Corona: Ndege za Precision Air haijasitisha safari
- Kampuni hiyo imezushiwa kusitisha safari kutokana na janga la Corona.
- Yakanusha uzushi huo na yasisitiza bado inatoa huduma.
- Precision Air ni kiungo muhimu cha usafiri wa anga Tanzania.
Dar es Salaam. Kama ulipanga au ni mteja wa usafiri wa ndege za kampuni ya Precision Air nchini Tanzania, huenda umekutana na taarifa mtandaoni inayosema kampuni hiyo inakusudia kusitisha huduma zake kutokana na kupungua kwa wateja kulikotokana na athari za janga la Corona.
Taarifa hiyo inayosambaa kupitia mtandao wa Whatsapp, Twitter pamoja na tovuti haina ukweli wowote kwa sababu uongozi wa kampuni hiyo tayari umekanusha madai hayo.
Uchunguzi uliofanywa na Nukta Fakti umebaini kwamba taarifa hiyo ilichapichwa katika tovuti ya sautikubwa.org ikiwa na kichwa ca habari kwa lugha ya Kiingereza kinachosema “Tanzania’s Precision Air to close business citing Corona effects, passenger scarcity”.
Kwa tafsiri isiyo rasmi kichwa hicho kinasema “Precision Air kufunga biashara kwa sababu ya kupungua kwa abiria kunakotokana na madhara ya Corona.
Zinazohusiana:
- Shirika la ndege la Emirates lachkua hatua dhidi ya virusi vya Corona
- Serikali yaeleza sababu kupungua usafirishaji mizigo uwanja wa ndege Mwanza
Precision Air yatoa tamko
Habari hiyo ni mwendelezo wa watu kutumia janga la Corona ambalo linaitesa duniani kutengeneza uzushi kwa malengo mbalimbali ikiwemo kuzua taharuki kwenye jamii.
Baada ya taarifa hiyo kusambaa mitandaoni, kampuni hiyo imetoa taarifa kukanusha madai hayo na imesisitiza kuwa hayana ukweli wowote na bado inatoa huduma za usafiri wa ndege kama kawaida.
“Tunakanusha madai hayo na tungependa kuujulisha umma kuwa Precision Air iko imara, inaendelea kufanya kazi na haitarajii kufunga biashara siku za hivi karibuni,” inaeleza taarifa ya kampuni hiyo iliyotolewa jana Desemba 30, 2020.
Public Notice.#YouAreWhyWeFly
#TukutaneAngani
pic.twitter.com/8XpdDBAK0O— Precision Air (@PrecisionAirTz) December 30, 2020
Hata hivyo, kampuni hiyo imekiri kuwa imepitia kipindi kigumu kama ilivyo kwa mashirika mengine ya ndege duniani kutokana na athari za janga la Corona lakini imefanikiwa kukabiliana na changamoto zote zilizoletwa na janga hilo.
“Tunaendelea kurejea katika hali ya kawaida wakati dunia ikiendelea kujiponya kutoka kwenye janga la Corona,” imesisitiza Precision Air.
Precision Air imekua kiungo muhimu cha usafiri wa anga nchini Tanzania, ambayo kwa sasa inatoa huduma sambamba na shirika la ndege la Tanzania (ATCL).
Kwa sasa kampuni hiyo inafanya safari zake katika mikoa tisa ya Tanzania ya Dar es Salaam, Arusha, Bukoba, Dodoma, Shinyanga, Kilimanjaro, Mbeya, Mtwara na Mwanza,
Pia inafanya safari zake visiwani Zanzibar na katika jiji la Nairobi nchini Kenya.
Latest