusanya mapato ya shilingi trilioni 44.19 kati ya maoteo ya shilingi trilioni 49. 35 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya Serikali,” amesema Dk. Nchemba.
Katika mwaka wa fedha 2023/2024 wizara hiyo imebainisha kuwa ilikadiriwa kukusanya Sh 39.79 trilioni kati ya makadirio yote ya Serikali ya kukusanya jumla ya shilingi trilioni 44.39.
Hadi kufikia Aprili 2024 wizara hiyo ilikusanya Sh 32.49 trilioni sawa na ufanisi wa asilimia 82 ya lengo la mwaka.
Vipaumbele vingine vitakavyotekelezwa na Wizara hiyo ni kuimarisha na kusimamia mifumo ya mapato, matumizi na mali za Serikali ikiwemo IDRAS, TANCIS, MUSE, NeST, CBMS na GAMIS.
Pia Wizara ya Fedha itahudumia deni la Serikali kwa wakati na kuboresha
kanzi data ya kutunza taarifa za deni, kutoa elimu ya huduma za fedha kwa wananchi kwa lengo la kukuza huduma jumuishi za fedha nchini na kujenga uwezo kwa wakaguzi wa ndani, kamati za ukaguzi pamoja na waratibu wa usimamizi wa vihatarishi katika taasisi za umma.